Tafuta

Vatican News
Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko: "Fratelli tutti: Yaani "Wote Ni Ndugu": Kuhusu Udugu na Ufariki wa Kijamii: Kardinali Pietro Parolin: Mahusiano na mafungamano ya Kimataifa. Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko: "Fratelli tutti: Yaani "Wote Ni Ndugu": Kuhusu Udugu na Ufariki wa Kijamii: Kardinali Pietro Parolin: Mahusiano na mafungamano ya Kimataifa.  (ANSA)

Waraka wa Kitume Wa Papa Francisko: "Fratelli tutti": Mahusiano Ya Kimataifa!

Kardinali Parolin katika hotuba yake amejikita zaidi katika mahusiano na mafungamano makini ya Jumuiya ya Kimataifa. Amegusia malengo ya Waraka huu wa Kitume, mshikamano wa kidugu, utawala bora sanjari na ujenzi wa utamaduni wa udugu. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wa Kitume: "Fratelli tutti": Anagusia: Magonjwa jamii; Upendo; Wakimbizi, Mshikamano na Dini!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” umegawanyika katika sura nane: Sura ya Kwanza: Wingu jeusi limetanda duniani, hapa anagusia magonjwa jamii na changamoto zake katika ulimwengu mamboleo. Sura ya Pili ni kuhusu wageni njiani, Msamaria mwema anawekwa mbele ya walimwengu kuwa ni mfano bora wa kuigwa katika kutangaza na kushuhudia Injili ya upendo kwa maskini. Sura ya Tatu ni kuhusu mwono wa ulimwengu wazi, sehemu hii inakazia maisha ya kiroho, mshikamano wa kidugu, utu, heshima na haki msingi za binadamu. Sura ya Nne, Moyo uliofungukia ulimwengu wote, hapa changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani, utawala bora, ushirikiano na mshikamano katika kukabiliana na changamoto mamboleo ni mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele cha pekee. Sura ya Tano, ni kuhusu siasa safi zaidi kwa ajili ya huduma kwa jamii, maendeleo, ustawi na mafao ya wengi; utu, haki msingi za binadamu na umuhimu wa kufanya mageuzi makubwa kwenye Umoja wa Mataifa ili kweli uweze kuwa ni “familia ya Mataifa”.

Sura ya Sita inajikita zaidi katika mchakato wa majadiliano na urafiki ili kujenga sanaa ya watu kukutana. Katika sura ya Saba, Baba Mtakatifu anapembua kuhusu makutano yaliyopyaishwa ili kujenga misingi ya haki na amani; msamaha kwa kuondokana na “dhana ya vita ya haki na halali” ambayo kwa sasa imepitwa na wakati kama ilivyo pia kwa adhabu ya kifo kwani inakwenda kinyume cha haki msingi za binadamu, utakatifu na zawadi ya maisha kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu anapinga kwa nguvu zote utamaduni wa kifo! Sura ya Nane inakita maudhui yake katika dini na udugu; umuhimu wa dini kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu na kwamba, Kanisa litaendelea kujizatiti katika mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu kwa kuzingatia kanuni msingi za Kiinjili.

Mwishoni wa Waraka huu wa kitume, Baba Mtakatifu anagusia mambo msingi yanayofumbatwa katika Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu iliyotiwa saini kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar, ulioko mjini Kairo, nchini Misri, tarehe 4 Februari  2019 huko Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu. Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican ni kati ya wawezeshaji wakuu walioshiriki katika mkutano wa kwanza wa uzinduzi wa Waraka "Fratelli Tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” uliofanyika mjini Vatican, Jumapili tarehe 4 Oktoba 2020. Kardinali Parolin katika hotuba yake amejikita zaidi katika mahusiano na mafungamano makini ya Jumuiya ya Kimataifa. Amegusia malengo ya Waraka huu wa Kitume, mshikamano wa kidugu, utawala bora sanjari na ujenzi wa utamaduni wa udugu. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wa Kitume: "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” anapembua utamaduni wa udugu wa kibinadamu kama chombo cha ujenzi wa ushirikiano na mafungamano ya Jumuiya ya Kimataifa kwa kubainisha njia itakayotumika na malengo yake katika uhalisia wa maisha ya watu.

