Tafuta

Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko: "Frateri tutti: Yaani "Wote Ni Ndugu": Kuhusu Udugu na Ufariki wa Kijamii utazinduliwa rasmi tarehe 4 Oktoba 2020. Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko: "Frateri tutti: Yaani "Wote Ni Ndugu": Kuhusu Udugu na Ufariki wa Kijamii utazinduliwa rasmi tarehe 4 Oktoba 2020. 

Waraka wa Kitume : "Fratelli tutti": Yaani "Wote Ni Ndugu": Udugu na Urafiki

Waraka wa Kitume: "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” umegawanyika katika sura nane: Wingu jeusi limetanda duniani; kuhusu wageni njiani; mwono wa ulimwengu; Moyo uliofungukia ulimwengu wote, siasa safi; majadiliano na urafiki. Makutano yaliyopyaishwa; Dini na udugu; umuhimu wa dini kulinda na kudumisha misingi ya haki na amani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko: "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii”, umetiwa mkwaju tarehe 3 Oktoba 2020 huko mjini Assisi, Italia na kuzinduliwa rasmi tarehe 4 Oktoba 2020 sanjari na Maadhimisho ya Sikukuu ya Mtakatifu Francisko wa Assisi aliyejikita katika: huduma bora kwa maskini, amani na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Udugu na urafiki wa kijamii ni dira na mwongozo wa mchakato wa ujenzi wa ulimwengu ulio bora zaidi na unaosimikwa katika misingi ya haki, amani na utulivu, dhamana na wajibu wa: watu wote pamoja na taasisi mbalimbali. Baba Mtakatifu anapinga kwa nguvu zote vita na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine.Waraka huu unajikita zaidi katika masuala msingi ya kijamii katika maisha ya mwanadamu. “Wote ni ndugu” ni maneno aliyokuwa anatumia Mtakatifu Francisko wa Assisi akiwataka ndugu zake watawa kuishi kadiri ya kanuni msingi za Kiinjili, kama njia ya kumwilisha upendo wa Mungu kwa binadamu, kiasi cha kujenga jamii inayosimikwa katika udugu wa kibinadamu. Waraka huu pamoja na mambo mengine unapania kuwahamasisha walimwengu kujenga udugu wa kibinadamu na urafiki wa kijamii kwa kutambua kwamba, wote ni watoto wa Baba mmoja, yaani Mungu mwenyezi, licha ya tofauti zao msingi.

Katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia, kuna mwingiliano mkubwa wa watu, kumbe, hakuna anayeweza kujiokoa mwenyewe, bali wote wanategemeana na kukamilishana. Baba Mtakatifu Francisko anapenda kufanya rejea za mara kwa mara katika Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu iliyotiwa mkwaju mwezi Februari 2019. Huu ni udugu unaopaswa kumwilishwa katika matendo kwa kutoa kipaumbele cha pekee kwa: Utu, heshima na haki msingi za binadamu; Ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Huu ni udugu unaofumbatwa katika: ukweli, haki, upendo na uhuru kamili. Baba Mtakatifu anapenda pia kukazia msamaha na upatanisho wa kweli; kumbukumbu hai pamoja na haki. Kila mtu anao wajibu na haki ya kulinda utu na heshima yake, kwa sababu ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Waraka huu wa Kitume wakati unaendelea kutungwa, mara ghafla, likazuka janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 na hivyo kuzua dharura ya afya duniani na kwamba, hakuna mtu awaye yote anayeweza kujiokoa mwenyewe, kwani “Wote ni Ndugu”.

