Tafuta

Vatican News
Papa Francisko Maadhimisho ya Sherehe za Noeli ni wakati muafaka wa kujenga na kudumisha upendo, mshikamano na udugu wa kibinadamu. Papa Francisko Maadhimisho ya Sherehe za Noeli ni wakati muafaka wa kujenga na kudumisha upendo, mshikamano na udugu wa kibinadamu.  (Vatican Media)

Papa Francisko: Sherehe za Noeli: Upendo na Mshikamano wa Kidugu

Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema katika kipindi cha Noeli, kupyaisha upendo na ukarimu wao kwa maskini na wanyonge ndani ya jamii kwa kutambua kwamba, wote ni ndugu wamoja. Ni wakati muafaka pia kwa ajili ya kusali na kuziombea familia mbalimbali zinazoteseka kwa wakati huu kutokana na changamoto za maisha. Umoja na udugu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya salam zake kwa mji wa Roma na Ulimwengu katika ujumla wake, “Urbi et Orbi” wakati wa maadhimisho ya Sherehe ya Noeli tarehe 25 Desemba 2020, amewatakia waamini na watu wote wenye mapenzi mema heri na baraka za Sherehe ya Noeli, wale wote waliokuwa wamejiunga naye kwa njia ya vyombo vya mawasiliano na mitandao ya kijamii. Amewashukuru kwa uwepo wao wa kiroho katika maadhimisho ya Sherehe ya Noeli. Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema katika kipindi cha Noeli, kupyaisha upendo na ukarimu wao kwa maskini na wanyonge ndani ya jamii kwa kutambua kwamba, wote ni ndugu wamoja. Ni wakati muafaka pia kwa ajili ya kusali na kuziombea familia mbalimbali zinazoteseka kwa wakati huu kutokana na changamoto za maisha.

Katika kipindi hiki cha maadhimisho ya Sherehe za Noeli, Fumbo la Umwilisho, Kuzaliwa kwa Mwana wa Mungu, Mama Kanisa anawatakia watoto wake wote, amani na utulivu wa ndani, furaha na matumaini. Ni wakati wa kunafsisha utukufu wa Mungu na amani kwa watu anaowaridhia. Hizi ni tunu ambazo zinapaswa kutangazwa na kushuhudiwa na waamini kutoka katika sakafu ya nyoyo zao, zipambe na kumwilishwa katika jamii na familia ya binadamu katika ujumla wake. Kipaumbele cha kwanza ni maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii na hasa kutokana na maambukizi makubwa ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii katika maadhimisho ya Sherehe ya Noeli, 25 Desemba 2020 anasema, kuzaliwa kwa Kristo Yesu, Neno wa Mungu ni upya unaowawezesha waamini kila mwaka, kuzaliwa upya kutoka katika undani wa maisha yao, kwa kujipatia kutoka kwa Kristo Yesu, nguvu ya kukabiliana na matatizo pamoja na changamoto za maisha kwa ari na moyo mkuu! Katika maadhimisho ya Sherehe ya Noeli kwa Mwaka 2020, Baba Mtakatifu Francisko ametoa vifaa 4, 000 vya kupimia homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 kwa ajili ya kusaidia kuwapima maskini na watu wasiokuwa na makazi maalum mjini Roma, watu ambao usalama na maisha yao yako hatarini kutokana na maambukizi makubwa ya Virusi vya Corona, COVID-19.

Vifaa hivi ni zawadi ambayo Baba Mtakatifu Francisko amepewa kutoka nchini Slovakia. Hizi ni juhudi za Kardinali Konrad Krajewski, Mtunza Sadaka Mkuu wa Kipapa anayeshirikiana na wadau mbalimbali katika sekta ya afya, ili kuhakikisha kwamba, hata maskini katika umaskini wao, wanapata huduma dhidi ya maambukizi ya Virusi vya Corona, COVID-19. Huduma hii imewawezesha maskini wa Roma walau kupata makazi ya kudumu na hivyo kuondokana na adha ya kulala barabarani. Na kwa sasa wanaweza pia kupimwa Virusi vya Corona, COVID-19 ili kuhakikisha usalama wa maisha yao. Maskini wa mji wa Roma wanatambua na kukiri upendo wa Baba Mtakatifu kwa ajili yao!

Papa: Shukrani

 

25 December 2020, 15:10