Tafuta

Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko: "Fratelli tutti: Yaani "Wote Ni Ndugu": Kuhusu Udugu na Ufariki wa wa Kijamii: Sura ya Tano: Siasa Safi! Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko: "Fratelli tutti: Yaani "Wote Ni Ndugu": Kuhusu Udugu na Ufariki wa wa Kijamii: Sura ya Tano: Siasa Safi! 

Waraka wa Kitume Wa Papa Francisko: "Fratelli tutti: Siasa Safi!

Papa Francisko: "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” kwenye Sura ya Tano: Siasa Safi. Pili ni mchango wa Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican kuhusu: Ufalme wa Mungu na utawala wa watu.Tatu ni Ujumbe wa Papa Francisko wa Siku ya Kuombea Amani Duniani mwaka 2019, uliongozwa na kauli mbiu “Siasa safi ni huduma ya amani”.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Radio Vatican inapenda kukushirikisha kwa muhtasari yale yaliyomo kwenye Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko: "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” kwenye Sura ya Tano: Siasa Safi. Pili ni mchango wa Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican kuhusu: Ufalme wa Mungu na utawala wa watu kama unavyopembuliwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika ujumbe wake wa Kwaresima kwa Mwaka 2020. Tatu ni Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko wa Siku ya Kuombea Amani Duniani mwaka 2019, uliongozwa na kauli mbiu “Siasa safi ni huduma ya amani”. Baba Mtakatifu anasema, upendo na fadhila za kiutu ziwe ni kwa ajili ya siasa safi inayohudumia haki msingi na amani, kila mtu akijitahidi kujikita katika mafao ya wengi, kama sehemu ya ujenzi wa mji wa Mungu hapa duniani, ili kuendeleza historia ya maisha ya familia ya binadamu. Haki na usawa; tabia ya kuheshimiana na kuthaminiana kama binadamu; ukweli, uwazi na uaminifu; ni tunu msingi zinazoboresha siasa safi. Mwanasiasa bora ni yule anayetambua dhamana na wajibu wake kwa jamii; anayeaminika na kuthaminiwa na jamii; ni kiongozi anayejitaabisha kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; mwaminifu katika ahadi zake kwa wananchi waliomchagua, daima akijitahidi kujenga na kudumisha umoja na mshikamano, tayari kuchochea mageuzi katika maisha ya watu; kwa kuwasikiliza na kutenda kwa ujasiri!

Siasa safi inayojikita katika ujenzi wa amani inatambua karama za watu na inaendeleza majadiliano na watu ili waweze kuaminiana na kuthaminiana. Katika siasa kuna watu wanatafuta umaarufu si kwa ajili ya huduma kwa watu bali wanataka kuwanyonya na kujineemesha binafsi. Siasa safi inatengeneza fursa za ajira, inawalinda wafanyakazi na kupambana na umaskini wa hali na kipato. Inakuza na kudumisha umoja na mshikamano unaoratibiwa na kanuni ya auni. Siasa safi inajielekeza zaidi katika kujibu kero zinazopelekea uvunjwaji wa haki msingi za binadamu na kuwatumbukiza watu katika mifumo ya utumwa mamboleo, ubidhaishaji maumbile ya binadamu; biashara haramu ya silaha na dawa za kulevya pamoja na matumizi yake haramu; ukahaba wa utalii, kazi za suluba, vitendo vya kigaidi yote haya ni uhalifu dhidi ya utu na heshima ya binadamu pamoja na baa la njaa linalowakosesha mamilioni ya watu haki ya chakula na lishe bora. Watu wa Mungu wanahitaji siasa safi inayotoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu na wala si katika mfumo wa fedha na soko huria linalokita mizizi yake katika faida kubwa.

