Tafuta

Vatican News
Papa Francisko: Sherehe za Noeli ni wakati muafaka wa kujenga na kudumisha upendo, amani na mshikamano wa udugu wa kibinadamu hasa na maskini na wahitaji zaidi. Papa Francisko: Sherehe za Noeli ni wakati muafaka wa kujenga na kudumisha upendo, amani na mshikamano wa udugu wa kibinadamu hasa na maskini na wahitaji zaidi. 

Papa Francisko: Sherehe za Noeli: Upendo, Mshikamano na Amani

Mungu mwingi wa huruma na mapendo, awajalie watu wote neema ya kuishi ujumbe wa Noeli, ambao kimsingi ni chemchemi ya amani, furaha na maisha mapya. Sherehe za Noeli zinapata umuhimu wa pekee, ikiwa kama zinaadhimishwa katika upendo na mshikamano. Kwa kuwakumbuka na kuwasaidia wagonjwa, maskini, wahitaji na wale wote wanaoelemewa na upweke hasi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Katika kipindi hiki cha maadhimisho ya Sherehe za Noeli, Mama Kanisa anawatakia watoto wake wote, amani na utulivu wa ndani, furaha na matumaini. Ni wakati wa kunafsisha utukufu wa Mungu na amani kwa watu anaowaridhia. Hizi ni tunu ambazo zinapaswa kutangazwa na kushuhudiwa na waamini kutoka katika sakafu ya nyoyo zao, zipambe na kunafsishwa katika jamii na familia ya binadamu katika ujumla wake. Hii ni sehemu ya salam na matashi mema yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa katekesi yake, Jumatano tarehe 23 Desemba 2020 kama sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Sherehe za Noeli kwa Mwaka 2020 Baba Mtakatifu anasema, kama ilivyokuwa kwa wachungaji waliokuwa wakikaa makondeni, walipoambiwa Habari Njema ya furaha kuu itakayokuwa kwa watu wote, ya kuzaliwa kwa ajili yao Mwokozi, ndiye Kristo Bwana, waliondoka mara na kwenda kushuhudia hayo waliyoambiwa na Malaika. Huu ni mwaliko hata kwa waamini kwenda kumwona Mtoto Yesu aliyelazwa katika hori ya kulia ng’ombe, ili aweze kuwakirimia mwanga angavu na amani yake katika maisha. Mtoto Yesu anapenda “kuwatajirisha waja wake kwa upendo, neema na baraka zinazobubujika kutoka kwake” wakati huu wa maadhimisho ya Fumbo la Umwilisho.

Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, awajalie watu wote neema ya kuishi ujumbe wa Noeli, ambao kimsingi ni chemchemi ya amani ya kweli, furaha na maisha mapya. Sherehe za Noeli zinapata umuhimu wa pekee, ikiwa kama zinaadhimishwa katika upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Kwa kuwakumbuka, kuwafariji na kuwasaidia wagonjwa, maskini, wahitaji na wale wote wanaoelemewa na upweke. Hawa ni watu wanaopenda kuonja uwepo wa jirani zao katika maisha, hata kama ni kwa njia ya simu au ujumbe wa imani, matumaini na mapendo, kwa hakika, Mwenyezi Mungu ajuaye yale yaliyoko sirini, atawakirimia pia kwa wakati wake. Mtoto Yesu katika kipindi hiki cha Noeli anasema Baba Mtakatifu Francisko awajalie waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kupata furaha na kuendelea kuwa ni vyombo na mashuhuda wa matumaini. Hii inatokana na ukweli kwamba, watu wengi sehemu mbalimbali za dunia, wanaadhimisha Sherehe za Noeli huku wakiwa wamejifungia majumbani mwao.

Kutokana na ongezeko kubwa la maambukizi ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, watu wengi zaidi hawataweza kusafiri na kuungana na familia pamoja na wapendwa wao. Lakini, Mtoto Yesu aliyelala Pangoni, anawachangamotisha waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema njia ya huruma na mapendo kwa kuwataka kujenga ujirani mwema kama sehemu ubinadamu wao. Kwa namna ya pekee kabisa, Baba Mtakatifu amewakumbuka wazee, vijana, wagonjwa na wanandoa wapya waliofunga pingu za maisha hivi karibuni. Upendo na uwajibikaji wa Bikira Maria na ukarimu uliyo tayari kutoka kwa Mtakatifu Yosefu viwe ni mfano bora kwa wote hawa katika kumkaribisha Mtoto Yesu, katika maadhimisho ya Fumbo la Umwilisho. Mwishoni mwa salam zake, Baba Mtakatifu Francisko amewatakia waamini na watu wote wenye mapenzi mema, maadhimisho ya Sherehe za Noeli na Mwaka Mpya wa 2021 amani na utulivu wa ndani!

Papa: Noeli Mshikamano

 

23 December 2020, 15:18