Tafuta

2015.11.10 Papa Francisko wakati wa chakula cha mchana na maskini. 2015.11.10 Papa Francisko wakati wa chakula cha mchana na maskini. 

Siku ya maskini Duniani ilianza tangu 2017.Lengo ni kuonesha ukarimu kwa walio wa mwisho!

Katika fursa ya hitimisho la Jubilei ya huruma Papa Francisko alianzisha Siku ya Maskini duniani na kuelekeza ifanyike kila Dominika ya XXXIII ya kipindi cha kawaida cha mwaka.Siku hii inaongozwa na kauli mbiu ya “Uwape maskini kwa ukarimu”.Misa Takatifu itaongozwa na Francisko katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro katika muktadha wa janga,tarehe 15 Novemba.

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican.

Papa Francisko aliandika Barua yake ya Kitume “Misericordia et misera” yenye  tarehe 20 Novemba 2016 wakati wa kuhitimisha Jubilei Maalum ya Huruma ambayo ilikuwa imefunguliwa mnamo tarehe 8 Desemba 2015 kwamba, “Wakati Milango ya Makanisa Makuu na madhabahu wakiifunga, nilihisi kuwa, na ishara zaidi ya dhati ya Mwaka Maalum, na ili kuiadhimisha katika Kanisa lote: “ Siku ya Maskini ulimwenguni”. Itakuwa siku ambayo itasaidia jumuiya na kila mtu aliyebatizwa kutafakari jinsi umaskini ulivyo kiini cha Injili na juu ya ukweli kwamba, hapatakuwapo na haki au amani kijamii ikiwa Lazaro ataendelee kulala mlangoni mwa nyumba zetu. Akiedelea na katika waraka wake wa kitume, ‘Misericordia et misera’, yaani, Huruma na amani alisisistizia umuhimu wa msamaha, kwamba kila  Injili  imejaa msamaha  kama alama ya upendo  na huruma  ya Mungu kwa mwanadamu.

Hata hivyo katika muktadha wa Ujumbe wake kwa Siku ya Maskini mwaka huu Papa Francisko anasema kukutana na mtu aliye katika hali ya maskini, daima inatuchangamotisha na kutupatia maswali, ni katika kipengele cha nne. Je ni jinsi gani ya kuchangia kuondoa au kurahisisha hali yake ya kubaguliwa na mateso yake? Tunawezaje kumsaidia katika umaskini wake wa kiroho?  Papa Francisko anafafanua kuwa Jumuiya ya Kikrsito inaalikwa kuhusika katika uzoefu huu wa ushirikishwaji kwa utambuzi kwamba siyo halali  kuweka mwakilishi mwingine. Ili kuwa msaada kwa maskini, na ni vema kuishi umaskini wa kiinjili ukiwa mstari wa mbele. Hatuwezi kuhisi mambo ni sawa, ikiwa mjumbe mmoja wa familia ya binadamu haonekani  na amekuwa kivuli. Kilio cha ukimya kwa maskini wengi kinapaswa kipate watu wa Mungu walio mstari wa mbele daima na kila mahali kupaza sauti kwa niaba yao, ili kuwalinda na kuwatetea, kuwashikamanisha nao dhidi ya  ubinafsi mwingi na ahadi zisizo timizwa na ili kuwakaribisha washiriki katika maisha ya jumuiya. Ni kweli kwamba Kanisa halina suluhisho kamili la kupendekeza, Papa anaongeza,  lakini pia linatoa kwa nguvu ya neema ya Kristo, ushuhuda wake na ishara za ushirikishwaji. Na zaidi Kanisa linahisi uwajibikaji wa kuwakilisha wale ambao hawana mahitaji ya kuishi. Wakristo wanalo jukumu la kukumbusha thamani kubwa ya maisha ya pamoja na hakuna anayesahulika miongoni mwa binadamu ambao wamekiukwa mahitaji yao msingi.

Siku ya IV ya Maskini duniani 2020, inaadhimishwa Dominika tarehe 15 Novemba, na kwa sababu ya janga la virusi vya corona, maadhimisho ya misa yatakuwa tofauti katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro, saa nne kamili. Washiriki watakuwa karibu mia mmoja tu wakiwakilisha hali halisi ya umaskini ulimwenguni. Kutokana na janga la virusi kuendelea, hata hivyo Papa Francisko katika fursa hii ameandaa mtandao wa mshikamano kwa ajili ya kuleta chakula, barakoo na misaada mbali mbali kwa maelfu ya familia karibu parokia 60 za Roma na nyumba za familia, na vyama vya hisani.

Katika fursa hiyo aidha gari moja linaloratibiwa na Sadaka ya Kitume kwa ajili ya kupeleka mahitaji kwa watu na siku hiyo itajikita kusaidia wahudumu kufanya vipimo vya covid-19. Uwape maskini kwa ukarimu mada ambayo inaoongoza mwaka huu kwa hakika inaangazia ulimwengu mzima ambao umekumbwa na janga la adui hasiye onekana na ambaye amesababisha na anaendelea kuleta uchungu na vifo, kukata tamaa, mahangaiko, kwa maana hiyo ni watu wengi ambao wanasubiri kupata msaada kwa njia ya mshikamano na ukarimu.

Kwa maneno ya Papa aliyosema tarehe 17 Novemba 2019, katika tukio kama hilo wakati wa mahubiri yake, alisema kuwa “ haraka inayojionesha ndani ya maisha yetu ya kila siku, ikitufanya tupoteze kile kilicho muhimu ambacho ni upendo. Kwa shauku ya kukimbia, kushinda kila kitu na mara moja, inawasumbua wale ambao wanabaki nyuma. Na kuwahukumu walio wadhaifu. : Ni wazee wangapi, ni watoto wangapi wasiozaliwa, walemavu, watu maskini wanaonekana kuwa hawana maana. Yote hiyo ni sababu ya kwenda haraka bila wasiwasi  na kuwa mbali, uchoyo wa wachache unaongeza umaskini wa wengi”. Na alishauri kwamba “Kubaki na maskini, kwa kuwahudumia maskini, tunajifunza wale wenye haki ya Yesu, tunatambua ni kitu gani kinabki na kile kinachoisha”.

14 November 2020, 15:12