Tafuta

Maadhimisho ya Sikukuu ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu: Kugundua tena umuhimu wa malezi na makuzi ya watoto ndani ya familia! Maadhimisho ya Sikukuu ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu: Kugundua tena umuhimu wa malezi na makuzi ya watoto ndani ya familia! 

Sikukuu ya Familia Takatifu ya Nazareti: Malezi Bora ya Watoto!

Papa Francisko anawaalika waamini kugundua umuhimu wa elimu, malezi na makuzi ndani ya familia yanayokita mizizi yake katika upendo unaojenga mahusiano na mafungamano yanayofungua mwelekeo wa matumaini. Ndani ya familia, watu wanaweza kuonja mshikamano, ikiwa kama familia hii ni kielelezo cha sala, toba na msamaha; unyenyekevu, huruma na utulivu .

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Familia ni Kanisa dogo la nyumbani: “Domus ecclesiae”, shule ya upendo, huruma, haki na ukarimu. Ni mahali patakatifu ambapo tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni zinarithishwa, tayari kuunda jamii inayowajibikiana na kutegemezana kama ndugu wamoja. Mama Kanisa anawahimiza waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, kweli wanakuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya Ndoa na Familia, kwa kutangaza na kushuhudia: Ukuu, ukweli, uzuri, utakatifu na dhamana ya maisha ya ndoa na familia katika jamii. Familia iwe ni nyumba ya sala na tafakari ya Neno la Mungu; mahali pa kusoma, kutafakari na hatimaye kumwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha na wito wao. Familia ni kitovu cha miito mbalimbali ndani ya Kanisa. Familia iwe ni mahali pa kuadhimisha mafumbo ya Kanisa, tayari kuyatangaza na kuyashuhudia! Familia iwe ni Kanisa dogo la nyumbani; kwa kuwa tayari kumtangaza na kumshuhudia Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu kwa njia ya ukarimu kwa jirani; kwa kujenga na kudumisha umoja, upendo na mshikamano wa kidugu, ili imani iweze kukua na hatimaye, kukomaa.

Kanisa linatambua kwamba, ndoa inaundwa na mahusiano thabiti kati ya bwana na bibi na wala hakuna mkanganyiko na mifumo mingine ya maisha inayopendekezwa na baadhi ya serikali kwa kutaka kuhalalisha hata ndoa za watu wa jinsia moja, kielelezo cha kukengeuka na watu kutaka kumezwa na utamaduni wa kifo. Familia mamboleo inakabiliwa na changamoto dekedeke zinazopaswa kupatiwa ufumbuzi kwa njia ya wongofu wa kichungaji! Katika nyakati za shida na karaha katika maisha ya ndoa na familia ni muda muafaka wa kujenga ukaribu na mafungamano ya dhati na Kristo Yesu kwa njia ya: Sala, Tafakari ya Neno la Mungu, Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu pamoja na maadhimisho mbali mbali ya Sakramenti za huruma ya Mungu kwa waja wake.

Ni katika muktadha huu, kama sehemu ya maadhimisho ya kumbukumbu ya Miaka 5 tangu Baba Mtakatifu Francisko achapishe Wosia wake wa Kitume: “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya Upendo ndani ya familia”, hapo tarehe 19 Machi 2021 ametangaza kwamba, itakuwa ni siku ya kuzindua Mwaka wa Furaha ya Upendo Ndani ya Familia, “Famiglia Amoris Laetitia” utakaohitimishwa wakati wa maadhimisho ya Siku ya X ya Familia Duniani itakayoadhimishwa mjini Roma tarehe 26 Juni, 2022 kwa kuongozwa na kauli mbiu: “Upendo wa familia: wito na njia ya utakatifu”. Baba Mtakatifu anasema, lengo la kuchagua tema hii ni kutaka kukazia mchakato wa utakatifu wa maisha unaofumbatwa katika uhalisia wa kila siku wa mahusiano ndani ya familia.Huu ni mwendelezo wa maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu kwa ajili ya familia. Tamko hili limetolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kutoka kwenye Maktaba ya Kitume, mjini Vatican wakati wa maadhimisho ya Sikukuu ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu, Jumapili tarehe 27 Desemba 2020.

Maadhimisho ya Mwaka wa Furaha ya Upendo ndani ya Familia kuanzia sasa yanaratibiwa na Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha. Baba Mtakatifu anapenda kuyaweka maandalizi ya Maadhimisho ya Mwaka wa Furaha ya Upendo ndani ya Familia chini ya ulinzi na tunza ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu; kwani maadhimisho haya yanazishirikisha familia zote duniani. Bikira Maria, azisaidie familia zote ziweze kuvutwa na ushuhuda wa tunu msingi za Kiinjili kutoka kwenye Familia Takatifu na kwa njia hii, ziweze kuwa ni chachu ya kupyaisha ubinadamu na ujenzi wa mshikamano wa kidugu unaokita mizizi yake katika uhalisia wa maisha na kwa ajili ya wengi.

Baba Mtakatifu Francisko mwanzoni mwa tafakari yake wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana amekumbusha kwamba, Mama Kanisa anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema katika Liturujia ya Neno la Mungu, Sikukuu ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu, kumtafakari Kristo Yesu, Mwana wa Mungu, aliyekuwa na mahitaji msingi kama watoto wengine wote! Alihitaji upendo unaobubujika kutoka ndani ya familia. Familia Takatifu ni mfano na kielelezo cha familia zote ulimwenguni kwani ndani yake zinaweza kupata uhakika na rejea makini na msukumo wa usalama wa uhakika. Mji wa Nazareti umekuwa ni chimbuko la mapambazuko ya maisha ya kibinadamu ya Mwana wa Mungu, aliyetungwa mimba tumboni mwa Bikira Maria kwa uwezo wa Roho Mtakatifu.

Katika kuta za Nyumba ya Nazareti, Mtoto Yesu aliweza kuonja furaha ya maisha ya utotoni, akiwa amezungukwa na upendo thabiti wa Bikira Maria na ulinzi na tunza ya Mtakatifu Yosefu, mambo yaliyomwezesha kuona huruma na upendo wa Mungu. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kugundua umuhimu wa elimu, malezi na makuzi ndani ya familia yanayokita mizizi yake katika upendo unaojenga mahusiano na mafungamano yanayofungua mwelekeo wa matumaini. Ndani ya familia, watu wanaweza kuonja umoja na mshikamano, ikiwa kama familia hii ni kielelezo cha sala, toba na msamaha; unyenyekevu, huruma na utulivu kama sehemu ya kutafuta, kuambata na kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha.

Ni katika hali na mazingira kama haya, familia zinafungua malango ya furaha ya Mungu anayewakirimia wote wanaotambua jinsi ya kuwashirikisha wengine furaha ya kweli! Kwa njia hii, familia pia inapata nguvu za maisha ya kiroho na hivyo kuweza kujifungua kwa ajili ya wengine, ili kutoa huduma kwa jirani pamoja na kushiriki katika mchakato wa ujenzi wa ulimwengu mpya ulio bora zaidi, lakini kwa kuhakikisha kwamba, familia zinakita maisha na utume wake katika mwelekeo chanya na katika mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Familia iwe ni kitovu cha msamaha wa kweli kwa kutambua kwamba, kukosa na kukoseana ni sehemu ya udhaifu wa kibinadamu, kutubu, kusamehe na kupatana ni mwanzo wa utakatifu wa maisha. Wanafamilia wajifunze kusema: Naomba, Asante na Samahani; maneno yanayoweza kuisaidia familia kuishi kwa amani na utulivu.

Papa: Familia: Malezi

 

 

27 December 2020, 15:48