Waraka wa Kitume"Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” umegawanyika katika sura nane: Sura ya Kwanza: Wingu jeusi limetanda duniani, hapa anagusia magonjwa jamii na changamoto zake katika ulimwengu mamboleo. Sura ya Pili ni kuhusu wageni njiani, Msamaria mwema anawekwa mbele ya walimwengu kuwa ni mfano bora wa kuigwa katika kutangaza na kushuhudia Injili ya upendo kwa maskini. Sura ya Tatu ni kuhusu mwono wa ulimwengu wazi, sehemu hii inakazia maisha ya kiroho, mshikamano wa kidugu, utu, heshima na haki msingi za binadamu. Sura ya Nne, Moyo uliofungukia ulimwengu wote, hapa changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani, utawala bora, ushirikiano na mshikamano katika kukabiliana na changamoto mamboleo ni mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele cha pekee. Sura ya Tano, ni kuhusu siasa safi zaidi kwa ajili ya huduma kwa jamii, maendeleo, ustawi na mafao ya wengi; utu, haki msingi za binadamu na umuhimu wa kufanya mageuzi makubwa kwenye Umoja wa Mataifa ili kweli uweze kuwa ni “familia ya Mataifa”.

Sura ya Sita inajikita zaidi katika mchakato wa majadiliano na urafiki ili kujenga sanaa ya watu kukutana. Katika sura ya Saba, Baba Mtakatifu anapembua kuhusu makutano yaliyopyaishwa ili kujenga misingi ya haki na amani; msamaha kwa kuondokana na “dhana ya vita ya haki na halali” ambayo kwa sasa imepitwa na wakati kama ilivyo pia kwa adhabu ya kifo kwani inakwenda kinyume cha haki msingi za binadamu, utakatifu na zawadi ya maisha kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu anapinga kwa nguvu zote utamaduni wa kifo! Sura ya Nane inakita maudhui yake katika dini na udugu; umuhimu wa dini kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu na kwamba, Kanisa litaendelea kujizatiti katika mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu kwa kuzingatia kanuni msingi za Kiinjili. Mwishoni wa Waraka huu wa kitume, Baba Mtakatifu anagusia mambo msingi yanayofumbatwa katika Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu iliyotiwa saini kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar, ulioko mjini Kairo, nchini Misri, tarehe 4 Februari  2019 huko Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu. Huu ni mwaliko na changamoto kwa waamini wa dini mbali mbali duniani, kuungana na kushikamana, ili kufanya kazi katika umoja na udugu wa kibinadamu, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Hati hii ni nguzo msingi ya haki, amani na upatanisho.

Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko: "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii”: Sura ya Kwanza: Wingu Jeusi Limetanda Duniani. Waraka unapembua kwa kina na mapana mambo msingi ambayo yamechakachuliwa katika ulimwengu mamboleo na hivyo kupindisha ukweli wake. Kati ya mambo hayo ni: dhana ya demokrasia, uhuru, haki pamoja na kupotea kwa maana halisi ya jumuiya ya kijamii na historia yake. Matokeo yake ni kuibuka kwa sera za ubinafsi na tabia ya kutowajali wengine katika mambo msingi kama vile vile mafao ya wengi. Kinachopewa kipaumbele cha kwanza ni mantiki ya soko huria linalotafuta kupata faida kubwa hata kwa gharama ya utu na heshima ya binadamu. Leo hii kuna utandawazi usioguswa na mahangaiko ya wengine ndio huo “utamaduni wa kutupa”; ukosefu wa fursa za ajira, mifumo mbalimbali ya ubaguzi, umaskini; ukosefu wa haki msingi na utekelezaji wake. Kuibuka na kukomaa kwa mifumo ya utumwa mamboleo kama vile biashara ya binadamu na viungo vyake; utamaduni wa kifo unaofumbatwa katika sera za utoaji mimba na kifo laini. Waraka unajadili matatizo na changamoto hizi kwa kuitaka Jumuiya ya Kimataifa kuchukua hatua madhubuti ili kukomesha mambo haya yanayohatarisha mustakabali wa binadamu duniani. Baba Mtakatifu anaonya tabia inayoendelea kuzuka ya watu kutaka kujenga kuta za utengano zinazokita mizizi yake katika biashara haramu ya silaha duniani na matokeo yake ni kuendelea kuibuka kwa makundi ya uhalifu kitaifa na kimataifa, hali ambayo ni matokeo ya upweke hasi!

