Tafuta

Papa Francisko: Mkataba wa Kimataifa wa Kupinga Matumizi ya Silaha za Nyuklia, TPNW unaanza kutumika rasmi tarehe 22 Januari 2021. Vatican tayari imetia saini mkataba huu. Papa Francisko: Mkataba wa Kimataifa wa Kupinga Matumizi ya Silaha za Nyuklia, TPNW unaanza kutumika rasmi tarehe 22 Januari 2021. Vatican tayari imetia saini mkataba huu. 

Mkataba wa Kimataifa Kupinga Silaha za Nyuklia: 22 Januari 2021

Papa Francisko: Tarehe 22 Januari 2021, Mkataba wa Kimataifa wa Kupinga Matumizi ya Silaha za Nyuklia, TPNW, ambao umeridhiwa na Mataifa zaidi 50 utaanza kutumika rasmi. Huu ni Mkataba wa Kimataifa unaopiga rufuku utengenezaji, ulimbikizaji na matumizi ya silaha za nyuklia kwani matumizi ya silaha hizi hayana macho wala pazia, na hayawezi kuchagua wala kubagua! AMANI!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maendeleo na hatimaye, utengenezaji, usambazaji na matumizi ya silaha za nyuklia ni mambo ambayo yako kinyume kabisa cha moyo na tunu msingi za Umoja wa Mataifa. Kutokana na mwelekeo huu, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, Mkataba wa udhibiti wa utengenezaji, usambazaji na matumizi ya silaha za nyuklia unatekelezwa pamoja na kupiga rufuku utengenezaji wa mabomu ya atomic. Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Katekesi yake, Jumatano tarehe 20 Januari 2021 amesema kwamba Ijumaa tarehe 22 Januari 2021, Mkataba wa Kimataifa wa Kupinga Matumizi ya Silaha za Nyuklia, TPNW, ambao umeridhiwa na Mataifa zaidi 50 utaanza kutumika rasmi. Huu ni Mkataba wa Kimataifa unaopiga rufuku utengenezaji, ulimbikizaji na matumizi ya silaha za nyuklia. Hii inatokana na ukweli kwamba, matumizi ya silaha hizi hayana macho wala pazia, na hayawezi kuchagua wala kubagua! Katika kipindi kifupi tu, matumizi ya silaha hizi yanaweza kusababisha maafa makubwa na yatakayodumu kwa muda mrefu kwa binadamu na mazingira yake.

Baba Mtakatifu ametumia fursa hii, kutoa wito kwa Mataifa ambayo bado hayajaridhia Mkataba huu, kushiriki na kuendelea kufanya kazi kwa pamoja ili kuhakikisha kwamba, dunia inakuwa ni mahali pa salama pasi na silaha za nyuklia, ili kuchangia katika mchakato wa kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani, ushirikiano na mshikamano wa Jumuiya ya Kimataifa unaohitajika sana kwa wakati huu! Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu, Jumapili, tarehe 24 Novemba 2019 alizungumzia kuhusu mateso na maafa makubwa yaliyosababishwa na mashambulizi ya mabomu ya atomiki, changamoto na mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete kulinda na kudumisha misingi ya: usalama, amani na utulivu kwa kuondokana na wasi wasi pamoja na hofu inayotawala akilini na nyoyoni mwa watu kiasi cha kushindwa kuaminiana, na hivyo, kudhohofisha mafungamano ya watu wa Mataifa pamoja na mchakato wa majadiliano. Amani na utulivu wa kimataifa vinaweza kujengeka katika msingi wa mshikamano na ushirikiano wa haki kwa ajili ya huduma kwa kutambua kwamba, watu wanategemeana na kukamilisha; na wanapaswa kuwajibika kama wamoja kwa ajili ya ustawi wa familia nzima ya binadamu.

