Tafuta

Papa Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, tarehe 8 Novemba 2020 Papa Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, tarehe 8 Novemba 2020 

Mwaliko wa Papa ni maisha ya upendo na siyo ubinafsi ili kujiandaa kukutana na Mungu

Papa Francisko katika tafakari yake kuhusu Injili ya Yesu inayoeleza wanawali kumi wenye busara amekumbusha kuwa matendo mema ya kila siku yaongozwe na upendo wa Kristo,na ambayo yanaruhusu kusubiri kwa utulivu siku kuu ya maisha zaidi ya kifo.Tusifikirie ya wakati uliopo bali kusubiri Bwana ni jambo la lazima na zuri ameshauri.

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican.

Papa Francisko katika tafakari yake ya Dominika tarehe 8 Novemba 2020  kwa mahujaji na waamini waliokusanyika katika Uwanja wa Mtakatifu Petro Vatican, ameongozwa na Injili ya siku (Mt 25,1-13), kwamba inatualika kufanya tafakari ndefu juu ya maisha ya milele ambayo imeanza wakati wa  fursa ya  kumbu kumbu ya Marehemu wote. Yesu anasimulia juu ya wanawali kumi walioalika katika siku kuu ya arusi, ishara ya Ufalme wa mbingu. Nyakati za Yesu, kulikuwa na utamaduni wa kufanya sherehe usiku. Kwa maana hiyo waalikwa walikuwa daima wafike na taa zao zikiwa zinawaka.  Wanawali wapumbavu walichukua taa bila kuwa na mafuta, na wenye busara wakawa na taa  na mafuta. Bwana arusi alichelewa kufika na wote wakasinzia.

Usiku wa manane sauti iliposikika kuwa Bwana arusi amefika, wapumbavu wakati huo ndiyo wakagundua hawana mafuta ya taa na kuwaomba wenye busara. Lakini wale waliwajibu hawawezi kuwapatia kwa maana yalikuwa hayatoshi kwa wote. Wakati wanawali wapumbavu wanakwenda kununua mafuta, basi bwana arusi akafika. Wanawali wenye busara wakaingia na yeye katika ukumbi wa arusi na milango ikafungwa. Waliokwenda kununua mafuta walifika wamechelewa na hawakuruhusiwa kuingia.  Kwa kusisitiza Papa Francisko amesema hii ni wazi kabisa kwamba Bwana Yesu anataka kutueleza jinsi ya kuwa  tayari kwa ajili ya kukutana naye. Si tu katika mkutano naye wa mwisho, lakini hata katika mikutano midogo na mikubwa ya kila siku kwa matazamio ya ule mkutano wa mwisho, mahali ambapo haitoshi taa ya imani, lakini pia hata mafuta ya upendo na matendo mema. Imani ya kweli inayotuunganisha na Yesu ni ile ambayo anasema Mtume Paulo kwamba “ inajikita katika matendo  kwa njia ya upendo (Gal,5,6), kwa maana  ya  kile kinachowakilishwa na wanawali wenye busara.

Kuwa na hekima na busara maana yake yake siyo kusubiri wakati wa mwisho kwa ajili ya kujibu neema ya Mungu, bali ni kufanya kwa uhai wote haraka. Kuanza sasa hivi, siyo kusubiri mbele zaidi. “Ongoka leo hii na badili maisha na wala siyo kesho. Ukisema kesho, na kesho hiyo haitafika kamwe”, Papa amesisitiza. Kwa kuongezea amesema “Ni leo hii. Ikiwa tunataka kuwa tayari kwa ajili ya mkutano wa mwisho na Bwana, lazima kuanza sasa kushirikishana na Yeye  na kutenda matendo mema ambayo yanaangaziwa na upendo”, Tunambua kuwa inawezakana kwa bahati mbaya kusahau hatima ya maisha yetu, yaani mkutano wa mwisho na Mungu na kupoteza maana ya subira na suluhisho la wakati uliopo. Wakati mtu anapoona suluhisho la  wakati uliopo, anatazama  ya sasa tu, na hupoteza hali ya matarajio, ambayo ni mazuri sana na ni muhimu sana, na kwa maana hiyo hutupa nje ubishani wa wakati huu. Mtazamo huo unapoteza maana ya subira,  unazuia mtazamo wowote zaidi na unafanya kila kitu kana kwamba hautaondoka kamwe kwenda katika maisha mengine”, Papa amefafanua. “Katika mtazamo huo ni kuanza  kujali tu kumiliki, au kujitokeza, na kujikamilisha ... Na zaidi na zaidi”. “Lakini ikiwa tunajiruhusu tuongozwe na kile kinachoonekana kwetu kuvutia zaidi, na kile tunachopenda, kwa kufuata masilahi yetu, maisha yetu yanakuwa tasa; hatukusanyi akiba yoyote ya mafuta kwa jili ya  taa yetu, na itazima kabla ya kukutana na Bwana”, Papa Francisko amebainisha.

Lazima tuishi leo hii, lakini leo inayoelekea kesho, kuelekea katika mkutano huo, na leo iliyobeba matumaini. Kwa upande mwingine, tukikesha na kufanya mema kwa kuendana na neema ya Mungu, tunaweza kungojea kwa utulivu kuwasili kwa bwana arusi. Bwana anaweza kuja hata wakati tumelala usingizi. Lakini hiyo haitatutia wasiwasi, kwa sababu tuna akiba ya mafuta yaliyokusanywa na kazi nzuri za kila siku, pamoja na matarajio ya Bwana, kwamba atakuja haraka iwezekanavyo na kwamba atakuja kunichukua pamoja naye”, amesisitiza. Kwa kuhitimisha Papa Francisko amesema kwa maombezi ya Maria Mtakatifu, atusaidie kuishi kama Yeye alivyofanya kuwa na imani hai na kuwa na taa angavu ambayo tunaweza kukatisha usiku zaidi ya kifo na kufikia siku kuu kubwa ya maisha.

08 November 2020, 15:17