Tafuta

Sala ya Malaika wa Bwana Sala ya Malaika wa Bwana 

Papa Francisko:Kanuni ya mkristo ni kuwa na furaha!

Katika Dominika ya tatu ya Majilio,tarehe 13 Desemba na ambayo imeangukia katika kumbukizi la miaka 51 ya ukuhani wa Papa Francisko,amezungumzia Injili ya Siku ambapo anatazama Yohane Mbatizaji kama kiongozi wa wakati wake aliyeishi kwa matarajio na furaha ya kuona anafika Masiha huku akielekeza wote kumfuata Yesu.Mkristo daima anaishi kwa furaha na ndiyo tabia ya imani.

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican.

Kwa kuongozwa na Injili ya Siku, Papa Francisko wakati wa tafakari yake kabla ya sala ya Malaika wa Bwana, tarehe 13 Desemba 2020 na ambayo kwa namna ya pekee ni siku ya kumbukizi la miaka 51 tangu Papa apewe daraja la kikuhani amesisitizia furaha ya kikristo kama muktadha wa Liturujia ya siku. Akianza amesema,“mwaliko wa furaha ndiyo kiini cha kipindi cha Majilio. Matarajio ya kuzaliwa kwa Yesu, matajario ambayo sisi tunaishi ni furaha ambayo kidogo tunaweza kusema kama vile tunapokuwa tunasubri kutembelewa na mtu ambaye tunampenda sana, kwa mfano rafiki ambaye hatujaonana  kwa siku nyingi na ndugu… daima tunakuwa na subira”. Ukuu huu wa furaha unajikita hasa leo hii katika Dominika ya tatu ambayo inafunguliwa na ushauri wa Mtakatifu Paulo katika utangulizi kwamba “ Furhaini katika Bwana daima ( Fil 4,4.5) Furahini ni  furaha ya kikristo.   

Je! Ni kwa sababu gani ya kuwa na furaha hii?  Papa amesema ni kwa sababu “Bwana yu karibu”. Kadiri Bwana anavyokuwa karibu, ndivyo tunakuwa na furaha; kadiri Yeye anavyokuwa mbali, ndiyo tunakuwa na huzuni zaidi. Hii ndiyo kanuni ya wakristo.  Papa ametoa mfano kuwa Mfalsafa mmoja alikuwa anasema kitu karibu sana na hiki: “Mimi sijuhi namna gani ya kuamini leo hii, kwa sababu wale ambao wanasema wanaamini, lakini wana sura za mkesha wa maombolezo”. Hawa hawatoi ushuhuda wa furaha ya ufufuko wa Yesu Kristo. Wakristo wengi ni wenye sura kama hiyo, Papa amekazia na wanafanya kana kwamba ni mkesha wa maombozezi, kuwa na uso wa huzuni… Lakini Kristo amefufuka! Kristo anakupenda! Na wewe hauna furaha? Ka maana hiyo Papa Francisko ameshauri kufikiria kidogo na kujitafakari kama unayo furaha kwa sababu Bwana yu karibu nawe, kwa sababu Bwana anakupenda na kwa sababu Bwana alikukomboa.

Injili ya Yohane imewakilisha mtu wa kibiblia na pia  Maria na Mtakatifu Yosefu ambao walikuwa wa kwanza kuishi subira ya Masiha na furaha ya kumwona anafika. Na mtu huyo mtu  huyo pia ni Yohane Mbatizaji (Yh 1,6-8.19-28). Mwinjili anamwakilisha kwa namna kuu kwamba “aliikuwa mtu aliyetumwa na Mungu (…). Alikuja kama shuhuda ili kushuhudia nuru. Mbatizaji alikuwa shuhuda wa kwanza wa Yesu, kwa Neno na kwa zawadi ya maisha. Injili zote zinakumbusha katika kumwonesha jinsi alivyoweza kutimiza utume wake  akielekeza Yesu kama Kristo, aliyetumwa na Mungu kama ahadi illiyotangazwa na manabii. Yohane mbatizaji alikuwa kiongozi wa wakati wake. Umaarufu wake ulikuwa umeenea Yudea yote na zaidi hadi kufikia Galilaya. Lakini Yeye hakushawishika hata kidogo kujiweka kipaumbele, bali  daima aliwaelekeza kwa Yesu ambaye alikuwa afike.

