Tafuta

Vatican News
Papa Francisko katika Waraka wake wa Kitume: "Admirabile signum" anafafanua maana na umuhimu wa Pango la Noeli. Papa Francisko katika Waraka wake wa Kitume: "Admirabile signum" anafafanua maana na umuhimu wa Pango la Noeli.  (Vatican Media)

Papa: Ishara ya Kushangaza: Maana na Umuhimu wa Pango la Noeli

Pango la Noeli limesheheni utajiri na amana ya Mafumbo ya maisha ya Yesu, ambayo yako karibu sana na maisha ya watu. Pango la kwanza la Noeli lilitengenezwa na Mtakatifu Francisko wa Assisi kunako tarehe 29 Novemba 1223 baada ya Papa Honorius III kupitisha Katiba ya Shirika lake. Pango hili la Noeli ni matokeo ya hija ya kiroho iliyofanywa na Mtakatifu Francisko wa Assisi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, wakati wa katekesi yake kuhusu Sherehe za Noeli, Jumatano tarehe 23 Desemba 2020, amewaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kujiandaa kikamilifu katika maadhimisho ya Sherehe za Noeli kufanya tena rejea katika waraka wake wa kitume “Admirabile signum” yaani “Ishara ya Kushangaza”: Maana na Umuhimu wa Pango la Noeli”. Itakumbukwa kwamba, ilikuwa ni Jumapili ya kwanza ya Majilio, tarehe 1 Desemba 2019 akiwa kwenye Madhabahu ya Wafranciskani huko Greccio, Rieti, Mkoani Lazio, nchini Italia, Pango la kwanza kabisa la Noeli lililotengenezwa na Mtakatifu Francisko wa Assisi, Papa alitia mkwaju kwenye Waraka wa Kitume “Admirabile signum” yaani “Ishara ya Kushangaza”: Maana na Umuhimu wa Pango la Noeli”. Baba Mtakatifu anasema, Pango la Noeli ni mahali ambapo panaonesha alipozaliwa Kristo Yesu, Mwana wa Mungu, alama hai ya Injili, mwaliko wa kutafakari Fumbo la Umwilisho, Neno wa Mungu alipofanyika mwanadamu, ili kukutana na watu wote, ili kuwaonjesha upendo wake na hatimaye, waweze kuunganika pamoja naye.

Kwa Waraka huu wa Kitume, Baba Mtakatifu anapenda kuwahamasisha waamini kuendeleza Mapokeo ya kuandaa Pango la Noeli kwenye familia, mahali pa kazi, shuleni, hospitalini, magerezani na kwenye maeneo ya wazi, kama kielelezo cha ibada katika Fumbo la Umwilisho. Mahali ambapo Ibada hii ilikuwa imeanza kufifia, Baba Mtakatifu anatoa mwaliko wa kuipyaisha tena. Injili zinatoa ufafanuzi wa Pango la Noeli kwa kusema kwamba, Bikira Maria, alizaa Mwanaye, akamlaza katika hori ya kulia ng’ombe,  kwa sababu hawakupata nafasi katika nyumba ya wageni. Yesu alilazwa kwenye “Praesepium” yaani “Pango la Noeli”. Hiki kikawa ni kitanda chake cha kwanza, Kristo Yesu ambaye alijifunua kama “Mkate ulioshuka kutoka mbinguni”, akalazwa Pangoni ili awe ni “chakula cha wasafiri”. Pango la Noeli limesheheni utajiri na amana ya Mafumbo ya maisha ya Kristo Yesu, ambayo yako karibu sana na maisha ya watu wa kawaida. Pango la kwanza la Noeli lilitengenezwa na Mtakatifu Francisko wa Assisi kunako tarehe 29 Novemba 1223 baada ya Papa Honorius III kupitisha Katiba ya Shirika lake.

Pango hili la Noeli ni matokeo ya hija ya kiroho iliyofanywa na Mtakatifu Francisko wa Assisi mjini Bethlehemu pamoja na picha alizowahi kuona kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu lililoko mjini Roma. Alilitengeneza Pango la Noeli, Siku 15 kabla ya Sherehe ya Noeli kama kumbu kumbu endelevu ya Fumbo la Umwilisho. Ilikuwa ni tarehe 25 Desemba 1223 watawa Wafranciskani kutoka sehemu mbali mbali za dunia walifika kwenye Madhabahu ya Wafranciskani huko Greccio. Pango likapambwa kwa uwepo wa mahujaji na wanyama mbali mbali na Ibada ya Misa Takatifu ikaadhimishwa Pangoni humo, ili kuonesha uhusiano wa dhati kati ya Fumbo la Umwilisho na Fumbo la Ekaristi Takatifu. Kwa mara ya kwanza, Pango halikuwa na sanamu mbali mbali kama zinavyonekana wakati huu. Pole pole, Pango la Noeli likapambwa na Sanamu ya Mtoto Yesu aliyelazwa kwenye hori la kulishia wanyama. Na wote walioshuhudia tukio hili wakarejea makwao wakiwa wamesheheni furaha kubwa nyoyoni mwao. Haya ni matunda ya uinjilishaji uliofanywa na Mtakatifu Francisko wa Assisi, kiasi kwamba, mafundisho yake, hadi leo hii yanaendelea kugusa sakafu ya maisha ya waamini kwa njia ya imani.

