Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko anasema, mabahari, wavuvi pamoja na familia zao ni kati ya makundi yaliyoathirika sana kutokana na Virusi vya Corona, COVID-19. Baba Mtakatifu Francisko anasema, mabahari, wavuvi pamoja na familia zao ni kati ya makundi yaliyoathirika sana kutokana na Virusi vya Corona, COVID-19.  (ANSA)

Papa: Mabaharia na Wavuvi Wameathirika Sana na COVID-19

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana Jumapili tarehe 20 Desemba 2020 amebainisha kwamba, kuna zaidi ya mabaharia na wavuvi 400, 000 kutoka sehemu mbali mbali za dunia ambao wameathirika sana kutokana na Virusi vya Corona, COVID-19. Wamezuliwa kwenye vyombo vyao vya kazi hata kama muda na mikataba yao ya kazi imekwisha. Mshikamano!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Jumuiya ya Kimataifa inapitia kipindi kigumu katika historia yake kutokana na janga kubwa la homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Maisha na kazi ya mabaharia, wavuvi pamoja na familia zao yameonesha umuhimu wake wa pekee katika kipindi hiki, kwa sababu wamesaidia sana kutoa chakula pamoja na mahitaji msingi kwa watu sehemu mbali mbali za dunia. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuchukua fursa hii, kuwapongeza na kuwashukuru kwa sadaka na majitoleo yao. Anatambua fika hatari za maisha wanazokumbana nazo katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku. Katika miezi ya hivi karibuni, maisha na kazi za mabaharia pamoja na wavuvi zimebadilika sana, kwa sababu wanapaswa kuendelea kujisadaka zaidi bila ya kujibakiza. Wametumia muda mrefu zaidi wakiwa kwenye vyombo vyao bila ya kuruhusia kutua nanga kwa hofu ya kusambaza maambukizi mapya ya Virusi vya Corona, COVID-19. Wameendelea kufanya kazi katika mazingira magumu na hatarishi kwa kutengwa na ndugu, jamaa, marafiki na hata nchi zao wenyewe.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili tarehe 20 Desemba 2020 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, amebainisha kwamba, kuna zaidi ya mabaharia na wavuvi 400, 000 kutoka sehemu mbali mbali za dunia ambao wameathirika sana kutokana na Virusi vya Corona, COVID-19. Wamezuliwa kwenye vyombo vyao vya kazi hata kama muda na mikataba yao ya kazi imekwisha. Baba Mtakatifu anamwomba Bikira Maria, Nyota ya Bahari kuwakumbuka na kuwaombea wafanyakazi hawa. Wakati huo huo, Baba Mtakatifu anaziomba Serikali mbalimbali duniani, kuhakikisha kwamba, mabaharia na wavuvi hawa wanarejea tena makwao salama salimini. Kwa mara nyingine tena, mabaharia na wavuvi wanakumbushwa kwamba, matatizo na changamoto zote hizi si rahisi sana kwa wao kuweza kuzibeba na hasa katika kipindi hiki! Baba Mtakatifu anapenda kuwahakikishia kwamba, wasidhani wako pweke na kwamba, wamesahauliwa.

Kwa njia ya maisha na utume wao baharini unaweza kuwajengea mazingira kwamba, wako pweke, lakini watambue kwamba, Baba Mtakatifu Francisko anawahifadhi na kuwaombea kila wakati kutoka katika undani wa moyo wake. Sala hii inasindikizwa pia na wahudumu wa maisha ya kiroho pamoja na watu wa kujitolea wanaotekeleza dhamana na wajibu wao kwenye Utume wa Bahari, maarufu kama “Stella Maris” yaani “Nyota ya Bahari”. Injili Takatifu inawakumbusha waamini kwamba, Mitume wa kwanza wa Kristo Yesu, walikuwa ni wavuvi. Baba Mtakatifu anapenda kutumia fursa hii, kuwapatia ujumbe; sala ya matumaini na faraja mintarafu matatizo na changamoto mbali mbali wanazokabiliana nazo katika maisha na utume wao. Anapenda pia kuwatia shime, wahudumu wa maisha ya kiroho na watu wa kujitolea, wanaoshirikiana nao bega kwa bega katika utume wa bahari kwa ajili ya mabaharia na wavuvi.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kutembelea Pango la Noeli kwa Mwaka 2020 ambalo kwa mwaka huu lina Mapango ya Noeli 100 yanayotoa katekesi ya imani ya watu wa Mungu. Mapango haya ya Noeli yamepambwa kuzunguka Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Hii ni fursa ya kutambua jinsi ambavyo waamini kwa njia ya sanaa wanatafuta kulielezea Fumbo la Umwilisho, jinsi Kristo Yesu alivyozaliwa mjini Bethlehemu. Mapango ya Noeli ni katekesi ya imani ya Kanisa. Baba Mtakatifu amewatakia waamini, mahujaji na wageni wote kutoka ndani na nje ya Italia waliohudhuria kwenye Sala ya Malaika wa Bwana, heri na baraka katika maandalizi ya Sherehe za Noeli kwa Mwaka 2020.

Hiki kiwe ni kipindi cha toba na wongofu wa ndani, sala na ushuhuda wa imani unaomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, ili kujenga na kudumisha udugu wa kibinadamu. Mateso na mahangaiko ya Kristo Yesu kwenye Pango la Noeli, iwe ni changamoto ya kutoa huduma ya mapendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Ni wakati wa kujenga na kudumisha mshikamano wa upendo wa udugu wa kibinadamu. Kwa njia hii, waamini na watu wote wenye mapenzi mema, wataweza kukutana mubashara na Kristo Yesu Mkombozi wa Ulimwengu. Mkesha wa Noeli, uwe ni mwanzo wa tafakari ya Fumbo la Umwilisho kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu.

Pango la Noeli 2020

 

 

 

 

20 December 2020, 15:35