Tafuta

Papa Francisko Waraka wa Kitume "Scripturae Sacrae Affectus": Waraka Wa Kitume Juu ya Maandiko Matakatifu, Miaka 1600 Tangu Alipofariki Dunia Mtakatifu Jerome, Padre na Mwalimu wa Kanisa. Papa Francisko Waraka wa Kitume "Scripturae Sacrae Affectus": Waraka Wa Kitume Juu ya Maandiko Matakatifu, Miaka 1600 Tangu Alipofariki Dunia Mtakatifu Jerome, Padre na Mwalimu wa Kanisa. 

Papa: Waraka Wa Kitume "Scripturae Sacrae affectus"

Mambo Msingi: Historia na Hekima ya Mtakatifu Jerome; Upendo kwa Maandiko Matakatifu, Masomo ya Maandiko Matakatifu yanayohitaji mwongozo makini ili kuweza kuyatafakari na hatimaye, kuyatafsiri na kuyamwilisha. Mchango wa Mtakatifu Jerome katika kutafsiri na kupanga Biblia ya Vulgata; Utamadunisho. Mahusiano ya Mtakatifu Jerome na Kiti Kitakatifu cha Mtakatifu Petro.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko tarehe 30 Septemba 2020 katika maadhimisho ya kumbukumbu ya Miaka 1600 tangu alipofariki dunia Mtakatifu Jerome, Padre na Mwalimu wa Kanisa amechapisha Waraka mpya wa Kitume unaojulikana kama: "Scripturae Sacrae Affectus" Yaani “Waraka wa Kitume Juu ya Upendo Kwa Maandiko Matakatifu, Miaka 1600 Tangu Alipofariki Dunia Mtakatifu Jerome”, Padre na Mwalimu wa Kanisa aliyeweka Maandiko Matakatifu kuwa kiini cha maisha yake, mwaliko kwa waamini kupyaisha ndani mwao upendo wa kusoma, kutafakari na kumwilisha Maandiko Matakatifu katika uhalisia wa maisha yao! Huu ni urithi, tunu na amana ambayo Mtakatifu Jerome ameliachia Kanisa. Katika Waraka huu wa "Scripturae Sacrae Affectus",  Baba Mtakatifu Francisko anachambua: Historia na mchango wa Mtakatifu Jerome katika Maandiko Matakatifu, Hekima ya Mtakatifu Jerome inayofumbatwa katika ushuhuda wake kwa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu; Upendo kwa Maandiko Matakatifu, Masomo ya Maandiko Matakatifu yanayohitaji mwongozo makini ili kuweza kuyatafakari na hatimaye, kuyatafsiri na kuyamwilisha katika uhalisia wa maisha ya mtu. Mchango wa Mtakatifu Jerome katika kutafsiri na kupanga Biblia ya Kilatini, Vulgata; Tafsiri yake kama sehemu ya utamadunisho. Mahusiano ya Mtakatifu Jerome na Kiti Kitakatifu cha Mtakatifu Petro. Mwaliko wa kupenda kile alichopenda Mtakatifu Jerome, yaani Maktaba ya Maandiko Matakatifu.

Historia na Mchango wa Mtakatifu Jerome, Padre na Mwalimu wa Kanisa (Jina kamili ni Eusebius Sophronius Hieronymus) aliyezaliwa kunako mwaka  345 huko Stridon na akapata malezi na majiundo makini ya Kikristo. Alibahatika kumpata Jaalimu aliyemfundisha Maandiko Matakatifu, kiasi cha kupenda kusoma na kulitafakari Neno la Mungu. Kwa agizo la Papa Damasi wa kwanza, kwa muda wa miaka 23 alifanya kazi ya kutafsiri na kupanga vitabu vya Biblia kwa lugha ya Kilatini, maarufu kama “Vulgata” iliyopitishwa na Mababa wa Mtaguso wa Trento (1545-1563) kwamba inafaa kufundishia imani. Alipenda na kuthamini sana maeneo Matakatifu pamoja na mahujaji; akaanzisha monasteri mbili kama kielelezo cha ukarimu na upendo kwa mahujaji waliotaka kutembelea katika Nchi Takatifu. Alipenda kusikiliza, kusoma na kuyatafakari Maandiko Matakatifu; alithamini sana maisha ya ufukara, utawala bora, unyenyekevu; ukweli na uwazi. Mtakatifu Jerome, aliwataka Mapadre kuhakikisha kwamba, mahubiri yao yanapambwa na rejea za Neno la Mungu kama kielelezo cha ufahamu wa Mafumbo ya Kanisa “mysterii” na Mafundisho ya Kanisa “Sacramentorum”. Mtakatifu Jerome alijitahidi sana kuyatasiri na kuyafafanua Maandiko Matakatifu kwa kushirikiana na Jumuiya yake, kielelezo makini cha dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa. Alisimama kidete kulinda na kutetea Mafundisho tanzu ya Kanisa dhidi ya wazushi wa nyakati zake.