Ni katika muktadha huu, vyama vingi vya kijamii vinaendelea kuibuka kama “wimbi la nguvu za kimaadili” zinazopaswa kutumiwa na jamii kwa kuratibiwa vyema, ili kwenda sanjari na sera ya siasa kwa ajili pamoja na watu maskini. Baba Mtakatifu anagusia pia umuhimu wa kufanya mageuzi makubwa katika Umoja wa Mataifa, ili kweli uweze kuwa ni “Familia ya Mataifa”. Umoja wa Mataifa usimame kidete kupigania ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; upambane na umaskini, kwa kulinda haki msingi za binadamu. Umoja wa Mataifa uwe ni jukwaa la majadiliano katika ukweli na uwazi; upatanisho na mwamuzi. Umoja wa Mataifa ujikite katika utekelezaji wa sera ya nguvu ya sheria na wala si sheria ya nguvu!

MAFUNDISHO YA MTAGUSO MKUU WA PILI WA VATICAN. Kadiri ya mafundisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican moja kati ya maeneo yaliyotiliwa mkazo ni uhusiano kati ya Ufalme wa Mungu na utawala wa watu, hususani katika Hati ya Kichungaji juu ya Kanisa na Ulimwengu (Gaudium et Spes-GS). Utambuzi hai wa hadhi ya binadamu katika mahali pengi duniani, unaamsha juhudi ya kuunda utaratibu wa kisiasa na kisheria ambapo haki za binadamu katika maisha ya hadhara zinalindwa vema zaidi. Nazo ndizo haki za kujumuika na kuunda umoja kwa uhuru, haki ya kila mmoja kutoa maoni yake na kukiri imani yake akiwa peke yake au hadharani. Maana, ulinzi wa haki za binadamu ni sharti la lazima ili raia, kila mmoja peke yake au kama wanachama, waweze kushiriki kimatendo maisha ya umma na uongozi wa mambo yanayowahusu. (Rej. GS. 73). Pamoja na maendeleo ya kiutamaduni, kiuchumi na kijamii, hamu ya walio wengi ya kuchukua wajibu mkubwa zaidi katika kuratibu maisha ya jumuiya ya kisiasa inazidi kupata nguvu. Katika dhamiri ya watu wengi bidii ya kuhifadhi haki za makundi ya wachache katika nchi zao inastawi, lakini bila ya makundi hayo ya wachache kusahau wajibu zao mbele ya jumuiya ya kisiasa. Aidha, inazidi kukua heshima mbele ya watu wenye maoni au dini tofauti.

Na wakati huohuo ushirikiano mpana zaidi unaundwa; nao unalenga kwa raia wote (Rej. GS. 73). Ili kuunda maisha ya kisiasa yaliyo kweli ya kibinadamu, hakuna lililo bora zaidi kuliko kustawisha ndani ya watu hisia za haki, upendo na huduma kwa manufaa ya wote. Pia ni kuuimarisha msimamo wa msingi mintarafu maumbile halisi ya jumuiya ya kisiasa; tena kuhusu lengo, matumizi halali na mipaka ya wajibu wa serikali (Rej. GS. 73). Utawala wa kisiasa, uwe unatekelezwa na jumuiya yenyewe au na vyombo vinavyowakilisha dola, ni lazima daima ufanyike ndani ya mipaka ya sheria ya kimaadili. Lengo lake ni kuyafikia manufaa ya wote, tena manufaa yenye maendeleo yake, kadiri ya kanuni za utaratibu wa kisheria uliokwisha kuwekwa, au wa kuwekwa. Na hapo ndipo raia wanapolazimishwa kutii kwa sababu ya dhamiri zao (Rej. GS. 74). Aidha katika Hati ya Kanisa katika Ulimwengu Mamboleo (GS), Mtaguso unasisitiza kuwa utekelezaji wa madaraka ya kisiasa daima ukusudie katika kumuunda mtu mwadilifu, mtulivu, na mkarimu kwa wote, kwa manufaa ya familia nzima ya wanadamu.

