Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko anawahamasisha Wakristo kumwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuwakirimia zawadi ya umoja kama ushuhuda wenye mvuto na mashiko katika mchakato wa uinjilishaji mpya. Baba Mtakatifu Francisko anawahamasisha Wakristo kumwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuwakirimia zawadi ya umoja kama ushuhuda wenye mvuto na mashiko katika mchakato wa uinjilishaji mpya. 

Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo: Ushuhuda Wa Wakristo!

Baba Mtakatifu Francisko amewahamasisha Wakristo kusali na kumwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuwakirimia wafuasi wa Kristo Yesu, zawadi ya umoja. Na kwa njia hii, wataweza kutangaza na kushuhudia Injili kwa ajili ya wokovu wa walimwengu wote. Pale inapowezekana Wakristo washirikiane na waamini wa Makanisa na Madhehebu mbalimbali ya Kikristo kwa sala! Ushuhuda!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Uinjilishaji mpya unaotekelezwa na Mama Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo unajikita katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene na kidini ili kujenga na kudumisha: utu, heshima, haki msingi za binadamu, ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu katika ujumla wao. Baba Mtakatifu Francisko anakazia uekumene wa: damu, maisha ya kiroho, sala na huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Ikumbukwe kwamba, uekumene wa utakatifu wa maisha unafumbatwa katika toba na wongofu wa ndani; kwa kujikana na kujivika fadhila ya unyenyekevu; moyo wa ukarimu na udugu wa kibinadamu; upole, unyoofu, uvumilivu na kutumikia katika upendo bila ya kujibakiza. Wakristo wanakumbushwa kwamba, kadiri wanavyojitahidi kuishi maisha matakatifu mintarafu Injili, ni kwa kadiri ile ile wataweza kuhamasishana kutekeleza mchakato wa ujenzi wa umoja wa Wakristo na udugu kati yao. Uekumene wa damu unajikita katika ushuhuda wa imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake.

Baba Mtakatifu katika katekesi yake kuhusu umuhimu wa sala kwa ajili ya kuombea umoja wa Wakristo Jumatano tarehe 20 Januari 2021, amewahamasisha Wakristo kusali na kumwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuwakirimia wafuasi wa Kristo Yesu, zawadi ya umoja. Na kwa njia hii, wataweza kutangaza na kushuhudia Injili kwa ajili ya wokovu wa walimwengu wote. Pale inapowezekana Wakristo washiriki katika sala ya kiekumene, kwa kushirikiana na waamini wa madhehebu mbalimbali Ni wajibu na dhamana kwa waamini kuomba nguvu ya Roho Mtakatifu, ili aweze kuimarisha mchakato wa umoja wa Wakristo, ili waweze kushikamana na Kristo Yesu pamoja na ndugu zao Wakristo, ili kweli waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda upendo wenye huruma katika ulimwengu mamboleo. Hii ni changamoto kwa Wakristo kuendelea kumjifunza na kumuiga Kristo Yesu katika upole na unyenyekevu, ili kweli waweze kuwa ni mashuhuda na vyombo vya ukweli na upendo!

Baba Mtakatifu amewakumbuka na kuwaombea wazee, vijana wa kizazi kipya pamoja na wanandoa wapya. Amewataka wawe mstari wa mbele kusali na kuombea umoja wa Wakristo, ili wote wawe na umoja katika imani moja ya Kanisa lililoanzishwa na Kristo Yesu, ili wote wawe wamoja! Kwa masikitiko makubwa, Baba Mtakatifu Francisko anasema, katika nyakati hizi za maambukizi makubwa ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID, -19, sala zake anapenda kuzielekeza zaidi kwa wagonjwa na waathirika wa Corona, COVID-19. Kwa namna ya pekee kabisa, Baba Mtakatifu ameyaelekeza mawazo yake huko nchini Brazil na kwa namna ya pekee huko Manaus nchini Brazil, Kaskazini mwa Brazil, ambako takwimu zinaonesha kwamba, watu wengi wameambukizwa na kuathirika vibaya na Virusi vya Corona, COVID-19. Wote hawa anawaombea baraka kwa Mwenyezi Mungu, mwingi wa huruma na faraja, aweze kuwalinda na kuwatunza katika kipindi hiki tete katika maisha ya watu wengi duniani.

Papa: Ushuhuda

 

20 January 2021, 15:12