Yohane alikuwa amesema: “Mimi sistahili kuilegeza gidamu ya kiatu chake”. Daima alikuwa akielekeza kwa Bwana. Kama vile Maria aliyekuwa daima alielekeza kwa Bwana na  kusema:“ Fanyeni atakayowaeleza”. Daima Bwana yuko katikati. Watakatifu waliomzunguka, walielekeza kwa Bwana. Hasiye mwelekeza Bwana siyo mtakatifu! Papa amesisitiza.  Hali ya kwanza ya Mkristo Papa amesema ni kujivua umimi na kumweka Yesu katikati. Hii sio kutengwa, kwa sababu Yesu ndiye kitovu, yeye ndiye nuru inayotoa maana kamili ya maisha ya kila mwanamume na mwanamke anayekuja ulimwenguni. Ni nguvu sawa ya upendo, ambayo unisaidia nitoke ndani ya umimi ili  nisijipoteze, lakini nijitafute wakati ninajitoa, wakati ninatafuta mema ya mwingine.

Yohane mbatizaji alifanya mchakato wa njia ndefu ili kufikia kushuhudia Yesu. Safari ya furaha siyo matembezi rahisi. Inahitaji kazi ya kuwa na furaha daima. Yohane aliacha yote tangu akiwa kijana ili kuweka Mungu katika  nafasi ya kwanza, kwa kumsikiliza kwa moyo wote na nguvu ya Neno lake. Yohane alikwenda kwenye jangwa akajivua kila kitu ili aweze kuwa huru na kufuata upepo wa Roho Mtakatifu. Kiukweli tabia zake nyingine ni za kipekee, zisizoweza kurudiwa, hazipatikani kwa kila mtu. Na ushuhuda wake ni kielelezo kwa kila mtu ambaye anataka kutafuta maana ya maisha yake na kupata furaha ya kweli. Hasa, Mbatizaji ni mfano kwa wale walio katika Kanisa ambao wameitwa kumtangaza Kristo kwa wengine. Hawa wanaweza kufanya hivyo tu kwa kujitenga kwao na kutoka katika ulimwengu, sio kwa kuwavutia watu kwao bali kwa kuwaelekeza kwa Yesu. Papa amebainisha.

Kwa kuhitimisha Papa Francisko amesema, furaha ndiyo hiyo ya kuelekeza kwa Yesu. Furaha inapaswa iwe ndiyo tabia ya imani yetu. Hata wakati ambao furaha ni kidogo, ni lazima kujua kuwa Bwana yuko nami na Bwana yuko nasi ambaye amefufuka. Bwana ndiyo kiini cha maisa yetu na ndiyo kiini cha furaha yetu. Ushauri ni kufikiria vema jinsi gani ninashi? Je mimi ni mtu mwenye furaha na kueneza kama mkristo au niko kama wale ambao daima wana huzuni utafikiri ni uso wa maombolezo? Ikiwa sina furaha ya imani yangu, siwezi kutoa ushuhuda na wengine watasema “ ikiwa imani ni huzuni namna hiyo ni bora kutokuwa nayo”. Katika kusali sala ya Malaika wa Bwana, tunaona kuwa hilo liliwezekana kwa njia ya Bikira Maria, ambaye alisubiri kwa ukimya Neno la wokovu wa Mungu: alilisikiliza, alilipokea na kulitunza. Kwake yeye katika Mungu aliyejifanya kuwa karibu, Kanisa linamwita: "Maria sababu ya furaha yetu”.

13 December 2020, 13:38