Tafuta

Vatican News
Dominika ya Neno la Mungu: Baba Mtakatifu Francisko amegusia kuhusu: Nguvu ya Neno la Mungu katika maisha ya Mitume wake, Ukaribu wa Mungu na kwamba, Neno la Mungu ni Waraka wa Upendo. Dominika ya Neno la Mungu: Baba Mtakatifu Francisko amegusia kuhusu: Nguvu ya Neno la Mungu katika maisha ya Mitume wake, Ukaribu wa Mungu na kwamba, Neno la Mungu ni Waraka wa Upendo.  (Vatican Media)

Dominika ya Neno la Mungu: Nguvu ya Neno na Ukaribu wa Mungu!

Papa Francisko: Kauli mbiu ya maisha na utume wa Kristo Yesu inayomwonesha Mwenyezi Mungu kuwa yu karibu na waja wake. Neno la Mungu li karibu sana nawe ili upate kupandikiza mbegu ya matumaini kwa njia ya ujirani mwema. Nguvu ya Neno la Mungu inajionesha miongoni mwa Mitume wa Yesu walioitwa kuwa ni wavuvi wa watu! Yaani: Neno la Mungu ni Waraka wa Upendo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko kwa njia ya Barua Binafsi, Motu Proprio: “Aperuit illis” yaani: “Aliwafunulia akili zao” ameanzisha Dominika ya Neno la Mungu inayoadhimishwa kila mwaka, Jumapili ya Tatu ya Mwaka wa Kanisa. Lengo kuu la Dominika hii ni: kwa ajili ya kuliadhimisha, kulitafakari na kulieneza Neno la Mungu. Maadhimisho haya ni matunda ya Mwaka wa Jubilei ya Huruma ya Mungu na pia yana mwelekeo wa kiekumene, kwani huu ni wakati ambapo Wakristo wanakutana pamoja ili kuombea umoja wa Wakristo. Maadhimisho ya Dominika ya Neno la Mungu kwa mwaka 2021 yanaongozwa na kauli mbiu “Mkishika neno la uzima”. Flp. 2:16. Mtume Paulo anaelezea wajibu wa Wakristo wa kuwa ni chemchemi ya furaha kwa watu wa Mataifa. Kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wake, Baba Mtakatifu Francisko, Dominika ya Neno la Mungu, tarehe 24 Januari 2021 hakuweza kushiriki wala kuongoza na badala yake Ibada hii ya Misa Takatifu iliyoadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican imeongozwa na mahubiri kusomwa kwa niaba yake na Askofu mkuu Salvatore Rino Fischella, Rais wa Baraza la Kipapa la Uhamasishaji wa Uinjilishaji Mpya.

Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake, anafafanua kauli mbiu ya maisha na utume wa Kristo Yesu inayomwonesha Mwenyezi Mungu kuwa yu karibu na waja wake. Neno la Mungu li karibu sana, liko katika kinywa chako na moyo wako upate kupandikiza mbegu ya matumaini kwa njia ya ujirani mwema. Nguvu ya Neno la Mungu inajionesha miongoni mwa Mitume wa Yesu walioitwa kuwa ni wavuvi wa watu! Kwa ufupi Neno la Mungu ni Waraka wa Upendo! Kristo Yesu alianza kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa kusema “Wakati umetimia, na ufalme wa Mungu umekaribia; tubuni, na kuiamini Injili” Mk. 1:15. Huu ni ujumbe unaonesha ukaribu wa Mungu kwa waja wake, kwa sababu Ufalme wake umeshuka kutoka mbinguni na yuko kati pamoja na waja wake. Kwa njia ya Fumbo la Umwilisho, Neno wa Mungu alipotwaa mwili na kuzaliwa na Bikira Maria, amefupisha ule umbali uliokuwepo kati ya Mungu na mwanadamu, kiasi kwamba, Kristo Yesu ameutwaa ubinadamu ili kutangaza na kushuhudia ukaribu wa Mungu ambao umekuwa ni kauli mbiu ya maisha na utume wake hapa duniani.

Huu ni muhtasari na kiini cha mahubiri yake, dira na mwelekeo wa maisha ya Wakristo. Kwa njia ya kutangaza na kushuhudia ukaribu wa Mungu, binadamu amekirimiwa neema na hivyo kuonja huruma ya Baba wa milele. Daima Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo ameendelea kuwahakikishia waja wake kwa kusema “Usiogope, niko pamoja nawe! Niko karibu na nitaendelea kuwa karibu nawe! Neno la Mungu li karibu sana, liko katika kinywa chako na moyo wako upate kupandikiza mbegu ya matumaini kwa njia ya uwepo na ujirani mwema. Huu ni mwaliko wa kuondokana na woga katika maisha na hivyo kutaka kujitenga. Mwenyezi kwa njia ya Neno lake anataka kuwa karibu na kuonesha ujirani mwema kwa wale wote wanaojisikia upweke, kwa kutambua kwamba, watu wote wamehifadhiwa katika “sakafu ya moyo wake”. Neno la Mungu ni chemchemi ya amani, faraja, toba na wongofu wa ndani. Kristo Yesu anawaalika waja wake kutubu na kumwongokea Mungu, tayari kujenga na kudumisha ujirani mwema, kama sehemu ya mchakato wa ushuhuda wa maisha ya Kikristo.