Sura ya Pili ni Kuhusu Wageni Njiani: Licha ya wingu jeusi kutanda katika uso wa dunia, lakini, Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuweka mbele ya macho ya waamini na watu wote wenye mapenzi mema mfano wa Msamaria mwema kama nanga ya matumaini. Msamaria mwema anawahamasisha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujitahidi kuwa watu wema kwa jirani zao, kwa kushinda na kuvuka vikwazo vya maamuzi mbele, mafao binafsi sanjari na vikwazo vya kihistoria na kitamaduni. Watu wote wanapaswa kutambua kwamba, wanawajibika kujenga na kudumisha jamii fungamani na jumuishi, ambayo iko tayari kuwainua wale walioteleza na kuanguka au wale wanateseka kwa sababu mbalimbali. Kwa namna ya pekee kabisa, Wakristo wanapaswa kumtambua Kristo Yesu anayeteseka kati pamoja na waja wake wanaotengwa, wanaodhulumiwa na kunyanyaswa!

Sura ya Tatu ni Kuhusu Mwono wa Ulimwengu Wazi: Hapa Baba Mtakatifu anazungumzia kanuni na uwezo wa kupenda, kwa kujitoa katika ubinafsi ili kuweza kupata maana halisi ya maisha kutoka kwa jirani, kama kielelezo cha Injili ya upendo na utilifu wa maisha ya wote. Katika muktadha huu, Waraka wa Kitume unafanya rejea katika maisha ya kiroho yanayopimwa kwa mwanga wa upendo unaochukua nafasi ya kwanza na kuwasukuma kutafuta maisha bora zaidi kwa ajili ya wengine, mbali kabisa na utamaduni wa ubinafsi. Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba, utambuzi wa maana ya mshikamano na udugu wa kibinadamu vinaanza ndani ya familia; mambo yanayopaswa kulindwa na kuheshimiwa katika mchakato wa kwanza na muhimu katika sekta ya elimu. Kila mtu anayo haki ya kuishi maisha yanayokidhi vigezo vya utu na heshima ya binadamu na kwamba, haki haina mipaka kwani haijalishi mahali alipozaliwa mtu. Kumbe, kuna haja ya kuzingatia kanuni maadili katika mahusiano na mafungamano ya Kimataifa, kwa sababu nchi zote ni mali ya wageni na mafao, kumbe kuna haja ya kuwa na mgawanyo bora zaidi wa mali za ulimwengu. Mtu anayo haki ya kumiliki mali binafsi, lakini mkazo unawekwa zaidi kwenye matumizi ya jumla ya bidhaa zinazozalishwa. Waraka unagusia pia deni kubwa la nje kwa Mataifa changa zaidi duniani. Kimsingi na kikanuni, deni lazima lilipwe, lakini kuna haja ya kuangalia kwamba, mchakato wa ulipaji wa deni la nje kutoka katika nchi changa duniani, lazima liangaliwe kwa umakini mkubwa ili lisilete madhara makubwa katika ukuaji wa uchumi na maisha ya watu katika Nchi changa zaidi ulimwenguni.

