Tafuta

2020.11.01 Sala ya Malaika wa Bwana 2020.11.01 Sala ya Malaika wa Bwana 

Papa Francisko:Sisi sote tunaitwa kuwa watakatifu kinyume na dunia hii!

Siku kuu ya watakatifu wote inatukumbusha kutafakari juu ya ushuhuda wao ambao ni kisima cha kuchota tumaini katika ufufuko na mtindo wa safari inayojikita katika Heri ambazo tunaweza kutembea kwa namna ya pekee na isiyoweza kurudiwa na upole ambao leo hii ulimwengu unahitaji sana.Ni katika tafakari ya Papa Francisko wakati wa sala ya Malaika katika sikukuu ya watakatifu wote.

Na Sr. Angela Rwezaula Vatican

Papa Francisko ameanza tafakari yake siku ya Jumapili tarehe Mosi Novemba 2020, kwa waamini na mahujajii waliofika katika uwanja wa Mtakatifu Petro Vatican kuungana naye kusali sala ya Malaika wa Bwana, akiongozwa Injili ya Siku na furaha ya siku kuu ambapo mama Kanisa kwa mara nyingine tena ametupatia fursa ya kuwakumbuka watakatifu na wenye heri mbinguni ambao wanatuelekeza njia ya kufuata. Papa Francisko akianza tafakari hiyo amesema "Katika Siku kuu hii ya watakatifu wote, Mama Kanisa anatualika kutafakari juu ya matumaini makubwa ambayo yanajikita juu ya ufufuko wa Kristo. Kwa maana Kristo amefufuka na hata sisi tutakuwa na Yeye. Watakatifu na wenye heri ni mashuhuda zaidi wenye madaraka ya matumaini ya kikristo kwa sababu waliishi kwa utimilifu wa maisha yao kati ya furaha na mateso, kwa kujikita katika  matendo ya heri  ambazo Yesu alihubiri na hata leo hii Liturujia inakumbusha tena (Mt 5,1-12a). Heri za kiinjili kiukweli  ni maisha ya utakatifu, na kwa maana hiyo nitajikita kuelezea heri mbili ya pili na ya tatu”.

Heri ya Pili inasema heri wanaoomboleza maana watafarijika 

Papa Francisko akiendelea na  kufafanua heri ya pili inasema “Heri wale wanaolia kwa machozi maana hao watafarijika. Haya ni maneno ambayo utafikiri yanakwenda kunyume kwa sababu kilio sio ishara ya furaha na kufuraia. Sababu ya kilio na mateso ni kifo, ugonjwa, matatizo ya kimaadili, dhambi na makosa. Kwa kusema kiurahisi ni maisha ya kila siku, madhaifu na ambayo yanakumbana na matatizo. Maisha ambayo wakati mwingine yamejeruhiwa na kujaribiwa kwa kutokuthamini na kutokuelewana. Yesu anatangazia heri kwa wale wanaolia katika ukweli huu na, kila kitu, hasa wale wanaomtumaini Bwana na kujiweka chini ya kivuli chake. Wao siyo wasiojali, wala hawafanyi mioyo yao kuwa migumu mbele ya maumivu, lakini kwa subira wanatarajia faraja ya Mungu. Na tayari wanapata faraja hii katika maisha haya.

Heri wapole watairithi nchi:Upole ni tabia ya Yesu

Papa Francisko akifafanua heri ya tatu ambayo Yesu anasema heri wapole maana hao watairithi nchi; anathibitisha kuwa upole ni tabia ya Yesu ambaye anasema “jifunzeni kutoka kwangu maana mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo” (Mt 11,29).  Wapole ni wale ambao wanajua kujithibiti wao wenyewe na kuwaachia nafasi wengine, wanawasikiliza na kuwaheshimu kwa namna ya mtindo wao wa kuishi, katika mahitaji yao na maombi yao. Hawana nia ya kuipindua au kuipuuza, hawataki kutawala na kutawala kila kitu, wala kulazimisha maoni yao na masilahi yao kwa madhara ya wengine. Watu hawa, ambao mawazo ya ulimwengu hawayathamini, badala yake ni wa thamani machoni pa Mungu, ambaye huwapa urithi nchi ya ahadi, ambayo ni uzima wa milele. Heri hii pia huanzia hapa chini na itatimizwa katika Kristo, Papa Francisko amesisitiza. Kwa kutoa mfano  amesema, “Lakini upole ... katika wakati huu wa maisha ya ulimwengu, pia ambamo kuna uchokozi mwingi pia katika maisha ya kila siku, jambo la kwanza ambalo linatoka kwetu ni uchokozi na ulinzi. Tunahitaji upole ili kuendelea mbele kwenye njia ya utakatifu. Kusikiliza, kuheshimu,na sio kushambulia bali kuwa na upole”.

Kuchagua usafi, upole na huruma, kutoka katika haki na amani

Papa Francisko akiendelea na tafakari hiyo amebanisha kuwa kuchagua usafi, upole na huruma ; kuchagua kujitoa kwa Bwana katika umaskini wa roho na shida; kujitoa katika  haki na amani, hii yote inamaanisha kwenda kinyume na mawazo ya sasa ya ulimwengu huu, utamaduni wa kumiliki, raha isiyo na maana, ya kiburi kuelekea walio dhaifu. Njia hii ya kiinjili imekuwa ikipitiwa na Watakatifu na wenyeheri. “Sherehe ya leo, ambayo inaadhimisha ya Watakatifu Wote, inatukumbusha juu ya wito wetu binafsi na wa ulimwengu ili kuwa na  utakatifu, na inatupatia mifano ya hakika ya safari hii, ambayo kila mmoja hutembea kwa njia ya uhakika na ya kipekee , kwa njia isiyoweza kurudiwa. Inatosha kufikiria zawadi mbali mbali na historia za kweli ambazo zipo kati ya watakatifu wa kike na kiume. Hazifanani, kwa maana kila mmoja anayo yake binafsi na imekuzwa katika  maisha yake katika utakatifu kwa mujibu wa karama yake na kwa maana hiyo kila mmoja anaweza kwenda katika njia hiyo ya upole amesisitiza Papa pia kuhimiza kwamba sisi sote tutakwenda katika utakatifu. Katika familia kubwa ya waamini, wafuasi wa Kristo wanaye Mama Bikira Maria. Sisi sote tunamheshimu kwa jina la Malkia wa watakatifu wote, lakini kwanza ni Mama wa wote, ambaye anafundisha kila mmoja kupokea na kufuata. Yeye atusaidie kukuza shauku ya utakatifu katika kutembea katika njia za Heri, amehitimisha Papa Francisko.

 

01 November 2020, 16:57