Tafuta

Tarehe 2 Desemba ni Siku ya kukomesha utumwa duniani Tarehe 2 Desemba ni Siku ya kukomesha utumwa duniani  

Siku ya Kukomesha Biashara ya Utumwa Duniani:Utumwa huondoa hadha yetu!

Kila tarehe 2 Desemba ni Siku ya Kukomesha Biashara ya Utumwa Duniani, ambapo mwaka 1949 Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha Mkataba wa Kukomesha Biashaŕa ya Watu na Ukahaba na kila aina nyingine ya udhalilishaji kama huo.Papa katika Ujumbe wake kwa njia ya mitandao katika fursa ya siku hii amesema,utumwa ni kutostahili kwetu,kwa sababu huondoa heshima na hadhi yetu sote.

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican.

Siku ya Kukomesha Biashara ya Utumwa Duniani, ifanyikayo kila tarehe 2 Desemba ya kila mwaka ilianzishwa mwaka 1949 na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ambapo ilipitisha Mkataba wa Kukomesha Biashara ya Watu na Ukahaba, unyonyaji na kila aina nyingine ya udhalilishaji kama huo na utumwa mamboleo. Katika fursa ya siku hii, Papa Francisko katika mtandao wa kijamii amesema “Leo kama jana, katika mzizi wa utumwa kuna dhana ya mwanadamu ambayo inakubali uwezekano wa kumchukulia kama kitu, cha kukanyaga hadhi yake. Utumwa ni kutostahili kwetu, kwa sababu huondoa heshima na hadhi yetu sote.

Mkataba kwa lengo la kutokomeza kila aina ya utumwa

Mkataba ni moja ya vyombo vya kimataifa vyenye lengo la kutokomeza utumwa, ambao sasa upo kwa jina la masharti ya madeni, vibarua vya kulazimishwa miongoni mwa watu wazima na watoto, unyonyaji wa ngono dhidi ya watoto, biashara ya watoto na kulazimishwa ndoa za utotoni na mengine. Mbele ya aina mpya za utumwa hakuna uwezekano wa kutokujali, lazima kuingilia kati katika muktadha huo. Katika ulimwenguni inahasabiwa wapo zaidi  watumwa milioni 40, ya kile kiitwacho utumwa mamboleo, na robo yao karibu ni watoto! Kuna sura nyingi za majanga haya ambayo yanalaaniwa karibu nchi zote. Ili kuongeza uelewa wa umma juu ya ukweli huu, Umoja wa Mtaifa (UN) kwa hakika uliweza kutangaza Siku ya Kimataifa ya Kukomesha Utumwa ili kutafuta namna ya kuwa utambuzi wa hali halisi ambayo inazungukia karibu kila kona ya dunia, utumwa huu na utumwa mamboleo.  Maombi ya Papa Francisko kila wakati ni kutokufunga macho mbele ya vidonda vya ndugu kaka na dada wengi wanaoteseka na janga hili la kuondolewa hadhi na utu wa mwanadamu.

Utumwa wa kisasa unaendelea kuwa janga 

Papa Francisko wakati wa afla ya kusaini Mkataba dhidi ya utumwe kwa upande wa watawa, waliokuwa kwenye mkutano wao huko Casina Pio IV, jiji Vatican, tarehe 2 Desemb 2014 alisema: “ Licha ya juhudi kubwa za wengi, utumwa wa kisasa unaendelea kuwa janga baya ambalo lipo, kwa kiwango kikubwa, ulimwenguni kote (...), kuwafanya wahanga wake kuingia katika ukahaba, usafirishaji wa watu, kazi ya kulazimishwa, kazi za utumwa, ukeketaji, uuzaji wa viungo, matumizi ya dawa za kulevya, ajira ya watoto.  Na jambo baya zaidi ni kwamba hali hii, kwa bahati mbaya inazidi kuwa mbaya kila siku”, alisisitiza Papa. 

Tunawezaje kusahau waathiriwa wengi waliojificha

Kwa maana hiyo ni wazi kwamba  Umoja wa Mataifa tangu mwaka 1949 ambapo waliamua  katika Mkutano wao mkuu kuthibiti usafirishaji haramu wa watu na unyonyaji wa ukahaba na ambao umekuwa siyo mazungumzo tu lakini kuna iana mbali mbali mpya za utumwa, ambapo jitihada zaidi zinahitajika,  hasa ni jukumu la kipaumbele kwa Wakristo.  “Hata leo lazima tuorodheshe aina nyingi za utumwa mpya ambao mamilioni ya wanaume, wanawake, vijana na watoto wanakabiliwa. (...) Tunawezaje kusahau mamilioni ya wahamiaji ambao ni wathiriwa kwa masilahi mengi yaliyofichwa, mara nyingi hutumika kwa matumizi ya kisiasa, ambao wananyimwa mshikamano na usawa? ”, Aliandika Papa Francisko katika ujumbe wa Siku ya Maskini Ulimwenguni mnamo  tarehe 17 Novemba 2019. Fikiria tu kile kinachotokea kwa wanaume na wanawake waliotekwa nyara na kusafirishwa nchini Libia na mara nyingi kulazimishwa kwenda baharini”.

Sala kwa maombezi ya Mtakatifu Bakhita

Hata hivyo pia mnamo tarehe 10 Februari mwaka jana, wakati wa sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili ambayo mama Kanisa  alikuwa anamkumbuka Mtakatifu Josephina Bakhita ambaye aliishi utumwani, akimaanisha hasa wahanga wa usafirishaji haramu, Papa Francisko alisema:“Tunaweza na lazima tushirikiane na kukemea kesi za unyonyaji na utumwa wa wanaume, wanawake na watoto”. Na alimwomba  Mtakatifu atuombee sisi sote ili tusiingie katika kutokujali, na ili tufungue macho yetu na tuweze kuangalia maumivu  na majeraha ya kaka na dada wengi wanaonyimwa utu wao uhuru wao na kusikiliza kilio chao wanaoomba msaada”.

02 December 2020, 17:29