Tafuta

Vatican News
Ratiba elekezi ya maadhimisho ya Sherehe za Noeli kwa Mwaka 2020 hadi mwaka 2021. Hizi ni Ibada zitakazoongozwa na Baba Mtakatifu Francisko hapa mjini Vatican. Ratiba elekezi ya maadhimisho ya Sherehe za Noeli kwa Mwaka 2020 hadi mwaka 2021. Hizi ni Ibada zitakazoongozwa na Baba Mtakatifu Francisko hapa mjini Vatican.  (ANSA)

Papa Francisko: Ratiba Elekezi Maadhimisho ya Noeli 2020-2021

Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kuongoza mkesha wa Sherehe za Noeli tarehe 24 Desemba 2020 kuanzia saa 1:30 kwa saa za Ulaya. Noeli tarehe 25 Desemba 2020 majira ya saa 6:00 mchana, atatoa ujumbe wa "Urbi et Orbi. Tarehe 31 Desemba 2020 ataongoza "Te Deum". Tarehe Mosi Januari Sherehe ya Bikira Maria Mama wa Mungu. Sherehe ya Epifania, tarehe 6 Januari 2021.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Sherehe ya Noeli hasa kwa mwaka 2020 ni muda muafaka kwa watu wa Mungu kujenga na kudumisha udugu wa kibinadamu; ukomavu wa imani na mshikamano wa upendo kwa maskini na wahitaji zaidi. Hiki ni kipindi ambacho Mama Kanisa anakumbuka kuzaliwa kwa Kristo Yesu, kielelezo cha huruma na upendo wa Mungu kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti! Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 24 Desemba 2020, Kesha la Noeli, anatarajiwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kuanzia saa 1:30 za Usiku kwa saa za Ulaya. Baba Mtakatifu katika Waraka wa Kitume “ADMIRABILE SIGNUM” yaani “Ishara ya Kushangaza”: Maana na Umuhimu wa Pango la Noeli” anapembua kwa kina na mapana mazingira ya giza na kimya kikuu kinachotanda usiku wa manane, kielelezo cha watu wanaotembea katika giza na uvuli wa mauti. Hali hii inawafanya watu kudhani kwamba, Mwenyezi Mungu amewasahau waja wake na kwamba, maisha hayana tena thamani hasa baada ya watu kuguswa na kutikiswa na maambukizi makubwa ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Huu ni usiku wa upendo, mshikamano kama chemchemi ya imani na matumaini kwa watu waliovunjika na kupondeka moyo!

Mwenyezi Mungu ndiye asili na hatima ya binadamu. Lakini mwanga utokao juu umewafikia na kuwaangaza wakaao katika giza na uvuli wa mauti. Mazingira ya Pango la Noeli yanaonesha magofu ya nyumba za kale kama ilivyokuwa kwa mji wa Bethlehemu uliogeuka kuwa ni makazi ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu. Magofu haya ni utambulisho wa mateso, mahangaiko, kuteleza, kuanguka kwa binadamu, kumezwa na malimengu na hatimaye, kujikuta akiwa amekata tamaa. Uwepo wa Kristo Yesu katika mazingira na hali kama hii unapania kupyaisha, kuganga na kutibu hali ya maisha ya binadamu ili yaweze kurejea tena katika mng’ao wake asilia. Ni mazingira yanayowaonesha wafugaji na mifugo yao, wanaofurahia kuzaliwa kwa Masiha, Mkombozi wa ulimwengu. Baba Mtakatifu Francisko tarehe 25 Desemba 2020, kuanzia saa 6:00 za Mchana kwa Saa za Ulaya, atatoa salam kwa ajili ya mji wa Roma na Ulimwengu katika ujumla wake, maarufu kama “Urbi et Orbi”. Hili ni tukio ambalo linawawezesha watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia kuunganika na Baba Mtakatifu kwa njia ya vyombo mbali mbali vya mawasiliano pamoja na mitandao ya kijamii ili kusikia kwa muhtasari ujumbe wa amani, upendo na matumaini kwa kugusa baadhi ya matukio matukio makubwa yaliyoitikisa dunia katika maeneo haya na mwelekeo mpya unosheheni mwanga wa matumaini.

Tarehe 31 Desemba 2020, Baba Mtakatifu Francisko kuaniza saa 11:00 Jioni kwa saa za Ulaya ataadhimisha Masifu ya Jioni, Sherehe ya Bikira Maria Mama wa Mungu, "Theotokos". Katika Ibada hii, waamini watapata nafasi ya kuimba na kumshukuru Mungu, “Te Deum” ambao ni maarufu wakati wa kufunga Mwaka licha ya changamoto kubwa ambazo zimwesababishwa na gonjwa la Corona, COVID-19. Baba Mtakatifu katika Waraka wa Kitume “ADMIRABILE SIGNUM” yaani “Ishara ya Kushangaza”: Maana na Umuhimu wa Pango la Noeli” Uwepo wa Mungu kwenye Pango la Noeli ni chachu ya mabadiliko makubwa yanayoleta matumaini pamoja na kukuza utu, heshima na haki msingi za binadamu. Kumbe, kuna haja ya kushirikishana na maskini utajiri na karama mbali mbali ambazo Mwenyezi Mungu amewakirimia waja wake, ili kujikita zaidi katika ujenzi wa utu na udugu wa kibinadamu ambamo, hakuna mtu anayetengwa wala kusukumizwa pembezoni mwa jamii. Waamini hupenda kupamba Pango la Noeli kwa sanamu za watu mbali mbali hata pengine hawana uhusiano wa karibu sana na simulizi za Injili.

Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume: "Fratelli Tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” anasema, ulimwengu umegubikwa na giza nene la ubinafsi kiasi kwamba, bado kuna watu wanathubutu kutembea katika giza totoro, lakini wapo pia wale wanaothubutu kuota ndoto ya matumaini kwa kujielekeza zaidi katika ujenzi wa udugu na urafiki wa kijamii. Leo hii dunia inashuhudia Vita ya Tatu ya Dunia ikiendelea kurindima vipande vipande sehemu mbali mbali za dunia. Soko huria linalokita mizizi yake katika faida kubwa linaonekana kuishinda siasa safi; na utamaduni wa kutupa unaonekana kuendelea kushamiri. Kilio cha Mama Dunia kuhusu uharibifu wa mazingira sanjari na kilio cha maskini duniani vinaendelea kugonga mwamba! Kilio cha maskini wanaopoteza maisha kwa baa la njaa, bado hakijasikilizwa, lakini kuna mtu mwenye ujasiri anayependa kuwaonesha walimwengu njia madhubuti ya ujenzi wa dunia mpya inayojikita katika utu na heshima ya binadamu.

Yote haya ni mambo yanayowahamasisha watu wa Mungu kushuhudia: Utakatifu na furaha ya maisha ya kila siku, kielelezo cha ushiriki wa Umungu wa Kristo katika hali na maisha ya binadamu. Baba Mtakatifu anasema, Bikira Maria Mama wa Mungu anayeoneshwa huku akiyatafakari matendo makuu ya Mungu, ni mtumishi wa Bwana aliyekubali kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yake. Akawa kweli ni Mama na Bikira na mwaliko kwa waamini kutii na kutekeleza yale yote wanayoambiwa na Kristo Yesu. Mtakatifu Yosefu, Baba mlishi na mlinzi mwaminifu wa Familia Takatifu ni mwalimu wa kwanza wa Mtoto Yesu aliyempenda kwa moyo wa Kibaba!

Baba Mtakatifu Francisko katika katika Waraka wake wa Kitume “Patris Corde” yaani “Kwa Moyo wa Kibaba”: “Mwaka wa Mtakatifu Yosefu, Kumbukumbu ya Miaka 150 Tangu Mtakatifu Yosefu alipotangazwa Kuwa Msimamizi wa Kanisa la kiulimwengu” uliozinduliwa rasmi tarehe 8 Desemba 2020 na unatarajiwa kufungwa tarehe 8 Desemba 2021 anataja sifa kuu za Mtakatifu Yosefu kuwa ni “Baba mpendelevu, mwenye huruma na mapendo; mtiifu na mwepesi kukubali. Ni Baba alibahatika kuwa na kipaji cha ugunduzi na ujasiri, lakini alibaki akiwa amefichwa kwenye vivuli, akawajibika na kuwa ni chanzo cha furaha na sadaka binafsi. Katika unyenyekevu Mtakatifu Yosefu aliyahifadhi mafumbo yote ya maisha yaliyomzunguka Mtoto Yesu na Mama yake Bikira Maria. Yosefu mtu wa haki, akajiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu na kuyatekeleza yale yote aliyoambiwa! Pango la Noeli linakamilika kwa uwepo wa Mtoto Yesu anayepyaisha mazingira yote. Mwenyezi Mungu anaonekana kama Mtoto mchanga anayetaka kuwabeba waja wake mikononi mwake. Anafunua nguvu na uweza wake unaoumba na kuleta mageuzi makubwa. Hii ni nguvu inayofunua ukuu wa upendo wake usiokuwa na mipaka, kwa kutabasamu na kuwakunjulia watu mikono yake. Mtoto Yesu anaonesha Fumbo la maisha ya binadamu kiasi kwamba, hata Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu walihisi uwepo wa Mungu kati yao.

Tarehe 1 Januari 2021, Sherehe ya Bikira Maria Mama wa Mungu sanjari na Siku ya 54 ya Kuombea Amani Duniani ambayo kwa mwaka 2021  Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko unaongozwa na kauli mbiu: Utamaduni wa Kutunza Kama Njia ya Amani. Baba Mtakatifu anafafanua kwa kusema kwamba, Mwenyezi Mungu ni kiini cha wito wa binadamu kutunza. Mwenyezi Mungu Muumbaji ni mfano bora wa kutunza unaoshuhudiwa pia katika utume wa Kristo Yesu na hatimaye, kunafsishwa katika utamaduni wa kutunza unaoshuhudiwa na wafuasi wa Yesu. Utunzaji ni kiini cha Mafundisho Jamii ya Kanisa mintarafu utamaduni wa kutunza unaohimiza: utu na haki msingi za binadamu; utunzaji wa mafao ya wengi; utunzaji kwa njia ya mshikamano pamoja na mchakato wa utunzaji bora wa mazingira, dira ya njia ya pamoja. Kumbe, kuna haja ya kuwafunda watu utamaduni wa kutunza kwani hakuna amani, ikiwa kama hakuna utamaduni wa kutunza na kujaliana!