Madhabahu ya Greccio yamekuwa ni kimbilio la watu wanaotaka kusali na kutafakari katika hali ya utulivu na kimya kikuu. Pango la Noeli anasema Baba Mtakatifu ni kielelezo cha upendo wa Mungu; zawadi ya maisha inayokumbatia udugu na urafiki unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu ambaye pia ana uwezo wa kuwasamehe watu dhambi zao na kuwaweka huru! Injili na Pango la Noeli ni msaada mkubwa katika kulitafakari Fumbo la Umwilisho, kwa kugusa nyoyo za watu na hivyo kuwazamisha katika historia ya wokovu katika muktadha wa mazingira na tamaduni za watu. Huu ni mwaliko wa “kugusa na kuhisi umaskini wa Mwana wa Mungu unaojionesha kwa namna ya pekee katika Fumbo la Umwilisho, ili kuchuchumilia na kuambata njia ya unyenyekevu, ufukara na sadaka ili kufuata ile njia kutoka mjini Bethelehemu hadi mlimani Kalvari. Waamini wanaalikwa kukutana na kumhudumia Kristo Yesu anayejitambulisha na ndugu zake maskini na wahitaji zaidi.

Baba Mtakatifu katika tafakari yake, anagusia mazingira ya giza na kimya kikuu kinachotanda usiku wa manane, kielelezo cha watu wanaotembea katika giza na uvuli wa mauti, kiasi cha kudhani kwamba, Mwenyezi Mungu amewasahau waja wake na kwamba, maisha hayana tena thamani. Mwenyezi Mungu ndiye asili na hatima ya binadamu. Lakini mwanga utokao juu umewafikia na kuwaangaza wakaao katika giza na uvuli wa mauti. Mazingira ya Pango la Noeli yanaonesha magofu ya nyumba za kale kama ilivyokuwa kwa mji wa Bethlehemu uliogeuka kuwa ni makazi ya Familia Takatifu. Magofu haya ni utambulisho wa kuanguka kwa binadamu, kumezwa na malimengu na hatimaye, kujikuta akiwa amekata tamaa. Uwepo wa Kristo Yesu katika mazingira na hali kama hii unapania kupyaisha, kuganga na kutibu hali ya maisha ya binadamu ili yaweze kurejea tena katika mng’ao wake asilia. Ni mazingira yanayowaonesha wafugaji na mifugo yao, wanaofurahia kuzaliwa kwa Masiha, Mkombozi wa ulimwengu.

Malaika wa Bwana na nyota angavu ni mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kwenda kumwabudu Mwana wa Mungu. Wachungaji wakawa ni watu wa kwanza kuona zawadi ya ukombozi. Maskini na wanyenyekevu wa moyo wakashuhudia Fumbo la Umwilisho. Kwa njia ya Kristo Yesu, Mwenyezi Mungu akapata tena nafasi ya kukutana na watoto wake katika mazingira ya Pango la Noeli. Mazingira ya Pango la Noeli kwa kawaida yanapaswa kuonesha uwepo wa maskini wanaothamini zaidi ufukara wa maisha ya kiroho. Hawa pia wanayo haki ya kuwa karibu na Mtoto Yesu na wala asiwepo mtu anayetaka kuwafukuzia mbali! Katika muktadha huu, nyumba inakuwa ni mahali pa ukarimu kwa maskini, kwa sababu hawa ndio watu wa kwanza kabisa kutambua uwepo wa Mungu kati ya waja wake na hawa kimsingi ndio walengwa wa Habari Njema ya Wokovu. Pango la Noeli ni ukumbusho kwamba, utajiri na raha za dunia ni mambo mpito.

Uwepo wa Mungu kwenye Pango la Noeli ni chachu ya mabadiliko makubwa yanayoleta matumaini pamoja na kukuza utu, heshima na haki msingi za binadamu. Kumbe, kuna haja ya kushirikishana na maskini utajiri na karama mbali mbali ambazo Mwenyezi Mungu amewakirimia waja wake, ili kujikita zaidi katika ujenzi wa utu na udugu wa kibinadamu ambamo, hakuna mtu anayetengwa wala kusukumizwa pembezoni mwa jamii. Waamini hupenda kupamba Pango la Noeli kwa sanamu za watu mbali mbali hata pengine hawana uhusiano wa karibu sana na simulizi za Injili. Yote haya ni mambo yanayoshuhudia: utakatifu na furaha ya maisha ya kila siku, kielelezo cha ushiriki wa Umungu wa Kristo katika hali na maisha ya binadamu. Baba Mtakatifu anasema, Bikira Maria Mama wa Mungu anayeoneshwa huku akiyatafakari matendo makuu ya Mungu, ni mtumishi wa Bwana aliyekubali kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yake. Akawa kweli ni Mama na Bikira na mwaliko kwa waamini kutii na kutekeleza yale yote wanayoambiwa na Kristo Yesu.

