Tafuta

SECAM Inampongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kuchapisha Waraka wa Kitume "Fratelli tutti" kwa kukazia umuhimu wa udugu wa kibinadamu na mshikamano wa upendo kati ya watu wa Mungu. SECAM Inampongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kuchapisha Waraka wa Kitume "Fratelli tutti" kwa kukazia umuhimu wa udugu wa kibinadamu na mshikamano wa upendo kati ya watu wa Mungu. 

SECAM: Waraka wa Kitume Wa Papa Francisko: "Fratelli tutti"

SECAM, inampongeza Papa Francisko kwa kuchapisha Waraka wake wa Kitume: "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” unaopania kupyaisha udugu wa kibinadamu, urafiki wa kijamii, amani na utulivu kati ya watu wa Mungu. Waraka unakazia umuhimu wa: Ujenzi wa udugu wa kibinadamu, mshikamano wa kweli katika huduma kwa maskini!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” uliozinduliwa rasmi tarehe 4 Oktoba 2020 unakamilishana na Waraka wa Kitume wa “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”. Baba Mtakatifu anapenda kuunganisha athari za uchafuzi wa mazingira, magonjwa ya kijamii; vita na kinzani; wimbi kubwa la wahamiaji na wakimbizi pamoja na baa la umaskini linalopekenya utu, heshima na haki msingi za binadamu. Lengo ni kuhakikisha kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inaunda mfumo wa uchumi na masuala ya kijamii yanayokita misingi yake katika haki, heshima na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, daima: utu, heshima na haki msingi za binadamu zikipewa kipaumbele cha kwanza. Baba Mtakatifu anakaza kusema, alama mbali mbali zinaonesha wazi kwamba, kuna uhusiano na mwingiliano mkubwa kati ya udugu wa kibinadamu na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote kama njia inayowaelekeza watu wa Mungu katika mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu, haki na amani; tunu msingi ambazo zimebainishwa na Mtakatifu Yohane XXIII, Mtakatifu Paulo VI na Mtakatifu Yohane Paulo II katika Mamlaka Matakatifu ya Ufundishaji katika Kanisa, yaani “Magisterium”.

Huu ni Waraka wa Kitume unaopembua: magonjwa jamii na changamoto zake katika ulimwengu mamboleo. Msamaria mwema anawekwa mbele ya walimwengu kama ni mfano bora wa kuigwa katika kutangaza na kushuhudia Injili ya upendo kwa maskini. Baba Mtakatifu anakazia maisha ya kiroho, mshikamano wa kidugu, utu, heshima na haki msingi za binadamu. Changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani, utawala bora, ushirikiano na mshikamano katika kukabiliana na changamoto mamboleo ni mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele cha pekee.  Baba Mtakatifu anagusia kuhusu siasa safi kwa ajili ya huduma kwa jamii, maendeleo, ustawi na mafao ya wengi; utu, haki msingi za binadamu na umuhimu wa kufanya mageuzi makubwa kwenye Umoja wa Mataifa ili kweli uweze kuwa ni “familia ya Mataifa”. Watu wa Mungu hawana budi kujikita zaidi katika mchakato wa majadiliano na urafiki ili kujenga sanaa ya watu kukutana.

Baba Mtakatifu anapembua kuhusu makutano yaliyopyaishwa ili kujenga misingi ya haki na amani; msamaha kwa kuondokana na “dhana ya vita ya haki na halali” ambayo kwa sasa imepitwa na wakati kama ilivyo pia kwa adhabu ya kifo kwani inakwenda kinyume cha haki msingi za binadamu, utakatifu na zawadi ya maisha kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu anapinga kwa nguvu zote utamaduni wa kifo! Dini na udugu ni chanda na pete; hapa mkazo ni umuhimu wa dini kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu na kwamba, Kanisa litaendelea kujizatiti katika mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu kwa kuzingatia kanuni msingi za Kiinjili. Ni katika muktadha huu, Kardinali Philippe Nakellentuba Ouédraogo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Ouagadougou, Burkina Faso, Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM, anamshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kuchapisha Waraka wake wa Kitume: "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” unaopania kupyaisha udugu wa kibinadamu, urafiki wa kijamii, amani na utulivu kati ya watu wa Mungu.

Ni Waraka unaokazia pamoja na mambo mengine umuhimu wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu, kwa kutambua kwamba, wote ni watoto wa Mwenyezi Mungu, wanaounda familia moja ya binadamu inayopaswa kuwajibikiana na kusaidiana, kwa sababu hakuna mtu ambaye anaweza kujiokoa peke yake! Watu wanategemeana na kukamilishana kama ambavyo imejidhihirisha katika janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Mshikamano wa kidugu na urafiki wa kijamii, ni nguzo msingi katika mchakato wa kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote. Mtakatifu Yohane Paulo II anasema, Kanisa ni Sakramenti ya Wokovu inayokita mizizi yake katika umoja, upendo na mshikamano wa kidugu kati ya Mwenyezi Mungu na binadamu. Kanisa linapaswa kuwa ni makazi na shule ya umoja kwa kusikiliza na kujibu kilio na matamanio halali ya watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia.

SECAM inapenda kumuunga mkono Baba Mtakatifu Francisko katika mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu na mshikamano; majadiliano katika ukweli na uwazi; kwa kukupokeana, kuheshimiana pamoja na kuthaminiana kama ndugu wamoja licha ya tofauti zao msingi zinazobubujika kutoka katika tamaduni, dini na imani. Ni wakati muafaka wa kuvunjilia mbali kuta za utengano kutokana na misimamo mikali ya kidini na kiimani; nyanyaso, dhuluma pamoja na vitendo vya kigaidi vinavyo dhalilisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Watu wa Mungu wanapaswa kushikamana ili kupambana fika na changamoto ambazo zinasababishwa na janga la Virusi vya Corona, COVID-19 pamoja na kusimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha uhuru wa kidini. SECAM inasema, kuna mamilioni ya watu wanaoteseka na kufa kwa baa la njaa, umaskini na magonjwa sehemu mbali mbali za dunia. Umefika wakati wa kuiga na kufuata mfano wa Msamaria mwema ili kumwilisha huduma ya upendo na mshikamano katika uhalisia wa maisha.

SECAM kwa upande wake, inapenda kukazia zaidi kuhusu: Familia kama Kanisa dogo la nyumba, shule ya upendo, huruma, haki na ukarimu. Ni mahali patakatifu ambapo tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni zinarithishwa, tayari kuunda jamii inayowajibikiana na kutegemezana. Ni wakati wa kuondokana na ukabila, udini na siasa zinazowatenga na kuwagawanya watu na badala yake, watu wa Mungu Barani Afrika wajikite katika mchakato wa ujenzi wa misingi ya haki, amani na upatanisho. Udugu wa kibinadamu na urafiki wa kijamii ni tunu msingi zinazopaswa kumwilishwa katika siasa safi na utawala bora; ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; daima utu, heshima na haki msingi za binadamu vikipewa kipaumbele cha kwanza. Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM linawahamasisha watu wa Mungu kuhakikisha kwamba, wanajitahidi kumwilisha katika uhalisia wa maisha yao Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” katika tunu msingi za maisha ya kifamilia, kitamaduni, kidini, kisiasa, kijamii na katika masuala ya biashara.

SECAM
08 October 2020, 14:54