Baba Mtakatifu anakazia umuhimu wa ujenzi wa ushirikiano na mafungamano yanayokita mizizi yake katika maendeleo na ushirikiano katika masuala ya kiuchumi kwa kuzingatia majadiliano ili kufikia malengo yaliyokusudiwa yaani amani. Kwa sababu vita inasababisha maafa kwa watu na mali zao; vita ina sababisha vifo, inaharibu mazingira pamoja na kufisha matumaini ya watu. Majadiliano katika ukweli na uwazi yanavunjilia mbali kuta za utengano: kiroho na kiakili; yanafungua nafasi ya msamaha na kukoleza upatanisho. Majadiliano ni chombo cha haki kinachochochea na kuimarisha mahusiano na mafungamano ya Jumuiya ya Kimataifa kwa kukazia amani. Majadiliano yanafumbata uvumilivu, yanajielekeza katika mchakato wa ushuhuda kama chombo cha ujenzi wa udugu wa kibinadamu, upendo na mafao ya wengi.

Malengo ya Waraka wa Kitume:"Fratelli tutti" ni kuhamasisha ujenzi wa mshikamano wa kidugu unaoratibiwa na kanuni auni, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu. Hii ni dhana inayokumbatia maisha ya kifamilia, kijamii, kitaifa na kimataifa. Ili kufikia lengo hili, kuna haja ya kujenga na kudumisha tasaufi ya udugu wa kibinadamu kama chombo cha kufanyia kazi katika medani za kimataifa, ili kusaidia kupata suluhu ya matatizo yanayoikumba Jumuiya ya Kimataifa. Huu ni msaada mkubwa katika kupambana na changamoto mamboleo kama vile: Vita na kinzani mbali mbali; baa la njaa na umaskini duniani pamoja na athari za uharibifu wa mazingira nyumba ya wote. Kipaumbele cha kwanza ni ustawi, maendeleo na mafao ya wengi Mshikamano wa kidugu usaidie ujenzi wa mahusiano na mafungamano ya Jumuitya ya Kimataifa kama ilivyo pia miongoni mwa wananchi wenyewe. Ujasiri na ukarimu ni mambo yanayohitajika ili kufikia malengo ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Baba Mtakatifu Francisko anakazia utawala bora kama sehemu muhimu sana ya Mafundisho Jamii ya Kanisa. Utawala bora unaozingatia: sheria, kanuni na taratibu zinazopaswa kutekelezwa na wengi. Hapa, dhana ya “Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa” ni mfano bora wa kuigwa! Kumbe, utawala bora unapaswa kuakisi matakwa ya jamii na wala si hisia za mtu binafsi. Lengo ni kuhakikisha kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inasimama kidete kupambana na hatimaye, kung’oa baa la njaa, umaskini, magonjwa pamoja na kusimamia utekelezaji wa haki msingi za binadamu! Ujenzi wa utamaduni wa udugu wa kibinadamu uisaidie Jumuiya ya Kimataifa kupambana na changamoto mamboleo, kwa kusikiliza na kujibu kilio cha Mama Dunia na Maskini katika ujumla wao. Hii ni changamoto ya kuwafunda raia ili waweze kuwa watu wema, mashuhuda na wajenzi wa misingi ya haki na amani ya kudumu. Hapa kila mtu anapaswa kutekeleza dhamana na wajibu wake.

Mahusiano na mafungamano ya kimataifa yanaweza pia kuangaliwa kwa njia ya haki, amani, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi yanayozingatia haki msingi za binadamu pamoja na diplomasia ya kimataifa. Amani inafungamana na wajenzi wa amani duniani; haki msingi za binadamu zinatekelezwa kwa kuangalia mahitaji msingi ya watu kama ilivyokuwa kwa Msamaria mwema, mfano bora wa kuigwa. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano yake katika msingi wa utu na udugu wa kibinadamu. Jumuiya ya Kimataifa na wanadiplomasia anasema Kardinali Pietro Parolin pamoja na wale wote wanaojipambanua kwa kutafuta amani duniani wanao wajibu wa kupyaisha maisha ya watu wa Mungu, kwa kuzingatia utu na udugu wa kibinadamu, ili kudumisha amani, utulivu na mafao ya wengi. Udugu wa kibinadamu unakita mizizi yake katika umoja na ushirikiano. Kwa njia ya utamaduni wa udugu wa kibinadamu, Baba Mtakatifu Francisko anakazia dhana ya upendo kwa watu wote, ili kujenga mahusiano, sheria, kanuni na taratibu zinazopania kudumisha amani na kuboresha maisha ya watu wote wa Mungu katika ujumla wao.

Kardinali Parolin
05 October 2020, 15:31