Tafuta

Vatican News
Dominika ya Neno la Mungu: Baba Mtakatifu Francisko amekazia maneno ya Kristo Yesu: Wakati umetimia, tubuni na kuiamini Injili kama kauli mbiu, dira na mwelekeo wa Kristo Yesu katika maisha na utume wake. Dominika ya Neno la Mungu: Baba Mtakatifu Francisko amekazia maneno ya Kristo Yesu: Wakati umetimia, tubuni na kuiamini Injili kama kauli mbiu, dira na mwelekeo wa Kristo Yesu katika maisha na utume wake.  (ANSA)

Dominika ya Neno la Mungu: Ufalme wa Mungu Na Wongofu!

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Dominika ya Neno la Mungu: esu alikwenda mjini Galilaya akihubiri Habari Njema ya Wokovu kwa kusema, “Wakati umetimia, na Ufalme wa Mungu umekaribia; tubuni, na kuiamini Injili”. Mk. 1:15. Mambo makuu mawili yanapewa kipaumbele cha kwanza na Kristo Yesu katika maisha na utume wake: Wakati na Toba!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Yohane Mbatizaji katika maisha na utume wake, alitangaza na kushuhudia Ubatizo wa toba na maondoleo ya dhambi. Akawataka watu kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu na hivyo, kuanza kutembea katika mwanga wa maisha mapya, kama njia makini ya kumpokea Masiha wa Bwana, atakayetambulika kwa uwepo wa Roho Mtakatifu juu yake na huyu ndiye atakayebatiza kwa Roho Mtakatifu. Wakati ulipotimia Yesu akajitokeza hadharani kando ya Mto Yordani, baada ya kukaa nyumbani kwao mjini Nazareti kwa muda wa miaka thelathini, ili aweze kubatizwa. Baada ya kubatizwa, Roho Mtakatifu akamshukia Yesu na mara sauti kutoka mbinguni ikasikika ikisema, “Huyu ni Mwanangu mpendwa wangu msikieni yeye”, alama ambayo Yohane Mbatizaji alikuwa akiisubiria na kwamba, Kristo Yesu ni Masiha wa Bwana.

Kristo Yesu alijionesha kama Mwanakondoo wa Mungu anayeichukua na kuiondoa dhambi ya ulimwengu. Yohane Mbatizaji ndiye aliyemtambulisha Kristo Yesu kuwa ndiye Mwanakondoo wa Mungu na wale wanafunzi wa kwanza wa Yohane Mbatizaji wakawa ni wafuasi wa kwanza wa Kristo Yesu. Kwa hakika Yohane Mbatizaji alitangulia kumwandalia Kristo Yesu njia na kumtambulisha wakati ulipowadia. Hata baada ya Yohane kutiwa gerezani, Kristo Yesu alikwenda mjini Galilaya akihubiri Habari Njema ya Wokovu kwa kusema, “Wakati umetimia, na Ufalme wa Mungu umekaribia; tubuni, na kuiamini Injili”. Mk. 1:15. Mambo makuu mawili yanapewa kipaumbele cha kwanza na Kristo Yesu katika maisha na utume wake: Wakati na Toba!

Huu ni muhtasari wa tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Dominika ya Neno la Mungu, tarehe 24 Januari 2021 kutoka kwenye Maktaba Binafsi ya Baba Mtakatifu iliyoko mjini Vatican. Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu hakuweza kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu Dominika ya Neno la Mungu na badala yake, Ibada hii ya Misa Takatifu imeadhimishwa na Askofu mkuu Salvatore Rino Fischella, Rais wa Baraza la Kipapa la Uhamasishaji wa Uinjilishaji Mpya. Wakati umetimia mintarafu Injili ya Marko ni kielelezo cha Kipindi cha Historia ya Wokovu kama ilivyotekelezwa na Mwenyezi Mungu na kwamba, sasa wakati umetimia na Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, amemtuma Mwanaye wa pekee, Kristo Yesu ili kuja kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti, kwa kuanzisha Ufalme wa Mungu ambao uko karibu sana na waja wake. Lakini, ikumbukwe kwamba, wokovu “si sawa na maji kwa glasi” bali ni zawadi ya upendo wa Mungu inayohitaji jibu makini linalofumbatwa katika toba na wongofu wa ndani.

Huu ni mchakato wa kubadili mawazo, maisha kwa kuondokana na malimwengu, tayari kumfuata Mwenyezi Mungu ambaye amejifunua kwa njia ya Kristo Yesu. Haya ni mabadiliko makubwa ya mtazamo na maelekeo ya watu. Uwepo wa dhambi na matokeo yake duniani, umepelekea tabia ya watu kutaka “kujikweza na kujimwambafai”, kwa kuwadharau wengine na hata kutoona umuhimu wa Mwenyezi Mungu katika maisha. Ni katika muktadha huu, watu wanajikuta wakitumbukia katika uwongo na matumizi ya nguvu, uchu wa mali na madaraka. Kristo Yesu anawaalika waja wake, kujitambua kwamba, wao ni wahitaji wa huruma na neema kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ili aweze kuwasaidia kutumia vyema rasilimali za dunia; kwa kuonesha moyo wa ukarimu na mapendo; kwa kujikita katika fadhila ya unyenyekevu; kwa kujielekeza zaidi katika mchakato wa kukutana na wengine pamoja na kumwilisha upendo katika huduma kwa jirani, lakini hasa zaidi kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, muda wa kupokea wokovu ni mfupi sana kwani unategemea maisha ya mtu hapa duniani. Hiki ni kipindi muafaka cha kuonja huruma na upendo wa Mungu sanjari na kupembua ili kuangalia kipimo cha upendo kwa Mwenyezi Mungu. Kila nukta ya maisha ya mwanadamu ni muhimu sana, kwa ajili ya kumpenda Mungu na jirani, ili hatimaye, kuweza kuingia katika maisha na uzima wa milele! Maisha ya binadamu yanaweza kupimwa kwa kutumia vigezo viwili. Kigezo cha kwanza ni kile kinachozingatia saa, siku na miaka na kigezo cha pili kinajielekeza zaidi katika maendeleo ya mtu tangu pale anapozaliwa hadi mauti yanapomfika kadiri ya mapenzi ya Mungu. Kila muda una umuhimu wake, kwani inaweza kuwa ni nafasi ya kukutana na Mwenyezi Mungu.

Fadhila ya imani inawasaidia waamini kutambua maana ya nyakati hizi katika maisha ya kiroho. Kila wakati una pande mbili, yaani upande wa chanya na upande wa hasi. Mwinjili Marko katika sehemu hiii ya Injili anawaonesha akina: Simoni, Andrea, Yakobo na Yohane, watu wazima, waliokuwa na kazi yao ya kuvua samaki pamoja na maisha ya kifamilia. Lakini, Kristo Yesu alipowaambia “Njoni mnifuate, nami nitawafanya kuwa wavuvi wa watu. Mara wakaziacha nyavu zao, wakamfuata”. Mk. 1: 17-18. Bikira Maria awasaidie waamini kutumia kila nukta ya maisha yao kama wakati wa wokovu, ambamo Kristo Yesu anapita na kuwapatia mwaliko wa kumfuasa. Awasaidie waamini kutubu na kumwongokea Mungu na hivyo kuanza kujikita zaidi kwenye upendo unaomwilishwa katika huduma makini kwa Mungu na jirani!

Malaika wa Bwana
24 January 2021, 15:42