Sura ya Nne, Moyo uliofungukia ulimwengu wote: Baba Mtakatifu anajadili kwa kina na mapana juu ya wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani, wanaoendelea hata kuhatarisha maisha yao wakitafuta: usalama, hifadhi na maisha bora zaidi. Hawa ni watu wanaokimbia: vita, dhuluma na nyanyaso; majanga asilia; na wakati mwingine wanatumbukizwa kwenye mifumo ya utumwa mamboleo na hivyo kung’olewa kutoka katika jumuiya zao asilia. Sera na mbinu mkakati wa Kanisa Katoliki katika huduma kwa wakimbizi na wahamiaji inajikita katika mambo makuu manne yaani: “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji” katika maisha ya jamii inayowapokea na kuwapatia hifadhi na usalama wa maisha! Baba Mtakatifu anapenda kutoa onyo kali kwa kusema kwamba, kama hakuna sababu msingi za kumfanya mtu kuikimbia nchi yake, ni vyema kila mtu akabaki katika nchi yake asilia. Hata hivyo kuna haja ya kuheshimu haki ya watu kutafuta maisha bora zaidi ugenini. Kumbe, hapa kuna haja ya kuhakikisha kwamba, nchi wahisani ambazo zinazotoa hifadhi kwa wakimbizi na wahamiaji zinaangalia kwanza haki za raia wao pamoja na kuhakikisha kwamba, zinaweza kutoa huduma kwa wakimbizi na wahamiaji, hasa kwa wale wanaokimbia majanga asilia. Watu wapewe hati za kuishi, fursa za mafunzo na ajira na kuwepo na sera za kuziunganisha familia zilizotengana. Watoto walindwe na kuendelezwa pamoja na watu kuhakikishiwa uhuru wa kidini. Kinachotakiwa hapa ni utawala bora kutoka katika Jumuiya ya Kimataifa, ushirikiano na mshikamano wa kidugu kwa ajili ya huduma kwa wakimbizi na wahamiaji kwa kuibua, kupanga na kutekeleza sera za muda mrefu kwa ajili ya wakimbizi, ili kuondokana na utekelezaji wa mipango ya “zima moto” na badala yake, kuwepo na mpango mkakati wa maendeleo kwa wote.

Sura ya Tano: Siasa Safi Zaidi: Baba Mtakatifu anasema, upendo na fadhila za kiutu ziwe ni kwa ajili ya siasa safi inayohudumia haki msingi na amani, kila mtu akijitahidi kujikita katika mafao ya wengi, kama sehemu ya ujenzi wa mji wa Mungu hapa duniani, ili kuendeleza historia ya maisha ya familia ya binadamu. Haki na usawa; tabia ya kuheshimiana na kuthaminiana kama binadamu; ukweli, uwazi na uaminifu; ni tunu msingi zinazoboresha siasa safi. Mwanasiasa bora ni yule anayetambua dhamana na wajibu wake kwa jamii; anayeaminika na kuthaminiwa na jamii; ni kiongozi anayejitaabisha kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; mwaminifu katika ahadi zake kwa wananchi waliomchagua, daima akijitahidi kujenga na kudumisha umoja na mshikamano, tayari kuchochea mageuzi katika maisha ya watu; kwa kuwasikiliza na kutenda kwa ujasiri! Siasa safi inayojikita katika ujenzi wa amani inatambua karama za watu na inaendeleza majadiliano na watu ili waweze kuaminiana na kuthaminiana. Katika siasa kuna watu wanatafuta umaarufu si kwa ajili ya huduma kwa watu bali wanataka kuwanyonya na kujineemesha binafsi. Siasa safi inatengeneza fursa za ajira, inawalinda wafanyakazi na kupambana na umaskini wa hali na kipato. Inakuza na kudumisha umoja na mshikamano unaoratibiwa na kanuni ya auni.

Siasa safi inajielekeza zaidi katika kujibu kero zinazopelekea uvunjwaji wa haki msingi za binadamu na kuwatumbukiza watu katika mifumo ya utumwa mamboleo, ubidhaishaji maumbile ya binadamu; biashara haramu ya silaha na dawa za kulevya pamoja na matumizi yake haramu; ukahaba wa utalii, kazi za suluba, vitendo vya kigaidi yote haya ni uhalifu dhidi ya utu na heshima ya binadamu pamoja na baa la njaa linalowakosesha mamilioni ya watu haki ya chakula na lishe bora. Watu wa Mungu wanahitaji siasa safi inayotoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu na wala si katika mfumo wa fedha na soko huria linalokita mizizi yake katika faida kubwa. Ni katika muktadha huu, vyama vingi vya kijamii vinaendelea kuibuka kama “wimbi la nguvu za kimaadili” zinazopaswa kutumiwa na jamii kwa kuratibiwa vyema, ili kwenda sanjari na sera ya siasa kwa ajili pamoja na watu maskini. Baba Mtakatifu anagusia pia umuhimu wa kufanya mageuzi makubwa katika Umoja wa Mataifa, ili kweli uweze kuwa ni “Familia ya Mataifa”. Umoja wa Mataifa usimame kidete kupigania ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; ipambane na umaskini, kwa kulinda haki msingi za binadamu. Umoja wa Mataifa uwe ni jukwaa la majadiliano katika ukweli na uwazi; upatanisho na mwamuzi. Umoja wa Mataifa ujikite katika utekelezaji wa sera ya nguvu ya sheria na wala si sheria ya nguvu!