Mtakatifu Jerome, alifariki dunia tarehe 30 Septemba 430 huko Bethlehemu katika Jumuiya aliyokuwa ameianzisha. Katika ujana wake alipenda na kuguswa sana na Maandiko Matakatifu katika Lugha ya Kilatini, kiasi cha kuacha chapa ya kudumu katika malezi na makuzi yake tangu ujanani. Masomo yake yalimwezesha kujisadaka bila ya kujiachia kwa ajili ya huduma kwa Maandiko Matakatifu, kiasi kwamba, akawa ni daeaja kati ya Kanisa la Mashariki na Magharibi. Alifahamiana sana na Magwiji wa Maandiko Matakatifu nyakati zake. Hawa ni akina Mtakatifu Ambrosi na Mtakatifu Augustino, Askofu na Mwalimu wa Kanisa. Mababa wa Kanisa kwa nyakati tofauti wamempatia heshima Mtakatifu Jerome kwa mfano Papa Benedikto XV tarehe 15 Septemba 1920, Miaka 1500 tangu alipofariki dunia Mtakatifu Jerome, alichapisha Waraka wa kitume unaojulikana kama “Spiritus Paraclitus” kwa kumwonesha Mtakatifu Jerome kuwa kweli ni “doctor maximus explanandis scripturis” yaani “Mwalimu mahiri aliyefafanua Maandiko Matakatifu”. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI, katika Katekesi zake, alijikita katika mafundisho ya Mtakatifu Jerome. Papa Francisko kwa upande wake anapenda kuadhimisha kumbukumbu ya Miaka 1600 tangu alipofariki dunia kwa kujikita zaidi katika ujumbe na mafundisho yake, kwa kuanza na upendo wake kwa Maandiko Matakatifu. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI katika Wosia wake wa Kitume “Verbum Domini” yaani “Neno la Mungu” wa tarehe 30 Septemba 2010 alikazia amana na urithi wa Mtakatifu Jerome katika Maandiko Matakatifu.

Hekima kama sehemu ya maisha ya Mtakatifu Jerome ilijikita zaidi katika upendo wa dhati kwa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Pili alijisadaka kusoma kwa juhudi na maarifa ili aweze kung’amua Mafumbo ya maisha ya Kikristo, katika Sala na Tafakari makini ya Neno la Mungu. Hii ni changamoto kwa wasomi na wanazuoni kutambua na kuthamini tunu msingi za maisha ya kiroho zinazofumbatwa kwa namna ya pekee katika upendo kwa Mungu, kuliko matamanio ya mambo ya kidunia. Alijipambanua katika mchakato wa huduma ya ukweli na kwa msaada wa Roho Mtakatifu akabahatika kupata ukomavu wa ndani. Mtakatifu Jerome alikuwa na “Mahaba” na upendo mkubwa kwa Maandiko Matakatifu yaliyomwezesha kumfahamu Kristo Yesu! Ndiyo maana Mtakatifu Jerome anasema “Kutojua Maandiko Matakatifu ni kutomfahamu Kristo”. Hii ina maana kwamba, Maandiko Matakatifu na Mapokeo Hai ya Kanisa ni muhimu sana katika mchakato wa kumfahamu Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Leo hii anasema Baba Mtakatifu Francisko kuna haja ya kugundua tena katekesi, sanaa na umahiri wa kuhubiri, kwa kuchota utajiri katika taalimungu na Maandiko Matakatifu kama chemchemi ya maisha ya kiroho, inayowawezesha waamini kuwa ni mashuhuda wa ukweli, wongofu wa ndani na ujasiri wa kumpendeza Mwenyezi Mungu