Mtakatifu Yosefu, Baba mlishi na mlinzi mwaminifu wa Familia Takatifu ni mwalimu wa kwanza wa Mtoto Yesu. Katika unyenyekevu wake, Yosefu mchumba wake Bikira Maria aliyahifadhi mafumbo yote ya maisha yaliyomzunguka Mtoto Yesu na Mama yake Bikira Maria. Yosefu mtu wa haki, akajiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu na kuyatekeleza yale yote aliyoambiwa! Pango la Noeli linakamilika kwa uwepo wa Mtoto Yesu anayepyaisha mazingira yote. Mwenyezi Mungu anaonekana kama Mtoto mchanga anayetaka kuwabeba waja wake mikononi mwake. Anafunua nguvu na uweza wake unaoumba na kuleta mageuzi makubwa. Hii ni nguvu inayofunua ukuu wa upendo wake usiokuwa na mipaka, kwa kutabasamu na kuwakunjilia watu mikono yake. Mtoto Yesu anaonesha Fumbo la maisha ya binadamu kiasi kwamba, hata Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu walihisi uwepo wa Mungu kati yao. Fumbo la Umwilisho ni ufunuo wa Injili ya uhai, changamoto na mwaliko wa kutafuta na kuambatana utukufu wake na kwamba, maisha ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Ili kutambua hatima ya maisha ya binadamu, kuna haja ya kuwa ni wafuasi wake amini.

Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka huu wa Kitume “Admirabile signum” yaani “Ishara ya Kushangaza”: Maana na Umuhimu wa Pango la Noeli” anasema, inapokaribia Sherehe ya Tokeo la Bwana, au Epifania, sanamu za Mamajusi watatu kutoka Mashariki zinawekwa kwenye Pango la Noeli. Hawa ni wataalam wa nyota kutoka Mashariki waliojitaabisha kumtafuta Mtoto Yesu na hatimaye walipomwona wakamzawadia: Ubani unaonesha Umungu wa Kristo; Manemane ni ushuhuda wa ubinadamu wa Kristo utakaokabiliwa na mateso, kifo na ufufuko kwa wafu. Dhahabu ni kielelezo cha Ufalme wa Kristo Yesu, yaani; Ufalme wa kweli na uzima; Utakatifu na neema; haki, upendo na amani. Kila mwamini anahimizwa kuwa kweli ni shuhuda na chombo cha matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama chemchemi ya furaha na amani inayobubujika kutoka kwa Mtoto Yesu. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Mamajusi kutoka Mashariki ya mbali ni kielelezo cha watu kutoka katika medani mbali mbali za maisha, wenye kiu ya kutaka kukutana na Mfame wa amani, anayetuliza kiu yao ya ndani.

Wanapomwona Mfalme katika hali ya Mtoto mchanga, kamwe hawashangazwi wala kuona kama hii ni kashfa ya mwaka, bali wanampigia magoti na kumwabudu kwa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu ambaye ni chemchemi ya hekima yote ndiye aliyewaongoza kwa kutumia nyota angavu hadi kumfikia. Huyu ndiye yule Mungu anayewaangusha wakuu katika viti vyao vya enzi na kuwakweza wanyonge. Bila shaka, Mamajusi waliporejea makwao waliweza kuwashirikisha wengine matendo makuu ambayo Mwenyezi Mungu aliwatendea katika maisha yao. Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha Waraka huu wa Kitume “Admirabile signum” yaani “Ishara ya Kushangaza”: Maana na Umuhimu wa Pango la Noeli” kwa kusema, Pango la Noeli ni muhimu sana katika mchakato wa kurithisha imani mintarafu historia na mazingira ya watu husika.

Ni changamoto na mwaliko wa kuendelea kushirikishana mang’amuzi na uzoefu huu kwa kusimulia kuhusu ufunuo wa upendo wa Mungu katika maisha ya mwanadamu. Mwenyezi Mungu anawapenda na yuko kati ya watu wake kwa njia ya Mwanaye mpendwa Kristo Yesu, chemchemi na furaha ya kweli katika maisha. Waamini wawe tayari kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Francisko wa Assisi kufungua nyoyo zao ili kupokea neema, ili wawe pia tayari kumtolea Mungu sifa na shukrani ambaye amewapenda upeo na anaendelea kubaki pamoja nao!

Waraka Pango la Noeli

 

 

 

23 December 2020, 16:18