Sura ya Sita: Majadiliano na Urafiki: Katika sura hii, Baba Mtakatifu Francisko anakazia umuhimu wa kukoleza majadiliano na urafiki katika jamii kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa sanaa na utamaduni wa watu kukutana, hata na wale ambao wako pembezoni mwa jamii bila kuwasahau watu asilia kwa sababu kila mtu anaweza kujifunza kutoka kwa mwingine. Hakuna mtu ambaye hafai kwa lolote na wala mtu mwenye thamani kubwa kuliko mwingine. Baba Mtakatifu anakazia kwa namna ya pekee umuhimu wa kukuza muujiza wa urafiki, mwelekeo unaopaswa kuvumbuliwa upya kama nyota angavu katikati ya giza nene ili kumwondona mwanadamu kutoka katika ukatili wa kutisha unaoendelea “kutamba” katika ulimwengu mamboleo. Hali ya watu kukata tamaa inapelekea watu haohao kubomoa madaraja yanayowaunganisha watu!

Sura ya Saba: Makutano Yaliyopyaishwa: Baba Mtakatifu anawahimiza watu wa Mungu kujenga utamaduni wa kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu kwa kutambua kwamba, amani ya kweli inasimikwa katika ukweli, haki na huruma. Huu ni mwaliko wa kuondokana na tabia ya kutaka kulipizana kisasi na badala yake, watu wajikite katika mchakato wa ujenzi wa jamii inayojipambanua kwa ajili ya huduma kwa wengine, ili kukuza na kudumisha ari na moyo wa upatanisho, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Amani ni sanaa inawayowashirikisha watu wote na kila mmoja anapaswa kutekeleza dhamana na wajibu wake barabara. Msamaha wa kweli unafungamanishwa na amani na kwamba, watu wajenge utamaduni wa kupendana bila ubaguzi. Hata kuwapenda wale wanaodhani kuwa ni adui zao, kunasaidia kuleta mabadiliko na hivyo kumsaidia kutoendelea na udhalimu wake. Msamaha unakwenda sanjari na haki pamoja na kumbukumbu endelevu kwa sababu kusamehe hakuna maana ya kusahau, bali ni mchakato wa “kufyekelea mbali” nguvu ya uovu inayoangamiza na kutaka kulipiza kisasi. Jumuiya ya Kimataifa kamwe haiwezi kusahau mauaji ya kimbari ya “Shoah”, mashambulizi ya mabomu ya atomik kule Hiroshima na Nagasaki; madhulumu na mauaji ya kikabila sehemu mbalimbali za dunia. Haya ni matukio ambayo yanapaswa kukumbukwa daima anasema Baba Mtakatifu Francisko, ili kuendelea kupyaisha dhamiri za watu, lakini zaidi ya yote ni vyema kukumbuka na kuenzi mazuri ya watu!

Dhana ya vita halali na ya haki imepitwa na wakati kwani, vita haina macho wala pazia! Kanisa kwa asili, maisha na utume wake anasema Baba Mtakatifu linapaswa kuwa ni chombo cha haki, amani na upatanisho. Leo hii amani ni changamoto pevu kutokana na kushamiri kwa biashara ya silaha duniani; uchu wa mali na utajiri wa muda mfupi unawafumba watu macho kiasi cha kushindwa kuona mahitaji ya jirani zao. Kumbe, amani inafumbatwa katika: ukweli, haki, upendo na uhuru. Vita ni kielelezo cha kushindwa kwa siasa na mwanadamu katika ujumla wake. Amani inatishiwa na uwepo wa silaha za maangamizi: za kemikali pamoja na silaha za kibayolojia zinazoweza kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kujizatiti kikamilifu kuhakikisha kwamba, kunakuwepo na amani duniani na kwamba, migogoro mbali mbali inapatiwa ufumbuzi wa amani, ili kujenga na kudumisha umoja, udugu na urafiki kati ya watu kwa kuzingatia kanuni maadili, ulinzi na usalama wa Jumuiya ya Kimataifa. Upigaji rufuku wa silaha za kinyuklia ni changamoto ya kimaadili na dhamana ya kiutu kwa kukazia kanuni maadili zinazoendeleza amani duniani; ushirikiano katika ulinzi na usalama. Rasilimali fedha inayowekezwa kwenye utengenezaji, ulimbikizaji na matumizi ya silaha za maangamizi ielewekezwe katika Mfuko wa Kimataifa wa Kupambana na baa la njaa duniani.

