Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko anawataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuwa na matumaini kwa mwaka 2021 sanjari na kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu Francisko anawataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuwa na matumaini kwa mwaka 2021 sanjari na kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu.  (AFP or licensors)

Papa Francisko: 2021 Mwaka wa Mshikamano Na Matumaini

Papa Francisko anawaalika waamini kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu kwa kuwa na matumaini na hivyo kuondokana na mawazo ya watu waliokata tamaa. Mambo yatakwenda sawia, ikiwa kama familia ya binadamu itaweza kufanya kazi kwa ushirikiano na umoja kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, maskini na wanyonge wakipewa kipaumbele cha kwanza.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Tafakari na Sala ya Malaika wa Bwana, kutoka kwenye Maktaba ya Kitume mjini Vatican, Jumapili tarehe 3 Januari 2021 amewatakia waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema matashi, neema na baraka za Mwaka mpya wa 2021. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu kwa kuwa na matumaini na hivyo kuondokana na mawazo ya watu waliokata tamaa. Mambo yatakwenda sawia, ikiwa kama familia ya binadamu itaweza kufanya kazi kwa ushirikiano na umoja wa kidugu, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, maskini na wanyonge wakipewa kipaumbele cha kwanza.

Hakuna mtu anayefahamu mipango ya Mwenyezi Mungu kwa mwaka 2021, lakini wote kwa pamoja wanapaswa kujishughulisha zaidi kwa ajili ya huduma kwa jirani sanjari na kujikita katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Kishawishi kikubwa kwa wakati huu ni watu kujihangaikia kwa ajili ya ustawi na mafao yao binafsi. Watu wanalenga zaidi faida kubwa ya kiuchumi, wanataka kuishi kwa raha mustarehe “huku wakila bata kwa mrija” yaani kwa maneno machache, kuna watu wanataka kutosheleza hamu ya mioyo binafsi. Katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu, inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 bado kuna watu wanathubutu kutoroka na kuvunja protokali ili kwenda kuvinjari.

Viwanja vya ndege vimefungwa, sehemu mbalimbali za dunia lakini kuna ndege zaidi 40 ziliruka kutoka katika nchi moja, ili kuwapeleka watu kuvinjari. Baba Mtakatifu anasema, mwelekeo wa namna hii, unamsikitisha sana kwa sababu ni kielelezo cha ubinafsi wa hali ya juu kabisa. Watu wamesahau, wale waliofariki dunia, wagonjwa wanaoendelea kuteseka hospitalini, watu ambao wamekosa fursa za ajira! Katika hali na mazingira haya, kuna watu ambao wametumbukizwa kwenye biashara na mifumo ya utumwa mamboleo. Baba Mtakatifu mwishoni, ametumia fursa hii kuwatakia heri na baraka, wanawake wajawazito wanaotarajia kujifungua hivi karibuni, kwa sababu, kuzaliwa kwa mtoto daima imekuwa ni chemchemi ya furaha na matumaini. Wote hawa watambue kwamba, Baba Mtakatifu Francisko yuko karibu nao kwa njia ya sala na sadaka yake. Waamini watambue kwamba, Kristo Yesu, Mwana wa Baba wa milele, amefanyika Neno na kuja kukaa pamoja nao katika hali njema na hata katika mapungufu yao ya kibinadamu.

Papa: 2021: Matumaini

 

 

 

 

 

03 January 2021, 14:39