Mtakatifu Jerome na Somo la Maandiko Matakatifu: Mwenyezi Mungu amejifunua kwa njia ya Maandiko Matakatifu na Kanisa kwa njia ya Mapokeo hai na msaada wa Roho Mtakatifu linatoa tafsiri sahihi ya Maandiko Matakatifu, jambo linalohitaji utii wa kiimani. Huu ni mwaliko wa kusoma na kutafakari Maandiko Matakatifu ili kuweza kutambua makusudi ya Mungu, ili hatimaye, kuweza kumpenda Mungu kwa dhati. Si kila wakati mwamini anaweza kuyafahamu Maandiko Matakatifu, kumbe, kuna haja ya kuwa na Mtumishi mwaminifu, hodari na mahiri atakayewasaidia ndugu zake katika Kristo Yesu kufahamu amana na utajiri unaobubujika kutoka katika Maandiko Matakatifu. Hivyo basi, kuna haja ya kujibidiisha kusoma Maandiko Matakatifu ili kuyatafsiri vyema kama ilivyokuwa kwa Filipo na towashi mkushi. Rej. Mdo. 8: 30-35. Filipo alimsaidia towasi mkushi kufahamu mafumbo ya maisha ya Kristo Yesu, kwa kumfafanulia mambo msingi katika Maandiko Matakatifu. Hapa kuna haja ya kujifunza kwa kina na mapana muswada wa Maandiko Matakatifu, tafiti za mambo ya kale na tafsiri sahihi ya historia ili kuwa na ufahamu sahihi wa Maandiko Matakatifu ambayo Mwenyezi Mungu ndiye mwandishi wake na umekabidhiwa kwa uvuvio wa Roho Mtakatifu. Kumbe, Biblia ni roho ya taalimungu na msaada mkubwa kwa maisha ya Kikristo na kwamba, tafsiri sahihi ya Maandiko Matakatifu, inapaswa kuongozwa na ujuzi maalum unaotolewa na Taasisi za Sayansi ya Maandiko Matakatifu. Wanafunzi wa taalimungu wanapaswa kupewa ujuzi utakaowasaidia kuyafahamu Maandiko Matakatifu.

Baba Mtakatifu Francisko anasikitika kusema kwamba, wanafunzi wa taalimungu wanapewa ujuzi kidogo sana wa kuweza kuyafahamu na kuyatolea ufafanuzi Maandiko Matakatifu. Somo la Maandiko Matakatifu halina budi kupewa kipaumbele cha pekee kwa Majandokasisi na Makatekista, bila kuwasahau waamini walei kama matunda ya hekima, matumaini na maisha. Waamini wanapaswa kuwa na uelewa na ushiriki makini katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu. Kwanza kabisa ni ufahamu wa Liturujia ya Neno la Mungu ambayo kwa Mtakatifu Jerome ni “Mwili na Mafundisho ya Kristo Yesu”. Familia za Kikristo zijibidiishe kufundisha na kuwarithisha watoto wao amana na utajiri wa Maandiko Matakatifu. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko kwa njia ya barua binafsi “Motu Proprio” “Aperuit Illis” ameanzisha “Domenika ya Neno la Mungu” itakayokuwa inaadhimishwa kuanzia sasa kila mwaka, Jumapili ya III ya Kipindi cha Mwaka wa Kanisa. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, Jumapili hiyo itakuwa ni fursa kwa watu wa Mungu kujenga utamaduni wa kusoma, kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha yao. Utambulisho wa Wakristo unafumbatwa kwa namna ya pekee, katika mahusiano ya dhati kati ya: Kristo Mfufuka, Maandiko Matakatifu na Jumuiya ya waamini. Ndiyo maana Mtakatifu Jerome anasema “Kutojua Maandiko Matakatifu ni kutomfahamu Kristo”. Baba Mtakatifu anasema, wazo la kuanzisha “Domenika ya Neno la Mungu” lilimwijia mara baada ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya Huruma ya Mungu, ili kuendeleza majadiliano kati ya Mwenyezi Mungu na waja wake; mwaliko wa kuendelea kulipyaisha Kanisa kwa amana na utajiri unaobubujika kutoka katika Maandiko Matakatifu.

