Tafuta

Nia za Baba Mtakatifu Francisko kwa Mwezi Januari 2021: Huduma ya udugu wa kibinadamu, kwa kukazia mambo msingi katika maisha ya waamini wote, ili kuona sura na mfano wa Mungu kwa kila mtu! Nia za Baba Mtakatifu Francisko kwa Mwezi Januari 2021: Huduma ya udugu wa kibinadamu, kwa kukazia mambo msingi katika maisha ya waamini wote, ili kuona sura na mfano wa Mungu kwa kila mtu! 

Nia za Baba Mtakatifu Mwezi Januari 2021: Huduma ya Udugu wa Kibinadamu!

Nia za Baba Mtakatifu Francisko kwa Mwezi Januari 2021: Watu wote wanahamasishwa kujielekeza katika huduma ya udugu wa kibinadamu. Papa anawaalika waamini kutoka katika dini, tamaduni na imani mbalimbali kurejea tena katika mambo msingi: upendo kwa jirani. Huu ni ujumbe unaopania kukabiliana na changamoto mamboleo ambazo zinazoikabili familia ya binadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” umegawanyika katika sura nane: Sura ya Kwanza: Wingu jeusi limetanda duniani, hapa anagusia magonjwa jamii na changamoto zake katika ulimwengu mamboleo. Sura ya Pili ni kuhusu wageni njiani, Msamaria mwema anawekwa mbele ya walimwengu kuwa ni mfano bora wa kuigwa katika kutangaza na kushuhudia Injili ya upendo kwa maskini. Sura ya Tatu ni kuhusu mwono wa ulimwengu wazi, sehemu hii inajikita zaidi katika maisha ya kiroho, mshikamano wa kidugu, utu, heshima na haki msingi za binadamu. Sura ya Nne, Moyo uliofungukia ulimwengu wote, hapa changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani, utawala bora, ushirikiano na mshikamano katika kukabiliana na changamoto mamboleo ni mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele cha pekee. Sura ya Tano, ni kuhusu siasa safi zaidi kwa ajili ya huduma kwa jamii, maendeleo, ustawi na mafao ya wengi; utu, haki msingi za binadamu na umuhimu wa kufanya mageuzi makubwa kwenye Umoja wa Mataifa ili kweli uweze kuwa ni “familia ya Mataifa”.

Baba Mtakatifu katika Sura ya Sita anajielekeza zaidi katika mchakato wa majadiliano na urafiki ili kujenga sanaa ya watu kukutana. Katika sura ya Saba, Baba Mtakatifu anapembua kuhusu makutano yaliyopyaishwa ili kujenga misingi ya haki na amani; msamaha kwa kuondokana na “dhana ya vita ya haki na halali” ambayo kwa sasa imepitwa na wakati kama ilivyo pia kwa adhabu ya kifo, kwani inakwenda kinyume cha haki msingi za binadamu, utakatifu na zawadi ya maisha kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu anapinga kwa nguvu zote utamaduni wa kifo! Sura ya Nane inakita maudhui yake katika dini na udugu; umuhimu wa dini kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu na kwamba, Kanisa litaendelea kujizatiti katika mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu kwa kuzingatia kanuni msingi za Kiinjili. Mwishoni wa Waraka huu wa kitume, Baba Mtakatifu anagusia mambo msingi yanayofumbatwa katika Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu iliyotiwa saini kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar, ulioko mjini Kairo, nchini Misri, tarehe 4 Februari 2019 huko Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu.

Baba Mtakatifu Francisko katika nia zake za jumla kwa Mwezi Januari 2021 kwa njia ya video inayosambazwa na Mtandao wa Utume wa Sala Kimataifa, anapenda kukita ujumbe wake katika huduma ya udugu wa kibinadamu. Watu wote wanahamasishwa kujielekeza katika huduma ya udugu wa kibinadamu. Papa anawaalika waamini kutoka katika dini, tamaduni na imani mbalimbali kurejea tena katika mambo msingi yaani upendo kwa jirani. Huu ni ujumbe unaopania kukabiliana na changamoto mamboleo ambazo zinazoikabili familia ya binadamu. Hizi ni changamoto zinazoweza kupatiwa ufumbuzi ikiwa kama watu watajenga umoja na mshikamano kwa kutambua kwamba, wao ni ndugu wamoja, licha ya tofauti zao msingi za kiimani, kitamaduni na Kimapokeo. Jumuiya ya mwanadamu inaweza kujenga jamii inayoshikamana au vinginevyo kesho ya mwanadamu itakuwa mashakani. Dini na madhehebu mbalimbali duniani, yanayo dhamana ya ujenzi wa madaraja yanayowakutanisha watu na tamaduni zao. Watu wote wanapaswa kutambua kwamba, wao ni watoto wa Baba mmoja na kamwe wao si watoto yatima, kumbe, wote wanaweza kuishi kwa amani. Tofauti za kidini, kiimani na Kimapokeo, kamwe zisiwe ni sababu za kushindwa kufikia utamaduni wa watu kukutana, kwa sababu wote ni ndugu wamoja wanaosali!

Baba Mtakatifu Francisko anakazia umuhimu wa fadhila ya imani kwa kutambua kwamba, kwa Wakristo, utu, heshima na haki msingi za binadamu zinapata chanzo chake kutoka katika Injili ya Kristo Yesu, changamoto na mwaliko kwa waamini kuchuchumilia na kuambata mambo msingi katika imani yaani: Uchaji kwa Mwenyezi Mungu na upendo kwa jirani. Waamini wa dini mbalimbali duniani wanaweza kuwa na vyanzo vyao vingine, lakini kwa Wakristo utu na udugu wa kibinadamu umesimikwa katika Injili ya Kristo Yesu. Kwa upande wake, Padre Frederic Fornos, SJ., Mkurugenzi wa Mtandao wa Utume wa Sala Kimataifa anapenda kukazia nia za Baba Mtakatifu Francisko kwa Mwezi Januari 2021, kwa kutambua madhara makubwa yaliyosababishwa na homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, VOVID- 19 hasa katika mfumo wa sekta ya afya duniani na katika masuala ya kijamii na kiuchumi. Nia ya Baba Mtakatifu Francisko inawawezesha watu kuchukuliana kama ndugu wamoja, kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa haki, amani na maridhiano kati ya watu. Dhamana na wajibu wa dini na madhehebu mbalimbali ni kubwa sana katika mchakato huu.

Baba Mtakatifu amefanya rejea katika Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu iliyotiwa mkwaju kati yake na Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar, ulioko mjini Kairo, nchini Misri, tarehe 4 Februari 2019 huko Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu. Sura ya Nane ya Hati hii, inakita maudhui yake katika dini na udugu; umuhimu wa dini kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu na kwamba, Kanisa litaendelea kujizatiti katika mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu kwa kuzingatia kanuni msingi za Kiinjili. Waamini wa dini mbalimbali wanahimizwa kuheshimiana kwani wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na kwa hiyo ni watoto wateule wa Mungu. Mtazamo huu utasaidia kwa kiasi kikubwa katika mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu kwa kulinda haki ndani ya jamii. Binadamu wote walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu wana haki, wajibu na utu sawa na wanahimizwa kuishi pamoja kama ndugu wamoja katika nyumba ya wote. Kimsingi udugu wa kibinadamu unaheshimu na kuthamini tofauti mbali mbali zinazojitokeza kati yao kama mtindo wa maisha ya Ufalme wa Mungu.

Papa Nia Januari

 

09 January 2021, 15:52