Ili kukuza maisha ya hadhara ya kisiasa, sharti ipatikane miundo ya kisiasa na kisheria inayowawezesha zaidi na zaidi raia wote – bila ubaguzi wowote – kushiriki kwa uhuru na kwa matendo katika kutengeneza misingi ya kisheria ya jumuiya ya kisiasa. Lengo lake ni kuongoza mambo ya dola, katika kuainisha uwanja wa kazi na mipaka yake kwa taasisi mbalimbali, na hatimaye katika kuwachagua viongozi. Kwa sababu hiyo, raia wote wakumbuke haki yao, ambayo pia ni wajibu, ya kutumia kura yao huru kwa minajili ya kuhamasisha manufaa ya wote. Kanisa linasifu na kuthamini wale ambao, kwa ajili ya kuwatumikia wanadamu, wanajitoa kwa manufaa ya dola na kubeba uzito wa wajibu husika (Rej. GS. 75). Katika nyakati zetu hizi, ugumu wa masuala yanayojitokeza unazilazimisha serikali kujihusisha zaidi katika fani za kijamii, kiuchumi na kiutamaduni ili kuleta mazingira yanayofaa zaidi, kusudi raia na makundi waweze kuyafuatilia kwa bidii na kwa uhuru manufaa kamili ya binadamu. Uhusiano mzuri miongoni mwa watu na uwezo wa kujiratibisha na kujiendeleza kwa mtu binafsi, unaweza kufikiriwa kwa namna tofauti katika nchi mbalimbali za ulimwengu na kwa mujibu wa maendeleo ya mataifa. Raia hawana budi kustawisha upendo kwa taifa lao kwa ari na unyofu, lakini si kwa mtazamo finyu, yaani hivi kwamba wayazingatie daima mema ya familia nzima ya wanadamu inayounganika kwa vifungo mbalimbali kati ya makabila, mataifa na nchi (Rej. GS. 75).

UJUMBE WA PAPA FRANCISKO (01.01.2019) Baba Mtakatifu Francisko, katika Ujumbe wa Siku ya Kuombea Amani Duniani mwaka 2019, wenye kauli mbiu ya “Siasa safi ni huduma ya amani”, aliangalia mambo kadhaa, kwa kuzingatia kuwa Injili ya amani ni sehemu ya utume wa Kanisa. Mambo hayo ni a) Changamoto za siasa safi; b) Upendo na fadhila za kiutu kwa ajili ya siasa inayohudumia haki msingi na amani; c) umuhimu wa siasa safi inayowashirikisha vijana na kujengeana imani; na d) kukataa kishawishi cha vita na mbinu mkakati wa vitisho, kwa kuwekeza katika mradi mkubwa wa amani. Changamoto za siasa safi: Baba Mtakatifu anafafanua kwa kusema, amani ni sawa na matumaini yanayosongwa na changamoto pamoja na magumu yanayowaandama walimwengu, hasa kutokana na uchu wa mali, madaraka na utajiri wa haraka haraka, na matokeo yake ni matumizi mabaya ya madaraka na uvunjwaji wa haki msingi za binadamu. Siasa safi ni nyenzo inayosaidia ujenzi wa huduma kwa binadamu, lakini siasa ikitumiwa vibaya inaweza kuwa chombo cha dhuluma, mipasuko na hatimaye kusababisha madhara makubwa kwa jamii. Kuhusiana na hilo naye Papa Paulo VI alikuwa na haya, “Siasa ikichukuliwa katika umuhimu wake kuanzia ngazi ya kijiji, kimkoa, kitaifa na kidunia- ni kukubali wajibu wa kila mtu kukiri ukweli na thamani ya uhuru ambao unatolewa kwake na jamii kuufanyia kazi kwa manufaa mazuri ya mji, taifa na binadamu wote,” (Rej. Octogesima Adveniens, 14 Mei 1971, 46).

Upendo na fadhila za kiutu ni kwa ajili ya siasa safi inayohudumia haki msingi na amani: Baba Mtakatifu Francisko akimnukuu Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI anasema, “Kila mtu ajitahidi kujikita katika mafao ya wengi, kama sehemu ya ujenzi wa mji wa Mungu hapa duniani, ili kuendeleza historia ya maisha ya familia ya binadamu” (Rej. Benedict XVI, Caritas in Veritate 29 June 2009). Haki na usawa; tabia ya kuheshimiana na kuthaminiana kama binadamu; ukweli, uwazi na uaminifu ni tunu msingi zinazoboresha siasa safi. Mwanasiasa bora ni yule anayetambua dhamana na wajibu wake kwa jamii; anayeaminika na kuthaminiwa na jamii; ni kiongozi anayejitaabisha kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Tena, anapaswa kuwa mwaminifu katika ahadi zake kwa wananchi waliomchagua, daima akijitahidi kujenga na kudumisha umoja na mshikamano, awe tayari kuchochea mageuzi katika maisha ya watu; kwa kuwasikiliza na kutenda kwa ujasiri.

