Tafuta

Vatican News
Taarifa Rasmi: Askofu msaidizi Moses Chikwe na Dereva wake Bwana Ndubuisi Robert waliokuwa wametekwa nyara tarehe 27 Desemba 2020 wameachiwa huru tarehe 1 Januari 2021 huko Owerri, Nigeria. Taarifa Rasmi: Askofu msaidizi Moses Chikwe na Dereva wake Bwana Ndubuisi Robert waliokuwa wametekwa nyara tarehe 27 Desemba 2020 wameachiwa huru tarehe 1 Januari 2021 huko Owerri, Nigeria. 

Askofu Msaidizi Moses Chikwe na Dereva Wake Waachiwa Huru Owerri, Nigeria

Askofu msaidizi Moses Chikwe na Bwana Ndubuisi Robert waliokuwa wametekwa nyara wameachia huru, tarehe 1 Januari 2021, wakiwa salama. Askofu mkuu Obinna amemtembelea kwenye makazi yake, ingawa alikuwa anaonekana kuwa mnyonge zaidi kutokana na magumu aliyokumbana nayo wakati alipokuwa ametekwa nyara. Bwana Ndubuisi Robert alipelekwa hospitalini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku ya 54 ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2021 umeongozwa na kauli mbiu “Utamaduni wa Utunzaji Kama Njia ya Amani”. Katika ujumbe huu, Baba Mtakatifu anazungumzia kuhusu madhara ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, majanga asilia, ukosefu wa uhakika wa usalama wa chakula duniani, hali ngumu ya uchumi kitaifa na kimataifa pamoja na wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani. Katika kipindi hiki kumeibuka pia utaifa, chuki dhidi ya wageni, vita na kinzani mambo ambayo yanapelekea maafa na uharibifu, kumbe, utamaduni wa utunzaji ni kama njia ya amani.

Wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Sherehe ya Bikira Maria Mama wa Mungu, “Theotokos” sanjari na Siku ya Kuombea Amani Duniani, tarehe 1 Januari 2021, Baba Mtakatifu Francisko amewaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuungana naye katika sala na sadaka kwa ajili ya kumwombea Askofu msaidizi Moses Chikwe pamoja na dereva wake Bwana Ndubuisi Robert waliotekwa nyara na kikundi cha kigaidi hapo tarehe 27 Desemba 2020. Katika muktadha huu, Baba Mtakatifu aliwakumbuka na kuwaombea watu wote waliotekwa nyara na kupelekwa mahali kusikojulikana, huko nchini Nigeria, waweze kuachiwa huru na hatimaye, Nigeria iweze tena kurejea katika hali ya usalama, maridhiano na amani ya kweli.

Taarifa rasmi iliyotolewa na Askofu mkuu Anthony J.V. Obinna wa Jimbo kuu la Owerri nchini Nigeria na Radio Vatican kupata nakala yake inabainisha kwamba, Askofu msaidizi Moses Chikwe pamoja na dereva wake Bwana Ndubuisi Robert waliokuwa wametekwa nyara wameachia huru, tarehe 1 Januari 2021, wakiwa salama salimini. Askofu mkuu Obinna amemtembelea kwenye makazi yake, ingawa alikuwa anaonekana kuwa mnyonge zaidi kutokana na magumu aliyokumbana nayo wakati alipokuwa ametekwa nyara. Bwana Ndubuisi Robert alipelekwa hospitalini kwa ajili ya kupatiwa matibabu baada ya kupata jeraha kwenye mkono wake, alipokuwa anapambana na magaidi.

Jimbo kuu la Owerri linaipongeza Serikali, vyombo vya ulinzi na usalama kwa jitihada walizofanya hata kufanikisha kuokoa maisha ya Askofu msaidizi Moses Chikwe pamoja na dereva wake. Askofu mkuu Obinna anamshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kuguswa na kuonesha moyo wa ushirikiano, umoja na udugu wa kibinadamu aliposikia habari za kutekwa nyara kwa Askofu Moses Chikwe pamoja na dereva wake, muda mfupi tu, kabla ya kuachiliwa huru. Kwa namna ya pekee, Jimbo kuu la Owerri linamshukuru Askofu mkuu Antonio G. Filippazzi, Balozi wa Vatican nchini Nigeria, kwa kuonesha ukaribu wa Baba Mtakatifu katika kipindi hiki kigumu cha hofu na mashaka makubwa. Anawashukuru watu wote wa Mungu ndani na nje ya Nigeria, waliosali ili kumwomba Mwenyezi Mungu aweze kuwaokoa waja wake, kielelezo makini cha umoja na upendo wa udugu wa kibinadamu!

Owerri Nigeria
02 January 2021, 09:58