Tafuta

Mwaka wa Furaha ya Upendo Ndani ya Familia: Famiglia Amoris Laetitia utazinduliwa rasmi tarehe 19 Machi 2021 na kuhitimishwa tarehe 26 Juni 2022 mjini Roma. Mwaka wa Furaha ya Upendo Ndani ya Familia: Famiglia Amoris Laetitia utazinduliwa rasmi tarehe 19 Machi 2021 na kuhitimishwa tarehe 26 Juni 2022 mjini Roma. 

Papa Francisko:Mwaka wa Furaha ya Upendo Ndani ya Familia 2021-2022

Kumbukumbu ya Miaka 5 tangu kuchapishwa kwa Wosia wake wa Kitume: “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya Upendo ndani ya familia”, tarehe 19 Machi 2021 itakuwa ni siku ya kuzindua Mwaka wa Furaha ya Upendo Ndani ya Familia, “Famiglia Amoris Laetitia” utakaohitimishwa wakati wa maadhimisho ya Siku ya X ya Familia Duniani itakayoadhimishwa Roma tarehe 26 Juni, 2022.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kama sehemu ya maadhimisho ya kumbukumbu ya Miaka 5 tangu Baba Mtakatifu Francisko achapishe Wosia wake wa Kitume: “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya Upendo ndani ya familia”, hapo tarehe 19 Machi 2021 ametangaza kwamba, itakuwa ni siku ya kuzindua Mwaka wa Furaha ya Upendo Ndani ya Familia, “Famiglia Amoris Laetitia” utakaohitimishwa wakati wa maadhimisho ya Siku ya X ya Familia Duniani itakayoadhimishwa mjini Roma tarehe 26 Juni, 2022 kwa kuongozwa na kauli mbiu: “Upendo wa familia: wito na njia ya utakatifu”. Baba Mtakatifu anatarajia kuhudhuria na kushiriki kikamilifu katika matukio yote haya! Hii ni changamoto na mwaliko kwa watu wote wa Mungu sehemu mbalimbali za dunia kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa furaha ya upendo ndani ya familia. Wosia huu wa Kitume: “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya Upendo ndani ya familia”, ni matunda ya mwanga wa Neno la Mungu unaozingatia ukweli na changamoto za maisha ya ndoa na familia katika ulimwengu mamboleo. Unatoa mwelekeo wa Kristo Yesu katika kukuza tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, ili kuzijengea familia uwezo wa kutangaza na kushuhudia Injili ya familia.

Mwaka wa Furaha ya Upendo Ndani ya Familia anasema Baba Mtakatifu Francisko ni muda muafaka kwa familia ya Mungu kurejea tena na kufanya tafakari ya kina kuhusu Wosia huu ambao unakazia: Upendo thabiti ndani ya familia; upendo unaogeuka kuwa ni chemchemi na asili ya maisha. Baba Mtakatifu anatoa mapendekezo yanayopaswa kufanyiwa kazi katika sera na mikakati ya shughuli za kichungaji, mintarafu utume wa maisha ya ndoa na familia. Anawahimiza wazazi na walezi kuimarisha elimu, malezi na makuzi ya watoto wao, ili waweze kuwajibika kikamilifu katika maisha yao. Ni wajibu wa Kanisa kuwasindikiza, kung’amua na kuwasaidia wanafamilia wanaolegalega katika maisha na wito wao wa ndoa na familia. Tafakari hii ifanywe kwa msaada wa nyenzo mbalimbali za shughuli za kichungaji kwa kusikiliza na kuyafanyia kazi mapendekezo yanayotolewa na watu wa Mungu. Mkazo utolewe kwenye maandalizi ya wana ndoa watarajiwa, elimu kuhusu maana na mahusiano ya kimaumbele miongoni mwa vijana wa kizazi kipya.

Waamini waelimishwe zaidi kuhusu: Ukuu, ukweli, uzuri, utakatifu na dhamana ya maisha ya ndoa na familia katika jamii. Iwe ni nafasi ya kuadhimisha makongamano ya kitaifa na kimataifa kuhusu: upendo wa familia, wito na njia ya utakatifu ili kukabiliana na changamoto mambaoleo zinazoendelea kuibuka kila kukicha kutokana na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia. Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha kuanzia sasa limetayarisha nyaraka mbalimbali zinazoweza kuwa msaada katika maandalizi na hatimaye, maadhimisho ya  Mwaka wa Furaha ya Upendo Ndani ya Familia, “Famiglia Amoris Laetitia”. Unaweza kupata habari zaidi kwa kupekua katika tovuti ya Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha kwa anuani ifuatayo: www.amorislaetitia.va. Tovuti hii itakuwa inapyaishwa kila wakati ili kutoa habari na ushauri motomoto kama unavyopokelewa kutoka sehemu mbalimbali za dunia.