Baba Mtakatifu anasema, Nagasaki ni mji ambao umeshuhudia maafa makubwa kwa binadamu sanjari na uharibifu wa mazingira nyumba ya wote; kielelezo cha mashindano ya utengenezaji wa silaha za maangamizi; upotevu mkubwa wa rasilimali fedha ambayo ingeweza kutumika kuchochea maendeleo fungamani ya binadamu pamoja na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Rasilimali fedha inayotumika kwa ajili ya kutengeneza, kuboresha na kuhifadhi na hatimaye, kuuza silaha za maangamizi, nyuma yake kuna kilio cha watoto na familia nyingi duniani. Watu wanatamani amani ya kudumu ili kuondokana na vitisho vya silaha za maangamizi na kwamba, hii ni changamoto inayowahusisha watu wote; kwa kujenga na kudumisha utamaduni wa kuaminiana na wala si katika tabia ya kupimana nguvu. Kuna haja ya kudhibiti biashara ya silaha kimataifa na maendeleo makubwa ya teknolojia kuhusu masuala ya kijeshi. Hii ni dharura inayohitaji kushughulikiwa na viongozi wote wa Jumuiya ya Kimataifa. Baba Mtakatifu alikaza kusema, Kanisa Katoliki kwa upande wake, litaendelea kuhimiza umuhimu wa watu wa Mataifa kudumisha amani.

Kanisa linaunga mkono Kanuni ya Sheria ya Kimataifa kuhusu Silaha za Nyuklia, ikiwa ni pamoja na Mkataba wa Kimataifa wa kupiga rufuku utengenezaji, ulimbikizaji na matumizi ya silaha za kinyuklia duniani. Amani ni kazi ya haki na matunda ya upendo! Amani inatishiwa sana na mashindano ya silaha; utengenezaji na biashara ya silaha pamoja na mchakato wa ulimbikizaji wa silaha duniani! Ni wajibu wa Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha amani ambalo ni jina jipya la maendeleo fungamani ya binadamu! Baba Mtakatifu anasema, dunia bila kuwa na silaha za kinyuklia inawezekana kabisa na ni muhimu sana na kwamba, silaha hizi za maangamizi kamwe haziwezi kuwasaidia viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kuwa na uhakika wa usalama wa raia na mali zao kitaifa na kimataifa. Kuna haja ya kufanya upembuzi yakinifu kuhusu madhara yake katika maisha ya watu sanjari na mazingira; kwa kuondoa hofu, mazingira ya kutoaminiana, chuki na uhasama vinavyozungumza “dhana ya silaha za nyuklia”.

Jumuiya ya Kimataifa haina budi kujielekeza zaidi katika kubuni sera na mikakati itakayosaidia utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ifikapo mwaka 2030. Kunako mwaka 1964, Mtakatifu Paulo VI alishauri kuanzishwa kwa Mfuko wa Maendeleo kwa Nchi Maskini, ambao ungechangiwa kwa kuchukua sehemu ya bajeti ya serikali mbali mbali kwa ajili ya matumizi ya kijeshi. Kumbe, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kutengeneza mazingira ya kuaminiana, kwa sababu hii ni changamoto pevu kwa Jumuiya ya Kimataifa. Umefika wakati wa kusikiliza na kujibu kilio cha maskini kutoka sehemu mbali mbali za dunia, kwa kujenga na kuimarisha utamaduni wa majadiliano; toba na wongofu wa ndani, ili utamaduni wa uhai, upatanisho na udugu viweze kutawala katika akili na nyoyo za watu.

Wakati huo huo, Bwana Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amezipongeza nchi ambazo zimeridhia Mkataba wa Kimataifa wa Kupinga Matumizi ya Silaha za Nyuklia, TPNW. Hizi ni juhudi zilizosimamiwa kidete na asasi za kiraia katika mchakato wa kuandaa mazungumzo na kuhakikisha kwamba makubaliano yanafikiwa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Jumuiya ya Kimataifa katika ujumla wake. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema mkataba huu unaanza kutekelezwa rasmi tarehe 22 Januari 2021, kilele cha harakati za Jumuiya ya Kimataifa za kuwakumbusha watu juu ya madhara makubwa kwa binadamu kutokana na matumizi ya silaha za nyuklia. Kuna watu ambao wameathirika sana kutokana na milipuko ya nyuklia sanjari na majaribio ya silaha hizo. Watu hawa ambao wameonja madhara yake wamekuwa ni miongoni mwa watu waliosimama kidete kuutetea mkataba huu. Umoja wa Mataifa unalenga kuwaondolea watu hofu ya maafa makubwa kwa binadamu kutokana na matumizi ya silaha za nyukilia duniani.

Mkataba wa Nyuklia
20 January 2021, 16:01