Adhabu ya Kifo: Hakuna uhakika unaosadifu bila shaka yoyote kwamba hukumu ya kifo imekuwa na mafanikio makubwa katika kudhibiti makosa ya jinai sehemu mbali mbali za dunia. Hukumu ya kifo imepitwa na wakati na kwamba, ni adhabu inayokwenda kinyume cha haki msingi za binadamu! Kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inafutulia mbali adhabu ya kifo kwani maisha ya binadamu awaye yote ni matakatifu na yanapaswa kulindwa, kudumishwa na kuendelezwa tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake! Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, leo hii, kuna baadhi ya watu katika familia ya binadamu wanathubutu kukumbatia utamaduni wa kifo kwa kutoa mimba, kuwafyekelea mbali maskini, walemavu pamoja na wazee.

Sura ya Nane: Dini na Udugu: Dini zina mchango mkubwa katika kukuza na kudumisha haki na amani duniani kwa kujikita katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote; kwa kutambua kwamba, huu ni msingi katika mchakato wa kukuza na kudumisha haki na amani. Waamini wa dini mbalimbali wanapaswa kutambua kwamba, wanashirikishana tunu msingi katika maisha yao; tunu ambazo zinafumbata kwa namna ya pekee, utu wa binadamu. Dini zinapaswa kujielekeza zaidi katika huduma kwa binadamu na kuondokana na tatizo la tafsiri potofu ya Vitabu Vitukufu, hali ambayo imepelekea kuibuka kwa misimamo mikali ya kidini na kiimani na matokeo yake ni kushamiri kwa vitendo vya kigaidi sehemu mbalimbali za dunia. Sera potofu kuhusu baa la njaa, umaskini, ukosefu wa haki na dhuluma ni hatari kwa umoja, mshikamano na mafungamano ya kijamii duniani. Hija ya amani miongoni mwa waamini wa dini mbalimbali ni jambo linalowezekana ndiyo maana kuna haja ya kudumisha uhuru wa kidini, msingi wa haki zote za binadamu. Kanisa katika maisha na utume wake, litaendelea kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadharani, kwa kujielekeza zaidi katika sera na mikakati inayogusa maisha ya mtu mzima: kiroho na kimwili; ustawi, maendeleo na mafao ya wengi mintarafu kanuni msingi za Habari Njema ya Wokovu.

Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu ilitiwa mkwaju kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar, ulioko mjini Kairo, nchini Misri, tarehe 4 Februari  2019 huko Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu. Hii ni nguzo msingi ya majadiliano ya kidini yanayopaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya waamini kama kielelezo makini cha ushirikiano na maelewano kama kigezo msingi. Ni mwaliko na changamoto kwa waamini wa dini mbali mbali duniani, kuungana na kushikamana, ili kufanya kazi katika umoja na udugu wa kibinadamu, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Hati hii ni nguzo msingi ya haki, amani na upatanisho. Hati inakazia pamoja na mambo mengine kwamba: binadamu wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mwenyezi Mungu; wanatakiwa kusimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha: uhai wa binadamu, mazingira nyumba ya wote, sanjari na kushikamana na maskini pamoja na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii.

Waraka: Wote ni Ndugu

 

 

04 October 2020, 14:03