Lengo kuu la Maadhimisho ya Mwaka wa Furaha ya Upendo Ndani ya Familia, “Famiglia Amoris Laetitia”. Kujitahidi kumwilisha furaha ya Injili katika uhalisia wa maisha ya waamini, tayari kujitoa na kujisadaka kuwa ni chemchemi ya furaha kwa ndugu, jamaa na jirani; zawadi kubwa kwa Mama Kanisa na jamii katika ujumla wake. Hii ni nafasi ya kutangaza na kushuhudia umuhimu wa Sakramenti Takatifu ya Ndoa, tayari kushiriki ujenzi wa familia kama Kanisa dogo la nyumbani. Ni Sakramenti inayopyaisha upendo wa kibinadamu. Baba Mtakatifu analitaka Kanisa kuhakikisha kwamba, linatoa kipaumbele cha kwanza katika maisha na utume wake familia na vijana, kwa kukazia malezi, katekesi na majiundo awali na endelevu kama sehemu ya mchakato wa ukomavu wa imani inayoweza kutolewa ushuhuda wa maisha. Maadhimisho ya Maadhimisho ya Mwaka wa Furaha ya Upendo Ndani ya Familia, “Famiglia Amoris Laetitia” liwe ni tukio shirikishi, litakalowagusa wana familia wote, kadiri ya wito na wajibu wao ndani ya familia, Kanisa na jamii katika ujumla wake. Maadhimisho haya yakoleze ari na mwamko wa maandalizi kwa wanandoa, kwa kuwasindikiza wanandoa wapya katika maisha na utume wao.

Wazazi wapewe katekesi kuhusu dhamana na wajibu wao wa malezi: kiroho, kiutu na kitamaduni, ili waweze kutekeleza wajibu huu kwa umakini zaidi. Wazazi wafundwe na wapewe nafasi ya kushirikisha: matatizo, changamoto, uzuri, ukuu na utakatifu wa maisha ya ndoa na familia, ili kutambua na hatimaye, kumwilisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, kwa kutangaza, kushiriki na kushuhudia mambo msingi katika maisha ya ndoa na familia. Wazee na wanandoa wapya waangaliwe kwa jicho la kichungaji. Tema kama vile: familia, wito wa kitawa na kipadre; useja, Injili ya uhai, utamaduni wa kifo; umuhimu na madhara ya kutumia mitandao ya kijamii; ufukara wa Kiinjili na umaskini wa hali na kipato; utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Maadhimisho haya yawakumbuke na kuwashirikisha watoto ambao ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Maadhimisho ya Mwaka wa Furaha ya Upendo Ndani ya Familia, “Famiglia Amoris Laetitia” usaidie kujenga na kuimarisha mahusiano na mafungamano kati ya familia na Kanisa, kwa kuwashirikisha zaidi wanandoa katika maisha na utume wa Kanisa. Malezi na katekesi ya kina, itolewe kwa mihimili yote ya Uinjilishaji, ili kukabiliana barabara na matatizo, changamoto na fursa mbalimbali zinazoendelea kuibuliwa katika maisha ya ndoa na familia. Jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, familia kama Kanisa dogo la nyumbani linaimarishwa zaidi, kwa kutambua dhamana na utume wake usiokuwa na mbadala! Ni wakati wa kukuza na kuhamasisha wito wa kimisionari ndani ya familia, kwa kuwajengea wazazi na walezi uwezo wa kufundisha na kuwarithisha watoto wao: imani na tunu msingi za Kiinjili; kwa kuwaandaa kikamilifu tangu awali kushiriki na kujisadaka katika maisha ya ndoa na familia, bila kusahau wito wa Daraja Takatifu. Kumbukizi ya ndoa iwe ni fursa ya kupyaisha tena katekesi na maagano ya ndoa, ili kuweza kuyatafakari yaliyopita kwa moyo wa shukrani, kuyaishi ya sasa kwa moyo wa hamasa na kuyakumbatia ya mbeleni kwa moyo wa matumaini.

Mwaka wa Furaha ya Familia
27 December 2020, 16:27