Malaika wa Bwana na nyota angavu ni mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kwenda kumwabudu Mwana wa Mungu. Wachungaji wakawa ni watu wa kwanza kuona zawadi ya ukombozi. Maskini na wanyenyekevu wa moyo wakashuhudia Fumbo la Umwilisho. Kwa njia ya Kristo Yesu, Mwenyezi Mungu akapata tena nafasi ya kukutana na watoto wake katika mazingira ya Pango la Noeli. Mazingira ya Pango la Noeli kwa kawaida yanapaswa kuonesha uwepo wa maskini wanaothamini zaidi ufukara wa maisha ya kiroho. Hawa pia wanayo haki ya kuwa karibu na Mtoto Yesu na wala asiwepo mtu anayetaka kuwafukuzia mbali! Katika muktadha huu, nyumba au familia inakuwa ni mahali pa ukarimu kwa maskini, kwa sababu hawa ndio watu wa kwanza kabisa kutambua uwepo wa Mungu kati ya waja wake na hawa kimsingi ndio walengwa wa Habari Njema ya Wokovu. Pango la Noeli ni ukumbusho kwamba, utajiri na raha za dunia ni mambo mpito.

Jumatano tarehe 6 Januari 2021, Sherehe ya Tokeo la Bwana, Epifania “'Eπιφάνια” ni kielelezo cha ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa watu wa Mataifa. Ni Sherehe inayoonesha kwamba, Kristo Yesu ndiye mwanga angavu wa Mataifa.  Sherehe ya Tokeo la Bwana pia ni Siku ya Utoto Mtakatifu, mwaliko kwa watoto kumtazama Mtoto Yesu, ili aweze kuwaongoza katika utume wao wa: sala, udugu, ushirikiano na mshikamano na watoto wenzao ambao ni wahitaji zaidi. Katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kuongoza Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kuanzia saa 4:00 Asubuhi kwa saa za Ulaya. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka huu wa Kitume “ADMIRABILE SIGNUM” yaani “Ishara ya Kushangaza”: Maana na Umuhimu wa Pango la Noeli” anasema, inapokaribia Sherehe ya Tokeo la Bwana, au Epifania, sanamu za Mamajusi watatu kutoka Mashariki zinawekwa kwenye Pango la Noeli. Hawa ni wataalam wa nyota kutoka Mashariki waliojitaabisha kumtafuta Mtoto Yesu na hatimaye walipomwona wakamzawadia: Ubani unaonesha Umungu wa Kristo; Manemane ni ushuhuda wa ubinadamu wa Kristo utakaokabiliwa na mateso, kifo na ufufuko kwa wafu. Dhahabu ni kielelezo cha Ufalme wa Kristo Yesu, yaani; Ufalme wa kweli na uzima; Utakatifu na neema; haki, upendo na amani. Kila mwamini anahimizwa kuwa kweli ni shuhuda na chombo cha matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama chemchemi ya furaha na amani inayobubujika kutoka kwa Mtoto Yesu.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Mamajusi kutoka Mashariki ya mbali ni kielelezo cha watu kutoka katika medani mbali mbali za maisha, wenye kiu ya kutaka kukutana na Mfame wa amani, anayetuliza kiu yao ya ndani. Wanapomwona Mfalme katika hali ya Mtoto mchanga, kamwe hawashangazwi wala kuona kama hii ni kashfa ya mwaka, bali wanampigia magoti na kumwabudu kwa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu ambaye ni chemchemi ya hekima yote ndiye aliyewaongoza kwa kutumia nyota angavu hadi kumfikia. Huyu ndiye yule Mungu anayewaangusha wakuu katika viti vyao vya enzi na kuwakweza wanyonge. Bila shaka, Mamajusi waliporejea makwao waliweza kuwashirikisha wengine matendo makuu ambayo Mwenyezi Mungu aliwatendea katika maisha yao. Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha Waraka huu wa Kitume “ADMIRABILE SIGNUM” yaani “Ishara ya Kushangaza”: Maana na Umuhimu wa Pango la Noeli” kwa kusema, Pango la Noeli ni muhimu sana katika mchakato wa kurithisha imani mintarafu historia na mazingira ya watu husika. Ni changamoto na mwaliko wa kuendelea kushirikishana mang’amuzi na uzoefu huu kwa kusimulia kuhusu ufunuo wa upendo wa Mungu katika maisha ya mwanadamu.

Ratiba ya Noeli 2020-2021

 

19 December 2020, 15:17