Siasa safi inajengeka katika unyenyekevu, kielelezo makini cha huduma katika ngazi mbali mbali za maisha ya binadamu: Lengo ni kukuza na kudumisha dhamana, utu, heshima na tunu msingi za maisha zinazoiwezesha jamii kutekeleza mafao ya wengi. Kumbe, utekelezaji makini wa siasa safi ni changamoto endelevu kwa viongozi wanaopewa dhamana ya kuongoza, kwani wanapaswa kuwalinda raia wao; kwa kushirikiana kikamilifu ili kuboresha maisha ya wananchi wao katika misingi ya haki, uhuru, utu na heshima ya binadamu na kwa njia hii, siasa safi inakuwa chombo cha upendo. Umuhimu wa siasa safi inayowashirikisha vijana na kujengeana imani: Baba Mtakatifu anaendelea kuhimiza umuhimu wa kudumisha siasa safi inayowashirikisha vijana na kujengeana imani, kiasi kwamba, hata vijana wa kizazi kipya wanajisikia kuwa ni sehemu ya mchakato wa ujenzi wa jamii yao na kwamba, wanaweza kushirikisha karama na mapaji waliokirimiwa na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya mafao ya wengi.Hawa ni vijana ambao dhamana ya amani inapenyeza katika akili na nyoyo zao, tayari kujitosa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Siasa safi inayojikita katika ujenzi wa Amani: Siasa ya namna hii inatambua karama za watu na inaendeleza majadiliano, watu kuaminiana, kuthaminiana na kujenga upendo. Haya yatafuta dalili za ubinafsi unaofumbatwa katika dhana ya utaifa usiokuwa na tija. Jamii inawahitaji wanasiasa ambao watakuwa wajenzi wa amani, watakaokuwa watangazaji, mashuhuda na vyombo vya wema, huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake ambaye anawatakia watoto wake furaha.

HITIMISHO: Hivyo, basi tunaalikwa tuwaombee viongozi wetu waweze kutawala kadiri ya mapenzi ya Mungu (Rej. Dn. 4:17). Daima watawala watambue kuwa uongozi ni utumishi, dhamana, uwakili, na kuwa watatakiwa kutoa hesabu ya utumishi wao kwa Mungu na kwa jamii. Hata hivyo, tunaamini kuwa watawala ni wajumbe wa Mungu ambao licha ya ubinadamu wao, neema ya Mungu huwasaidia katika kutimiza majukumu yao (Rej. Mith. 8:15-16). Ndiyo maana ni muhimu kuwaombea watawala. Mtakatifu Paulo alipendekeza hata alipokuwa akiteswa, kuwa “sharti pawepo dua, sala, maombi na sala za shukrani kwa Mungu kwa ajili ya watu wote, kwa ajili ya wafalme na watu wote wenye mamlaka, ili tupate kuishi maisha ya utulivu na amani pamoja na uchaji wa Mungu na mwenendo mwema” (1Tim 2:1 – 2). Nipende kuhitimisha makala hii kwa kuwakumbusha watanzania kwamba, tarehe 14 Oktoba kwa watanzania ni Siku ya Mwalimu Nyerere. Alipokuwa anakaribia kuaga dunia mwezi Oktoba 1999 akiwa kwenye Hospitali ya St. Thomas nchini Uingereza alisema, anaondoka, akiwa amewaachia Taifa moja lenye umoja na amani. Wosia wake kwa watanzania ni kuipenda nchi yao kama wanavyowapenda mama zao. Wajue hawana nchi nyingine zaidi ya Tanzania.

Siasa Safi
13 October 2020, 14:15