Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko tarehe 18 Desemba 2020 amekutana na kuzungumza na kikundi cha wanataalimungu wa kiekumene wanaozungumza Kijerumani kutoka mjini Yerusalemu. Baba Mtakatifu Francisko tarehe 18 Desemba 2020 amekutana na kuzungumza na kikundi cha wanataalimungu wa kiekumene wanaozungumza Kijerumani kutoka mjini Yerusalemu.  (Vatican Media)

Papa Francisko Awataka Waamini Kuwa Mashuhuda wa Uwepo wa Mungu Duniani

Ni wajibu wao kwa siku za usoni kuingia katika majadiliano ya kina na ulimwengu unaoonesha kana kwamba, hakuna tena nafasi ya dini. Hii ni dhamana na wajibu ambao waamini wa dini mbalimbali duniani wanashirikishana kwa kutambua kwamba, uwepo wa Mungu kati ya waja wake ni jambo muhimu sana katika jamii. Jitihada hizi zifanyike kwa njia ya ushuhuda wa maisha!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kwa mara ya kwanza katika historia ya Chuo Kikuu cha Sayansi ya Maandiko Matakatifu kilichoko mjini Yerusalemu, kwa mwaka 2020, hakikuweza kuendesha kozi zake kutokana na maambukizi makubwa ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Katika muktadha huu, Taasisi ya Kipapa ya Liturujia katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Anselmi iliyoko mjini Roma, imekuwa ni mwenyeji wa kozi hii. Ijumaa tarehe 18 Desemba 2020, Baba Mtakatifu Francisko amebahatika kukutana na kuzungumza wafanyakazi na wanafunzi wa taalimungu kutoka katika Abasia ya Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni iliyoko mjini Yerusalemu, wanaozungumza lugha ya Kijerumani: “Theologisches Studienjahr” . Huu ni mradi wa kiekumene unaopania kuwapatia wanafunzi wa taalimungu ujuzi na maarifa ya Sayansi ya Maandiko Matakatifu. Mafunzo haya yanawawezesha kutembelea maeneo maarufu katika Maandiko Matakatifu na kuona Makanisa ya Mashariki sanjari na kukoleza moyo wa majadiliano ya kidini kwa kuona na kushuhudia ulimwengu wa dini ya Kiyahudi na Kiislam.

Lakini kwa bahati mbaya, kutokana na janga la Virusi vya Corona, COVID-19, wanafunzi hawa wamejikuta wakiwa uhamishoni kama anavyofafanua Padre Schnabel. Mafunzo ya kina kuhusu Sayansi ya Maandiko Matakatifu, Majadiliano ya Kiekumene na Kidini ni kati ya mambo yanayopewa kipaumbele cha kwanza katika malezi na majiundo yao ya kitaalimungu. Uwepo wao mjini Roma anasema Baba Mtakatifu Francisko utawawezesha kupata pia mwelekeo mpya ili hatimaye, kuweza kufikia lengo linalokusudiwa. Kama vijana wa kizazi kipya wanaojishughulisha kusoma taalimungu, kwa ajili ya vijana wenzao pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, wanatamani kuona ushuhuda wa umuhimu wa uwepo wa Mungu katika maisha na utimilifu unaotoa mwangwi wa imani inayomwilishwa katika maisha. Ni wajibu wao kwa siku za usoni kuingia katika majadiliano ya kina na ulimwengu unaoonesha kana kwamba, hakuna tena nafasi ya dini. Hii ni dhamana na wajibu ambao waamini wa dini mbalimbali duniani wanashirikishana kwa kutambua kwamba, uwepo wa Mungu kati ya waja wake ni jambo muhimu sana katika jamii.

Baba Mtakatifu anatambua mchango mkubwa unaotolewa na dini mbalimbali duniani katika ujenzi wa udugu wa kibinadamu; kwa kulinda na kudumisha haki ndani ya jamii. Lakini kuna wakati ambapo watu wanataka kumng’oa Mungu kutoka katika jamii na matokeo yake ni kuanza kuabudu miungu wadogo hali ambayo inamfanya mwanadamu kujipoteza mwenyewe. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, masomo haya ya taalimungu itakuwa ni hatua muhimu sana katika malezi na majiundo yao: kiroho na kiutu na kwamba, baada ya kuwa huku “uhamishoni, wataweza kupata nafasi ya kuona na kushuhudia “Nchi ya Ahadi”, maeneo matakatifu katika Biblia. Katika maandalizi ya maadhimisho ya Sherehe ya Noeli kwa Mwaka 2020, Baba Mtakatifu anapenda kuwahakikishia kwamba, watakuwa wanajiunga na mahujaji wengine kiroho kwenda kumtembelea Mtoto Yesu kule mjini Bethlehemu. Imanueli awakirimie na kuwajaza furaha na amani, ili hatimaye, awawezeshe kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa Imanueli yaani Mungu pamoja na nasi. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewapatia baraka zake za kitume na kuwaomba kumkumbuka na kumwombea katika sala zao.

Taalimungu

 

 

 

18 December 2020, 14:54