Tafuta

Vatican News
Papa Francisko: Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo: 18 - 25 Januari, Sikukuu ya Wongofu wa Mtakatifu Paulo, Mtume na Mwalimu wa Mataifa: Umoja wa Wakristo. Papa Francisko: Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo: 18 - 25 Januari, Sikukuu ya Wongofu wa Mtakatifu Paulo, Mtume na Mwalimu wa Mataifa: Umoja wa Wakristo. 

Papa Francisko: Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo: 18-25 Januari

Kauli mbiu kwa Mwaka 2021: “Kaeni katika pendo langu, ili mzae matunda”. Rej. Jn 15-5-9. Kristo Yesu ndiye Mzabibu wa kweli ni ufafanuzi unaotolewa katika Injili ya Yohane 15:1-17. Jumuiya ya Wamonaki 50 kutoka katika Makanisa na Madhehebu mbalimbali ya Kikristo wa Grandchamp iliyoko nchini Uswisi ndiyo iliyopewa dhamana ya kuandaa masomo, sala na tafakari kwa 2021.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili tarehe 17 Januari 2021 kutoka kwenye Maktaba yake binafsi mjini Vatican, amewakumbusha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kwamba, Jumatatu tarehe 18 Januari hadi tarehe 25 Januari, Wakristo sehemu mbalimbali za dunia, wanasali kwa ajili ya kuombea Umoja wa Wakristo. Baba Mtakatifu anatarajia kuhitimisha Juma hili kwa Sala ya Masifu ya Jioni, yatakayoadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Paulo, Nje ya Kuta za Roma. Hili ni tukio litakalowashirikisha viongozi wa Makanisa na Jumuiya mbalimbali za Kikristo, wanaoishi hapa mjini Roma. Huu ni mwaliko kwa Wakristo wote kuendelea kusali, ili hatimaye, ile hamu ya Kristo Yesu, ili wote wawe wamoja iweze kutimia. Umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu! Umoja una nguvu zaidi kuliko kinzani na misigano ya kidini! Wakristo sehemu mbalimbali za dunia wanakumbushwa kwamba, jitihada za kuombea umoja wa Wakristo ni mchakato endelevu unaopaswa kutekelezwa katika hija ya kila siku ya maisha ya mwamini katika kipindi cha mwaka mzima.

Lakini Makanisa yametenga kuanzia tarehe 18 Januari hadi tarehe 25 Januari. Hizi ni siku ambamo Mama Kanisa anakumbuka Ukulu wa Mtakatifu Petro inayoadhimishwa hapo tarehe 22 Februari kila mwaka na tarehe 25 Januari, Sikukuu ya Kuongoka kwa Mtakatifu Paulo, Mtume na Mwalimu wa Mataifa kuwa ni Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo; tukio ambalo lilianzishwa kunako Mwaka 1908 na Paul Wattson. Baraza la Makanisa Ulimwenguni, WCC., kwa kushirikiana na Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo tangu mwaka 1968 hutayarisha masomo, sala na tafakari kwa ajili ya kuombea umoja wa Wakristo.  Masomo, sala na tafakari hizi zinaweza kutungwa pia kadiri ya hali na mazingira ya Makanisa husika ili kukoleza zaidi ari, moyo na majadiliano ya kiekumene miongoni mwa Wakristo, daima wakijitahidi kusoma alama za nyakati. Wakristo wanapaswa kutangaza fadhili za Mungu katika maisha yao huku wakiendelea kuambata huruma na upendo wa Mungu hasa katika kipindi hiki ambacho kuna maambukizi makubwa ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19.

