Tafuta

Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko: "Fratelli tutti: Yaani "Wote Ni Ndugu": Kuhusu Udugu na Ufariki wa Kijamii: Yaliyojiri kwenye mkutano wa kwanza baada ya kuzinduliwa kwa Waraka huu. Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko: "Fratelli tutti: Yaani "Wote Ni Ndugu": Kuhusu Udugu na Ufariki wa Kijamii: Yaliyojiri kwenye mkutano wa kwanza baada ya kuzinduliwa kwa Waraka huu. 

Waraka wa Papa Francisko: "Fratelli tutti": Yaliyojiri Mkutanoni!

Waraka wake wa Kitume "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” yaliyojiri kwenye mkutano wa kwanza kuhusu Waraka huu: Mahusiano na mafungamano ya kimataifa; Majadiliano ya kidini; athari za vita duniani; Umuhimu wa kudumisha ukweli, wema, uhuru na udugu: Dhana ya Msamaria mwema inakita mizizi yake huduma na urafiki wa upendo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 4 Oktoba 2020 amezindua Waraka wake wa Kitume "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii”. Uzinduzi huu umekwenda sanjari na mkutano wa kimtaifa uliopembua kwa kina na mapana maudhui yaliyomo kwenye Waraka huu ambao unajikita zaidi katika masuala ya kijamii. Kati ya wawezeshaji wakuu alikuwa ni Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican ambaye amekita mawazo yake mintarafu mahusiano na mafungamano ya Kimataifa. Kardinali Miguel Ángel Ayuso Guixot, M.C.C.I, Rais wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini, amezungumzia kuhusu umuhimu wa majadiliano ya kidini katika maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko. Professa Andrea Riccardi, Muasisi wa Jumuiya ya Mtakatifu Egidio na Jaalimu wa Historia mamboleo amekazia kuhusu dhana ya udugu katika kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano. Wengine ni Jaji Mohamed Mahmoud Abdel Salaam, Katibu mkuu wa Kamati Kuu ya Utekelezaji wa Hati ya Udugu wa Kibinadamu amedadavua kuhusu; ukweli, wema, uhuru na udugu. Kwa upande wake, Professa Anna Rowlands, Jaalimu wa Mafundisho Jamii ya Kanisa na Utekelezaji wake kutoka Chuo Kikuu cha Durham, nchini Uingereza amekazia kuhusu dhana ya Msamaria mwema inayofumbatwa katika upendo, sheria na ujenzi wa urafiki wa kijamii.

Kardinali Miguel Ángel Ayuso Guixot, M.C.C.I, Rais wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini amempongeza sana Jaji Mohamed Mahmoud Abdel Salaam, Katibu mkuu wa Kamati Kuu ya Utekelezaji wa Hati ya Udugu wa Kibinadamu kama kielelezo makini cha udugu wa kibinadamu, kwa kutambua umuhimu wa dini katika mchakato wa kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu na kwamba, Kanisa litaendelea kujizatiti katika mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu kwa kuzingatia kanuni msingi za Kiinjili. Majadiliano ya kidini ni kati ya vipaumbele vya maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko anayetamani kuwaona waamini wa dini mbalimbali wakiheshimiana na kuthaminiana kama ndugu wa Baba mmoja yaani, Mwenyezi Mungu. Majadiliano ya kidini ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa, vilivyopewa kipaumbele cha pekee na Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican na kwa sasa Baba Mtakatifu Francisko anataka kukazia udugu wa kibinadamu.

Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu iliyotiwa saini kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar, ulioko mjini Kairo, nchini Misri, tarehe 4 Februari  2019 huko Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu ni nguzo msingi ya majadiliano ya kidini inayochota maudhui yake katika udugu wa kibinadamu. Msingi wake ni ukweli na ushirikishwaji wa mang’amuzi ya maisha, hekima na ushuhuda unaopania kujenga jamii inayosimikwa katika: haki, umoja na mshikamano; uaminifu na upendo kwa ajili, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, maskini wakipewa kipaumbele cha kwanza. Huu ni mchakato wa ujenzi wa umoja katika tofauti, kila mwamini akitambua mambo msingi ya dini yake, ili hatimaye, waamini wa dini mbali mbali duniani waweze kuwa ni wajenzi wa jamii inayosimikwa katika haki, amani na maridhiano hasa katika ulimwengu mamboleo. Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, ndiye Muumba wa vyote vinavyoonekana na vile visivyoonekana na kwamba, binadamu wote wanaunda familia moja na kubwa ya binadamu.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini wa dini mbalimbali duniani kujenga jamii stahimilivu, kwa kuendelea kutoa kipaumbele cha pekee katika huduma ya udugu wa kibinadamu, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya binadamu wote. Umoja na mshikamano wa kidugu uwe ni sehemu ya majadiliano ya kidini ili kusimama kidete kulinda na kutunza misingi ya haki, amani na maridhiano. Majadiliano ya kidini yawe ni nguzo imara katika ujenzi wa urafiki wa kijamii, ili kudumisha usawa kwa watu wote. Professa Andrea Riccardi, Muasisi wa Jumuiya ya Mtakatifu Egidio na Jaalimu wa Historia mamboleo anakazia udugu wa kibinadamu kama chachu ya kuondokana na vita na kinzani za maisha ambazo mara nyingi zimekuwa zikiendeshwa na viongozi wa serikali na kisiasa wakati wananchi wa kawaida wanaambulia madhara yake. Vita ni tishio kubwa la amani duniani. Udugu wa kibinadamu ni sehemu ya tunu msingi za Kiinjili na kiutu! Vita ni kati ya matukio ambayo yanaendelea kuacha majanga makubwa katika maisha ya watu. Watu wanapaswa kuzingatia historia na kuwa na kumbukumbu hai. Umefika wakati kwa familia ya binadamu kugundua tena na tena udugu wa kibinadamu, amani, demokrasia na umoja na kwamba, majadiliano katika ukweli na uwazi, yawe ni sehemu ya utamaduni wa kuzuia vita duniani.