Hii ni changamoto kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuachana na tabia ya kuwatenga na kutowajali wengine. Kwa wale wote wanaolikumbatia Neno la Mungu wanapaswa kutambua kwamba, huu ni wakati wa kutoka na kuwaendea wengine kwa njia ya Neno wa Mungu aliyejifanya kuwa ni jirani mwema. Huu si wakati kwa mwamini kutaka kujitafuta na kujilinda mwenyewe, bali kusaidia mchakato wa kupandikiza mbegu ya matumaini kwa njia ya ujirani mwema, kama anavyofanya Mwenyezi Mungu kwa waja wake. Kristo Yesu alianza kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa wavuvi wa Galilaya. Hawa walikuwa ni watu wa kawaida kabisa, waliotegemea kupata mahitaji yao msingi kwa njia ya mikono yao wenyewe, kwa kufanya kazi usiku na mchana! Hawakuwa wataalam waliotalaumiwa katika Sayansi ya Maandiko Matakatifu, wala maarifa na tamaduni. Hawa waliishi mbali na miji iliyotambulikana kutokana na umaarufu wake wa kutoa elimu. Galilaya ulikuwa ni mji wa watu kutoka katika makabila na imani tofauti. Huu ni mji uliokuwa mbali sana na “dini safi” pamoja na mji wa Yerusalemu, kiini cha imani ya Waisraeli.

Kwa mshangao mkubwa anasema Baba Mtakatifu Francisko, Kristo Yesu alianza kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu pembezoni mwa jamii, ili kuonesha kwamba, watu wote wanakumbatiwa na Mwenyezi Mungu na wala hakuna aliyesahauliwa na kusukumwa pembezoni mwa jamii. Kila mtu anayo fursa ya kuweza kupokea Neno la Mungu na kukutana na Kristo Yesu. Mahubiri ya Kristo Yesu yanakuja baada ya yale yaliyotolewa na Yohane Mbatizaji na huo unakuwa ni mwanzo wa “kuandika ukurasa mpya”. Yohane Mbatizaji alikuwa anawakusanya watu jangwani, kwa wale waliokuwa na nafasi ya kuacha masuala yao mijini na kuanza kumwendea! Lakini, Kristo Yesu anatangaza na kushuhudia Neno la Mungu katikati ya jamii na kwa ajili ya watu wote mahali popote pale walipo! Hakuwa na muda maalum wala mahali ambapo alipapatia upendeleo wa pekee. Ndiyo maana alipokuwa akipita kando ya bahari ya Galilaya aliwaona wavuvi na kuwaita kuwa ni wafuasi wake, watakaosaidia kuwavua watu.

Hii ndiyo nguvu kuu ya Neno la Mungu inayowafikia wote na katika medani mbali mbali za maisha! Neno la Mungu lina nguvu ya ajabu katika maisha ya kila mwamini. Ndiyo maana Mitume hawakusahau kamwe maneno waliyoambiwa na Kristo Yesu walipokuwa wakitupa jarife, walipokuwa karibu na ndugu zao pamoja na wafanyakazi wenzao. Haya ni maneno ambayo yalikita mizizi yake katika akili na nyoyo zao hata kuendelea kuyakumbuka. Kristo Yesu alisema, “Njoni mnifuate, nami nitawafanya wavuvi wa watu” Mk. 1:17. Kristo Yesu alitumia Neno la Mungu kufafanua kuhusu maisha na utume wao kwamba, tangu sasa watakuwa ni wavuvi. Baadaye Mitume wanatambua kwamba, maneno na wito wa Kristo Yesu umekuwa ni chemchemi ya furaha ya kweli, ikilinganishwa na jinsi walivyokuwa wavuvi wa watu, kwani Kristo Yesu alionesha upendo wake kwao na kwa jinsi walivyokuwa na akaongoza hatua zao polepole katika maisha na utume wao. Kama ilivyokuwa kwa wale wavuvi wa Galilaya, hata leo hii, Kristo Yesu anataka kuwapatia waja wake, changamoto ya kubadili mwelekeo wa maisha, kwa kuanza kumfuasa, huku kila mtu akichukua vyema Msalaba wake.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Neno la Mungu ni sawa na Waraka wa Upendo ulioandikwa na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya waja wake, kwani anawatambua fika kuliko mtu mwingine awaye yote. Kwa kusoma na kulitafakari Neno la Mungu, waamini wanasikia tena sauti yake mwanana, wanaona ufunuo wa Uso wake wenye huruma na mapendo na hivyo kumpokea Roho wake Mtakatifu. Neno la Mungu linawawawezesha waamini kuwa karibu zaidi na Mwenyezi Mungu, kumbe, hii ni changamoto ya kuhakikisha kwamba, Neno la Mungu linakuwa karibu zaidi na waamini. Neno la Mungu libebwe mifukoni, kwenye simu za viganjani na litunzwe kwa heshima majumbani. Waamini wajenge utamaduni wa kulisoma, kulitafakari na kulimwilisha Neno la Mungu katika uhalisia na vipaumbele vya maisha yao. Waamini wafungue Neno la Mungu wanapoianza na kuhitimisha siku, ili baadhi ya mistari ya Neno la Mungu iweze kuzama zaidi katika akili na nyoyo za waamini.

Ili kuweza kufikia uamuzi huu anasema Baba Mtakatifu Francisko anapohitimisha mahubiri yaliyosomwa kwa niaba yake na Askofu mkuu Salvatore Rino Fischella, Rais wa Baraza la Kipapa la Uhamasishaji wa Uinjilishaji Mpya anakaza kusema kwamba, hapa kweli yataka moyo! Yaani kuzima luninga na kuanza kusoma Maandiko Matakatifu! Kuzima simu na kufungua sehemu ya Injili. Mwaka B wa Liturujia ya Kanisa, watu wa Mungu wanaongozwa na Injili kama ilivyo andikwa na Marko. Hii ni Injili ambayo ni rahisi na ni fupi! Baba Mtakatifu anawaalika waaamini kusoma sehemu ya Injili hii, kila siku, hatua kwa hatua, mwishoni, wataweza kugundua “siri ya urembo”.

Papa: Dominika ya Neno

 

24 January 2021, 15:59