Tafsiri ya Biblia kwa lugha ya Kilatini, maarufu kama “Biblia Sacra Vulgata” ni matunda ya kazi ya mikono ya Mtakatifu Jerome, Padre na Mwalimu wa Kanisa aliyejitahidi kutumia vyema ufahamu wake wa lugha ya Kigiriki na Kiyunani na hatimaye, kuandika Biblia kwa lugha ya Kilatini, chemchemi ya utamaduni na sanaa ya Kikristo. Hii ni amana na utajiri mkubwa sana kutoka kwa Mtakatifu Jerome kwa ajili ya Kanisa. Biblia hii inaweza kutumika kwa ajili ya masomo, mahubiri na mjadala wa hadhara. Mtakatifu Paulo VI kwa kuzingatia ushauri wa Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican alipitia Biblia ya “Vulgata” na kunako mwaka 1979 Mtakatifu Yohane Paulo II akaridhia machapisho ya “Vulgata Mpya”. Baba Mtakatifu Francisko anasema, tafsiri ya “Biblia Sacra Vulgata” katika lugha ya Kilatin ni matunda ya utamadunisho kwa ajili ya kulitajirisha Kanisa kwa lugha mbalimbali na kwamba, bado kuna hitaji muhimu la kuhakikisha kwamba, Biblia inatafsiriwa katika tamaduni mbalimbali za watu katika ulimwengu mamboleo, ili kujenga na kudumisha utamaduni wa watu kukutana. Hadi sasa Biblia imekwisha kutafsiriwa katika lugha zaidi ya elfu tatu sehemu mbalimbali za dunia, kazi na juhudi kubwa iliyotekelezwa na wamisionari kwa nyakati mbalimbali, ili kuweza kuwafikia watu wa Mungu kwa njia ya Neno la Mungu. Hata hivyo bado kuna haja ya kuongeza juhudi katika kutafsiri  Maandiko Matakatifu.

Mtakatifu Jerome alikuwa na uhusiano wa pekee na Kiti Kitakatifu na alijisikia kuwa ni sehemu ya raia na Padre chini ya uongozi wa Papa Damas, Khalifa wa Mtakatifu Petro, msingi wa Kanisa la Kristo Yesu, kielelezo cha umoja wa Kanisa. Mtakatifu Jerome alipambana sana na wazushi wa nyakati zake, akajipambanua kuwa ni mtetezi wa imani, mpenda ukweli na amani inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu. Hii ni amani inayowakirimia waamini uwezo wa kukutana na Kristo Yesu, chemchemi ya amani duniani inayowaunganisha watu na wala si kusababisha vita na ghasia. Baba Mtakatifu anakaza kusema, ulimwengu mamboleo unahitaji dawa ya huruma ya Mungu, umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu, kwa kupendana kama ushuhuda wa kuwa ni wanafunzi wa Kristo Yesu. Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha Waraka mpya wa Kitume unaojulikana kama: "Scripturae Sacrae Affectus" Yaani “Waraka wa Kitume Juu ya Upendo Kwa Maandiko Matakatifu, Miaka 1600 Tangu Alipofariki Dunia Mtakatifu Jerome”, Padre na Mwalimu wa Kanisa kwa kuwaalika waamini na hasa zaidi vijana wa kizazi kipya kujichotea utajiri, amana na urithi mkubwa kutoka katika “Maktaba kuu” ya Maandiko Matakatifu, ili kuboresha imani na maisha ya kiroho.

Waamini watoe kipaumbele cha pekee katika kusoma, kutafakari na hatimaye, kuyamwilisha Maandiko Matakatifu katika maisha yao. Vijana waoneshe kiu ya kweli za maisha ya kiroho kwa kuondokana na ujinga wa kutoyafahamu Maandiko Matakatifu. Waamini wajifunze utalaam na sanaa ya kutafsiri na kuyatamadunisha Maandiko Matakatifu katika uhalisia wa maisha yao. Vijana wajifunze amana na utajiri wa historia na tamaduni zao kwa kumwangalia Mtakatifu Jerome ambaye alijipambanua na kuwa kama “Maktaba ya Kristo Yesu”, Maktaba endelevu hata baada ya miaka 1600 bado inaendelea kuwafundisha waamini upendo wa Mungu unaowawezesha kukutana na Mwenyezi Mungu. Watu waguswe na tasaufi ya maisha yake, wajenge ndani mwao kiu ya kutaka kumfahamu Mwenyezi Mungu aliyejifunua kwa njia ya Maandiko Matakatifu. Bikira Maria ni mfano bora wa kusoma, kuyatafakari na hatimaye kuyahifadhi katika sakafu ya moyo wake. Rej. Lk. 2:19.51. Bikira Maria aliyafahamu fika Maandiko Matakatifu, mwaliko kwa waamini kujiaminisha chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, ili aweze kuwafunda namna bora zaidi ya kusoma, kutafakari na kusali mbele ya Mwenyezi Mungu anaendelea kujionesha katika maisha ya waja wake.

Waraka Biblia
01 October 2020, 16:22