Kauli mbiu inayoongoza maadhimisho ya Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo kwa Mwaka 2021 ni “Kaeni katika pendo langu, ili mzae matunda”. Rej. Jn 15-5-9. Kristo Yesu ndiye Mzabibu wa kweli ni ufafanuzi unaotolewa katika Injili ya Yohane 15:1-17. Jumuiya ya Wamonaki 50 kutoka katika Makanisa na Madhehebu mbalimbali ya Kikristo wa Grandchamp iliyoko nchini Uswisi ndiyo iliyopewa dhamana ya kuandaa masomo, sala na tafakari kwa mwaka 2021. Tema hii ni kielelezo cha wito wao unaojielekeza kwa namna ya pekee katika sala, upatanisho na umoja wa Makanisa sanjari na familia kubwa ya binadamu katika ujumla wake. Wamonaki hawa wanarutubisha maisha na utume wao kwa njia ya: sala ukimya na tafakari ya Neno la Mungu. Ni Wamonaki ambao kwa miaka mingi wamekuwa na mahusiano ya karibu na Jumuiya ya Kiekumene ya Taizè chini ya uongozi wa Padre Paul Coururier, maarufu sana katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene. Wamonaki hawa wanapenda kukazia mambo makuu matatu: Sala, Maisha ya Kijumuiya na Ukarimu, ili kubaki pamoja na Kristo Yesu, ili hatimaye, kuvuka vikwazo vya utengano miongoni mwa Makanisa.

Huu ni mwaliko wa kumsikiliza kwa makini Kristo Yesu na kuendelea kuwa karibu naye, ili kutekeleza ile Amri kuu ya Upendo kwa Mungu na jirani. Maisha ya kijumuiya si tatizo linalohitaji ufumbuzi, bali ni fumbo na changamoto katika maisha. Wamonaki hawa wanataka kuiga na kufuata mfano wa maisha ya Fra Roger, Muasisi wa Jumuiya ya Kiekumene ya Taizè. Hakuna upendo na urafiki wa kweli, ikiwa kama hakuna mateso yanayotoka moyoni na wala hakuna upendo kwa jirani, ikiwa kama hakuna Msalaba. Kumbe, ni wajibu na dhamana ya Wakristo kutambua changamoto kubwa inayoendelea kusababishwa na mipasuko ya Makanisa ya Kikristo. Hii ni kashfa inayowapelekea Wakristo wengi kulikimbia Kanisa. Mchakato wa upatanisho unahitaji nguvu na sadaka, ili “Wote wawe na umoja; kama wewe, Baba, ulivyo ndani yangu, nami ndani yako; hao nao wawe ndani yetu; ili ulimwengu upate kusadiki ya kwamba wewe ndiwe uliyenituma. Nami utukufu ule ulionipa nimewapa wao; ili wawe na umoja kama sisi tulivyo umoja. Mimi ndani yao, nawe ndani yangu, ili wawe wamekamilika katika umoja; ili ulimwengu ujue ya kuwa ndiwe uliyenituma, ukawapenda wao kama ulivyonipenda mimi”. Jn. 17:21-23.

Waamini wakiwa wamebaki huku wameungana na Kristo Yesu wanaweza kupata nguvu, hekima na busara ya kupambana dhidi ya mifumo yote inayosababisha dhuluma, nyanyaso na ukosefu wa haki msingi za binadamu. Waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanapaswa kutambua kwamba, wote ni ndugu wamoja katika udugu wa kibinadamu. Watambue kwamba, kama Wakristo, wao ni vyombo na mashuhuda wanaoitwa na kutumwa kutangaza ulimwengu mpya unaosimikwa katika haki, amani na upendo; kwa kuheshimiana na kuthaminiana sanjari na kuwa wamoja na kila kiumbe. Watawa wanasali na kutekeleza utume wao, ili hatimaye, siku moja Mwenyezi Mungu aweze kutawala maisha ya waja wake, “Ili wote wawe na umoja” (Yn 17:21). Huu ni mwelekeo wa sala unaomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya waamini, ili wote waweze kuwa wamoja. Makanisa mbalimbali ya Kikristo katika Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo yanaandaa mahali pa kukutanika kwa sala na tafakari ya Neno la Mungu, ingawa kwa mwaka huu, kutokana na maambukizi makubwa ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 maadhimisho haya yanafanyika kwa njia za mawasiliano na mitandao ya kijamii.

Umoja wa Wakristo
17 January 2021, 15:38