Vita inaendelea kuangamiza maisha ya binadamu, kuharibu mazingira pamoja na miundombinu. Vita na kinzani mbali mbali zimekuwa ni chanzo cha kuibuka kwa wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani; chuki na uhasama. Vitendo vya kigaidi ni uhalifu mkubwa dhidi ya utu na heshima ya binadamu. Huu ni wakati wa kukumbatia na kumwilisha ndoto ya amani duniani, changamoto inayopaswa kuvaliwa njuga na waamini wa dini mbali mbali duniani. Mtakatifu Yohane Paulo II anasema, Jumuiya ya Kimataifa inawahitaji manabii na wajenzi wa amani, ili kudumisha udugu wa kibinadamu. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kudumisha utawala wa sheria utakaowawezesha wote kujisikia kuwa ni ndugu wamoja. Jaji Mohamed Mahmoud Abdel Salaam, Katibu mkuu wa Kamati Kuu ya Utekelezaji wa Hati ya Udugu wa Kibinadamu, amekazia: ukweli, wema, uhuru na udugu wa kibinadamu. Anampongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa ujasiri wake, kwa kusimama kidete kulinda, kutetea utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Waraka huu wa Kitume ni chachu ya matumaini kwa watu waliokata tamaa, ili kuanza mchakato wa kupyaisha udugu wa kibinadamu, kwa kuondokana na ubinafsi na uchoyo; utaifa usiokuwa na mvuto wala mashiko pamoja na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine. Umoja, upendo na mshikamano ni mambo msingi yanayopaswa kuvaliwa njuga na wote!Janga la Virusi vya Corona, COVID-19 liisaidie Jumuiya ya Kimataifa kuibua mtindo mpya wa maisha. Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu pamoja na Waraka wa Kitume "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” ni nguzo msingi katika kulinda na kudumisha: utu, heshima na haki msingi za binadamu. Kamati Kuu ya Utekelezaji wa Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa siku za usoni, inatarajia kuandaa makongamano kadhaa kwa ajili ya vijana wa kizazi kipya, ili maudhui ya ujumbe huu yaweze kuwafikia watu wengi zaidi. Kumbe, kuna haja ya kushirikiana na kushikamana ili kufikia malengo ya ujenzi wa udugu wa kibinadamu.

Kwa upande wake, Professa Anna Rowlands, Jaalimu wa Mafundisho Jamii ya Kanisa na Utekelezaji wake kutoka Chuo Kikuu cha Durham, nchini Uingereza anasema, dhana ya “Fratelli tutti” yaani “Wote ni Ndugu” ni changamoto inayokita mizizi yake katika wongofu wa kiekolojia, masuala ya kisiasa, kiuchumi na kijamii kwa kutambua kwamba, wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mwenyezi Mungu. Udugu wa kibinadamu na urafiki wa kijamii ni sawa na chanda na pete; ni mambo yanayotegemeana na kukamilishana, ili kujenga umoja na mafungamano miongoni mwa waamini wa dini mbali mbali duniani. Waamini wanapaswa kujielekeza zaidi katika mchakato wa toba na wongofu wa ndani, ili hatimaye, waweze kuwa ni mifano bora katika mchakato wa majadiliano ya kidini, wajenzi wa haki na amani; na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Waamini wajenge utamaduni wa watu kukutana ili kukuza na kudumisha utu, mshikamano pamoja na ugawanaji na matumizi bora ya rasilimali na amana za ulimwengu huu. Lengo ni kujenga jamii inayosimikwa katika ukweli, kwa kuwashirikisha watu wote. Waraka huu wa Kitume unatumia lugha ya upendo inayowaunganisha watu na viumbe vyote.

Mkutano wa Fratelli Tutti
04 October 2020, 13:32