Tafuta

Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko: "Frateri tutti: Yaani "Wote Ni Ndugu": Kuhusu Udugu na Ufariki wa Kijamii unakazia utu, heshima na haki msingi za binadamu! Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko: "Frateri tutti: Yaani "Wote Ni Ndugu": Kuhusu Udugu na Ufariki wa Kijamii unakazia utu, heshima na haki msingi za binadamu!  Tahariri

Waraka wa Kitume Wa Papa Francisko: "Fratelli tutti": Utu wa mtu!

Soko huria linaonekana kuishinda siasa safi na utamaduni wa kutupa unaonekana kushamiri. Kilio cha Mama Dunia na maskini duniani vinaendelea kugonga mwamba! Kuna watu wanaokufa kwa njaa na bado hawajasikilizwa. lakini kuna mtu mwenye ujasiri anayependa kuwaonesha walimwengu njia madhubuti ya ujenzi wa dunia mpya inayojikita katika utu na heshima ya binadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” uliozinduliwa rasmi tarehe 4 Oktoba 2020, unagusia magonjwa jamii na changamoto zake katika ulimwengu mamboleo. Msamaria mwema anawekwa mbele ya walimwengu kama ni mfano bora wa kuigwa katika kutangaza na kushuhudia Injili ya upendo kwa maskini. Baba Mtakatifu inakazia maisha ya kiroho, mshikamano wa kidugu, utu, heshima na haki msingi za binadamu. Changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani, utawala bora, ushirikiano na mshikamano katika kukabiliana na changamoto mamboleo ni mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele cha pekee.  Baba Mtakatifu anagusia kuhusu siasa safi kwa ajili ya huduma kwa jamii, maendeleo, ustawi na mafao ya wengi; utu, haki msingi za binadamu na umuhimu wa kufanya mageuzi makubwa kwenye Umoja wa Mataifa ili kweli uweze kuwa ni “familia ya Mataifa”.

Watu wa Mungu hawana budi kujikita zaidi katika mchakato wa majadiliano na urafiki ili kujenga sanaa ya watu kukutana. Baba Mtakatifu anapembua kuhusu makutano yaliyopyaishwa ili kujenga misingi ya haki na amani; msamaha kwa kuondokana na “dhana ya vita ya haki na halali” ambayo kwa sasa imepitwa na wakati kama ilivyo pia kwa adhabu ya kifo kwani inakwenda kinyume cha haki msingi za binadamu, utakatifu na zawadi ya maisha kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu anapinga kwa nguvu zote utamaduni wa kifo! Dini na udugu ni chanda na pete; hapa mkazo ni umuhimu wa dini kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu na kwamba, Kanisa litaendelea kujizatiti katika mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu kwa kuzingatia kanuni msingi za Kiinjili.

Dr. Andrea Tornielli, Mhariri Mkuu wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano katika tahariri yake kuhusu Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” anasema, ulimwengu umegubikwa na giza nene la ubinafsi kiasi kwamba, bado kuna watu wanathubutu kutembea katika giza totoro, lakini wapo pia wale wanaothubutu kuota ndoto ya matumaini kwa kujielekeza zaidi katika ujenzi wa udugu na urafiki wa kijamii. Leo hii dunia inashuhudia Vita ya Tatu ya Dunia ikiendelea kurindima vipande vipande sehemu mbali mbali za dunia. Soko huria linalokita mizizi yake katika faida kubwa linaonekana kuishinda siasa safi na utamaduni wa kutupa unaonekana kuendelea kushamiri. Kilio cha Mama Dunia kuhusu uharibifu wa mazingira sanjari na kilio cha maskini duniani vinaendelea kugonga mwamba! Kilio cha maskini wanaopoteza maisha kwa baa la njaa, bado hakijasikilizwa, lakini kuna mtu mwenye ujasiri anayependa kuwaonesha walimwengu njia madhubuti ya ujenzi wa dunia mpya inayojikita katika utu na heshima ya binadamu.

Takribani miaka mitano iliyopita yaani tarehe 24 Mei 2015, Baba Mtakatifu Francisko alichapisha Waraka wa Kitume wa “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”. Huu ni Waraka unaozungumzia kwa muhtasari mambo yanayotokea katika mazingira; Injili ya Uumbaji; Vyanzo vya mgogoro wa ekolojia vinavyohusiana na watu; Ekolojia msingi; Njia za kupanga na kutenda na mwishoni ni elimu ya ekolojia na maisha ya kiroho. Baba Mtakatifu anapenda kuunganisha athari za uchafuzi wa mazingira, magonjwa ya kijamii; vita na kinzani; wimbi kubwa la wahamiaji na wakimbizi pamoja na baa la umaskini linalopekenya utu, heshima na haki msingi za binadamu. Lengo ni kuhakikisha kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inaunda mfumo wa uchumi na masuala ya kijamii yanayokita misingi yake katika haki, heshima na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, daima: utu, heshima na haki msingi za binadamu zikipewa kipaumbele cha kwanza.

Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” unatoa dira na mwongozo wa kuweza kufikia malengo haya kwa watu kutambuana kwamba, wao ni ndugu wamoja na wanahamasishwa kutegemezana na kusaidiana, kwani wote wako ndani ya mashua moja! Hili limejidhihirisha wazi zaidi katika janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Vurusi vya Corona, COVID-19. Huu ni mwaliko kwa watu wa Mungu kutojikatia tamaa na hatimaye, kutumbukia katika kishawishi cha “Mwanadamu kugeuka kuwa Mbwa mwitu” “homo homini lupus” kwa kujenga kuta za utengano na badala yake, wamtazame Msamaria mwema, ili kumwilisha Injili ya upendo inayomwondoa mwanadamu kutoka katika miundombinu iliyopitwa na wakati. Huu ni mwaliko kwa binadamu kutambuana kuwa wao ni ndugu wamoja na kwa namna ya pekee kwa waamini, ni kujitahidi kumwona Kristo Yesu kati ya watu wote walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Waamini wajitahidi kumtambua Kristo Yesu anateseka kati pamoja na maskini; wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; waliosahaulika na kutelekezwa; Kristo Mfufuka awasaidie wote hawa kusimama tena dede! Ujumbe wa udugu wa kibinadamu unawagusa na kuwaambata watu wa dini na madhehebu mbali mbali, kiasi kwamba, wanaweza kushirikishana amana na utajiri unaobubujika kutoka katika Waraka huu wa Kitume! Waraka wa Kitume wa "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” ni kitovu cha Mamlaka Matakatifu ya Ufundishaji katika Kanisa, mintarafu masuala ya kijamii kadiri ya Baba Mtakatifu Francisko. Huu ni muhtasari wa mafundisho, hotuba na mawazo yake tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki kunako mwaka 2013. Waraka huu wa kijamii unachota amana na utajiri mkubwa kutoka katika Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu uliotiwa mkwaju kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar, ulioko mjini Kairo, nchini Misri, tarehe 4 Februari  2019 huko Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu.

Hii ni nguzo msingi ya majadiliano ya kidini yanayopaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya waamini kama kielelezo na nguzo msingi wa ushirikiano na maelewano. Ni mwaliko na changamoto kwa waamini wa dini mbali mbali duniani, kuungana na kushikamana kwa kufanya kazi katika umoja na udugu wa kibinadamu, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Hati hii ni nguzo msingi ya haki, amani na upatanisho. Hati inakazia pamoja na mambo mengine kwamba: binadamu wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mwenyezi Mungu; wanatakiwa kusimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha: uhai wa binadamu, mazingira nyumba ya wote, sanjari na kushikamana na maskini pamoja na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Majadiliano ya kidini na ushirikiano ni mbinu mkakati na kigezo msingi katika mshikamano wa kidugu. Waraka wa Kitume wa "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” anasema, Dr. Andrea Tornielli, Mhariri Mkuu wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano katika tahariri yake kwamba ni waraka unaowagusa na kuwaambata watu wote. Unatoa dira na mwanga katika dhamana na utekelezaji wa masuala ya kisiasa na kijamii.

Hii ni sauti ya mtu aliaye nyikani, ikiwataka wanasiasa kujikita katika siasa safi na utawala bora. Sura ya Tano inazungumzia zaidi kuhusu Siasa Safi. Baba Mtakatifu anasema, upendo na fadhila za kiutu ziwe ni kwa ajili ya siasa safi inayohudumia haki msingi na amani, kila mtu akijitahidi kujikita katika mafao ya wengi, kama sehemu ya ujenzi wa mji wa Mungu hapa duniani, ili kuendeleza historia ya maisha ya familia ya binadamu. Haki na usawa; tabia ya kuheshimiana na kuthaminiana kama binadamu; ukweli, uwazi na uaminifu; ni tunu msingi zinazoboresha siasa safi. Mwanasiasa bora ni yule anayetambua dhamana na wajibu wake kwa jamii; anayeaminika na kuthaminiwa na jamii; ni kiongozi anayejitaabisha kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; mwaminifu katika ahadi zake kwa wananchi waliomchagua, daima akijitahidi kujenga na kudumisha umoja na mshikamano, tayari kuchochea mageuzi katika maisha ya watu; kwa kuwasikiliza na kutenda kwa ujasiri! Siasa safi inayojikita katika ujenzi wa amani inatambua karama za watu na inaendeleza majadiliano na watu ili waweze kuaminiana na kuthaminiana. Katika siasa kuna watu wanatafuta umaarufu si kwa ajili ya huduma kwa watu bali wanataka kuwanyonya na kujineemesha binafsi. Siasa safi inatengeneza fursa za ajira, inawalinda wafanyakazi na kupambana na umaskini wa hali na kipato. Inakuza na kudumisha umoja na mshikamano unaoratibiwa na kanuni ya auni.

Kati ya mambo nyeti na tata yanayodadavuliwa katika Waraka huu wa Kitume ni dhana ya vita na adhabu ya kifo; mambo ambayo yanakumbatiwa na utamaduni wa kifo. Waraka huu unachota amana na utajiri mkubwa kutoka katika Waraka wa Kitume wa Pacem in terris wa Mwaka 1963 unajikita katika: ukweli, haki, upendo na uhuru. Hakuna uhakika unaosadifu bila shaka yoyote kwamba adhabu ya kifo imekuwa na mafanikio katika kudhibiti makosa ya jinai sehemu mbali mbali za dunia. Hukumu ya kifo imepitwa na wakati na kwamba, ni adhabu inayokwenda kinyume cha haki msingi za binadamu! Kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inafutulia mbali adhabu ya kifo kwani maisha ya binadamu awaye yote ni matakatifu na yanapaswa kulindwa, kudumishwa na kuendelezwa tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake! Ndoto ya watu wa Mungu kwa wakati huu ni ujenzi wa misingi ya haki na amani; ili watu waweze kuwa na ndoto inayotekelezwa kwa pamoja, kabla mambo hayajaharibika sana!

Tahariri
06 October 2020, 15:38