Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko amewaandikia watu wa Mungu nchini Lebanon  waraka wa matumaini na faraka, akitumaini kuwatembelea hali itakapokuwa shwari! Baba Mtakatifu Francisko amewaandikia watu wa Mungu nchini Lebanon waraka wa matumaini na faraka, akitumaini kuwatembelea hali itakapokuwa shwari! 

Papa Francisko: Waraka wa Noeli 2020 Kwa Wananchi wa Lebanoni!

Lengo la Waraka huu ni kutaka kuwafariji na kuwatia shime wakati huu, Mama Kanisa anapoadhimisha Sherehe ya Kuzaliwa kwa Kristo Yesu, Mfalme wa amani. Baba Mtakatifu anakazia kuhusu mateso ya watu watu wa Mungu; Lebanon katika Maandiko Matakatifu, mwaliko kwa viongozi wa kisiasa na kidini pamoja na nia yake ya kutembelea Lebanon, pale hali itakapokuwa shwari.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko kupitia kwa Kardinali Béchara Boutros Raï, Patriaki wa Kanisa la Wamaroniti Wakatoliki nchini Lebanon, amewaandikia watu wa Mungu nchini Lebanon Waraka wa matashi mema kwa Maadhimisho ya Sherehe za Noeli kwa Mwaka 2020. Lengo la Waraka huu ni kutaka kuwafariji na kuwatia shime wakati huu, Mama Kanisa anapoadhimisha Sherehe ya Kuzaliwa kwa Kristo Yesu, Mfalme wa amani. Baba Mtakatifu pamoja na mambo mengine, anakazia kuhusu mateso na mahangaiko ya watu wa Mungu nchini Lebanon, Lebanon katika Maandiko Matakatifu, mwaliko kwa viongozi wa kisiasa na kidini pamoja na nia yake ya kutembelea Lebanon, pale hali itakapokuwa shwari. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake kwa familia ya Mungu nchini Lebanon, anasema anasikitika sana kuona jinsi ambavyo wananchi wa Lebanon wanavyoteseka, walivyopokonywa hata ile hali ya kuishi kwa amani na hivyo kushindwa kuendelea kuwa ni mashuhuda na vyombo vya uhuru, amani na maridhiano kati ya watu. Baba Mtakatifu anasema, anashiriki pamoja nao furaha, mateso na matumaini yao halali. Inasikitisha kuona kwamba, vijana wengi nchini Lebanon waliopokonywa matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi. Hawa ni kama watu wanaotembea katika uvuli wa dhambi na mauti. Lakini katika Maadhimisho ya Sherehe ya Noeli kama anavyosema Nabii Isaya, “Watu wale waliokwenda katika giza wameona nuru kuu; wale waliokaa katika nchi ya uvuli wa mauti, nuru imewaangazia” Isa. 9:2.

Huu ni mwanga wa imani na matumaini kwamba, Mwenyezi Mungu hataweza kuiacha Lebanon na atageuza mateso yake kuwa ni chemchemi ya wema! Na Mzaburi anakaza kusema, “Mwenye haki atastawi kama mtende, atakua kama mwerezi wa Lebanon.” Zab. 92:12. Katika Maandiko Matakatifu Mwerezi ni kielelezo cha uimara, uthabiti na ulinzi; kielelezo cha mtu mwadilifu ambaye amekita maisha yake kwa Mwenyezi Mungu na hivyo anakuwa ni alama ya uzuri, ustawi, kiasi hata cha kuzaa matunda mema hata wakati wa uzee! Mwenyezi Mungu katika kipindi hiki cha Noeli anataka kuambatana na kutembea pamoja na waja wake, ili kujenga ujirani mwema. Jambo la msingi ni kuamini uwepo wake endelevu na uaminifu wake. Baba Mtakatifu anawahimiza watu wa Mungu nchini Lebanon kujenga na kuzamisha mizizi yao katika umoja wa Kitaifa, ili kudumisha mshikamano wa kidugu; kwa kugundua na kuendeleza utambulisho wao kama Taifa. Kwa miaka mingi Lebanon imejipambanua kuwa ni taifa la watu wanaoheshimiana, wanaoishi katika umoja na maridhiano, licha ya tofauti zao msingi. Utambulisho wao umekuwa ni urithi mkubwa kwa wakimbizi na wahamiaji. Wananchi wa Lebanon wanayo ndoto ya leo na kesho iliyo bora zaidi.

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuwaalika na kuwakumbusha viongozi wa kisiasa na kidini kwamba, wao wana wajibu wa kutafuta na kuweka mbele masilahi ya wananchi wao, matendo yale si kwa ajili ya mafao binafsi, bali kwa ajili ya ustawi, maendeleo ya watu wa Mungu wanaowawakilisha. Mwishoni mwa Waraka wake, Baba Mtakatifu Francisko anaonesha nia ya kutaka kutembelea nchini Lebanon mapema iwezekanavyo, hali itakapokuwa shwari. Huu ni mwendelezo wa ushuhuda kutoka kwa watangulizi wake. Kwa mara nyingine tena, Baba Mtakatifu anawaalika viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kuisaidia Lebanon, ili kuweza kuondokana na vita pamoja na kinzani za Ukanda wa Mashariki ya Kati. Familia ya Mungu nchini Lebanon inaalikwa kuitazama kwa matumaini Nyota angavu ya Bethlehemu, ili iweze kuwaangaza na kuwatia shime, ili kutambua mpango wa Mungu katika maisha yao, ili kuimarika katika mapito na matumaini yao!

Papa Waraka Lebanon
24 December 2020, 14:43