Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko amemwombolezea Edwin kutoka Nigeria ambaye amefariki dunia hivi karibuni kutokana na baridi kali, kielelezo cha utandawazi usioguswa na mahangaiko ya wengine! Baba Mtakatifu Francisko amemwombolezea Edwin kutoka Nigeria ambaye amefariki dunia hivi karibuni kutokana na baridi kali, kielelezo cha utandawazi usioguswa na mahangaiko ya wengine!  (ANSA)

Papa Francisko Amwombolezea Edwin Aliyefariki kwa Baridi, Roma!

Baba Mtakatifu Francisko amesema, tarehe 20 Januari 2021, kijana Edwin, kutoka Nigeria alikutwa amefariki dunia kwenye Viunga vya Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Katika kipindi cha miezi mitatu hivi, zaidi ya maskini na watu wasiokuwa na makazi maalum wapatao 10 wamefariki dunia kutokana na baradi kali pamoja na ugonjwa wa Corona, COVID-19.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika mzunguko mpya wa katekesi uliokuwa unanogeshwa na kauli mbiu “Uponyaji wa Ulimwengu”, Jumatano tarehe 19 Agosti 2020 alikita tafakari yake hasa kuhusu: Upendeleo kwa maskini na fadhila ya upendo. Katika roho ya Heri za Mlimani, muhtasari wa mafundisho makuu ya Kristo Yesu. Upendeleo wa pekee ni lazima utolewe kwa maskini, wenye njaa, wagonjwa, kwa wageni, kwa wale wanaonyanyaswa na kudhulumiwa, kwa wafungwa, kwa wahamiaji ambao wanadharauliwa, kwa wakimbizi au wanaofukuzwa makwao (Rej. Mt .25:31-46). Kujibu katika haki na upendo mbele ya mahitaji ya watu hawa ni juu ya kila mtu. Upendeleo kwa ajili ya maskini ni sehemu ya Mapokeo thabiti ya Mama Kanisa yanayopata chimbuko lake kwenye Heri za Mlimani, Ufukara wa Kristo Yesu pamoja na huduma yake kwa maskini katika sura zake mbali mbali. Kristo Yesu mwenyewe alijilinganisha na maskini! Kumbe, Kanisa ni chombo cha faraja, utetezi na ukombozi kwa ajili ya maskini. Ikumbukwe kwamba, maskini ni walengwa wakuu wa Habari Njema ya Wokovu inayopaswa kutangazwa na kushuhudiwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili.

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko, wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Dominika ya Neno la Mungu, tarehe 24 Januari 2021, alirejea tena kwenye tukio la tarehe 20 Januari 2021. Kijana Edwin, kutoka Nigeria alikutwa amefariki dunia kwenye Viunga vya Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Katika kipindi cha miezi mitatu hivi, zaidi ya maskini na watu wasiokuwa na makazi maalum wapatao 10 wamefariki dunia kutokana na baradi kali pamoja na ugonjwa wa Corona, COVID-19. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusali kwa ajili ya kumkumbuka na kumwombea Marehemu Edwin pamoja na wale wote waliofariki dunia katika mazingira ya baridi ya kutisha pamoja na magonjwa nyemelezi. Mtakatifu Gregori Mkuu aliwahi kusema, ikiwa kama maskini na mtu asiye kuwa na makazi anafariki dunia kutokana na baridi kali, basi, siku hiyo hakuna sababu ya kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwani ni sawa na Ijumaa kuu.

Marehemu Edwin katika umri wa miaka 46 amepoteza maisha kutokana na baridi kali, akapuuzwa na watu wengi waliokuwa wanapita katika njia ile hata na viongozi wa Kanisa. Kutokana na sababu zilizokuwa nje ya uwezo wake, Baba Mtakatifu Francisko, Dominika ya Neno la Mungu, tarehe 24 Januari 2021 hakuweza kushiriki wala kuongoza na badala yake Ibada hii ya Misa Takatifu iliyoadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican imeongozwa na mahubiri kusomwa kwa niaba yake na Askofu mkuu Salvatore Rino Fischella, Rais wa Baraza la Kipapa la Uhamasishaji wa Uinjilishaji Mpya. Baada ya maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, Baba Mtakatifu akiwa kwenye makazi yake yaliyoko kwenye Hosteli ya Santa Marta, mjini Vatican amekabidhi Biblia Toleo Maalum kwa baadhi ya waamini walioshiriki katika Ibada ya Misa Takatifu Dominika ya Neno la Mungu kwa Mwaka 2021 ambayo imenogesgwa na kauli mbiu “Mkishika neno la uzima”. Flp. 2:16.

Kifo cha Edwin

 

25 January 2021, 16:10