Tafuta

Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko: "Fratelli tutti: Yaani "Wote Ni Ndugu": Kuhusu Udugu na Ufariki wa Kijamii utazinduliwa rasmi tarehe 4 Oktoba 2020 wakati wa maadhimisho ya Sikukuu ya Mt. Francisko wa Assisi. Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko: "Fratelli tutti: Yaani "Wote Ni Ndugu": Kuhusu Udugu na Ufariki wa Kijamii utazinduliwa rasmi tarehe 4 Oktoba 2020 wakati wa maadhimisho ya Sikukuu ya Mt. Francisko wa Assisi. 

Waraka wa Papa Francisko: "Fratelli tutti": Udugu Ni Zawadi

Ndugu katika umoja wao ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, wanapaswa kupokelewa, kuheshimiwa, kuthaminiwa, lakini zaidi kupendwa jinsi walivyo katika udhaifu na utofauti wao, kazi ya Roho Mtakatifu. Udugu unapomwilishwa katika uhalisia wa maisha unakuwa ni chachu ya mageuzi ya dhati kabisa, kwa kutambua wote ni watoto wa Baba mmoja, yaani Mwenyezi Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko tarehe 3 Oktoba 2020 majira ya jioni baada ya kuadhimisha Ibada ya Misa takatifu kwenye Kanisa lililoko chini ya Kanisa kuu la Mtakatifu Francisko wa Assisi, mjini Assisi, nchini Italia, atatia mkwaju kwenye Waraka wake wa Kitume ambao umepewa kichwa cha habari "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii”. Waraka utazinduliwa rasmi tarehe 4 Oktoba 2020 katika maadhimisho ya Sikukuu ya Mtakatifu Francisko wa Assisi aliyekazia: amani, utunzaji bora wa mazingira pamoja na huduma makini kwa maskini, aliyeteuliwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa ni somo wake katika maisha na utume kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. “Fratelli Tutti” yaani “Wote ni Ndugu” kama Waraka huu wa kitume utakavyojulikana ni utajiri wa maneno kutoka kwa Mtakatifu Francisko wa Assisi, anayewaalika ndugu zake watawa wote, kuchukuliana kama ndugu; na kwa mchungaji mwema, ili kuweza kuwaokoa kondoo wake anavumilia mateso ya Msalaba.

Katika maisha ya Mtakatifu Francisko wa Assisi udugu wa kibinadamu ni uhalisia unaotambua maisha kuwa ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Waraka huu ni mwendelezo wa tafakari ya Baba Mtakatifu Francisko kuhusu utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote kama anavyouchambua katika Waraka wa Kitume: “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”. Hii ni tafakari inayozama katika utu na heshima ya binadamu kwa kutambua kwamba, Mtakatifu Francisko wa Assisi alijisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma ya upendo kwa maskini na hasa wagonjwa wa ukoma, ushuhuda angavu wa Injili. Ndugu katika umoja wao ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, wanapaswa kupokelewa, kuheshimiwa, kuthaminiwa, lakini zaidi kupendwa jinsi walivyo katika udhaifu na utofauti wao, kazi ya Roho Mtakatifu. Udugu unapomwilishwa katika uhalisia wa maisha unakuwa ni chachu ya mageuzi ya dhati kabisa, kwa kutambua wote ni watoto wa Baba mmoja, yaani Mwenyezi Mungu, mwingi wa huruma na mapendo na wala hakuna sababu ya kuangaliana kwa “macho ya kengeza”.

Toba na wongofu wa ndani, ulimwezesha Mtakatifu Francisko wa Assisi kukutana na Kristo Yesu katika hija ya maisha yake. Wote wakitambua kuwa ni ndugu wamoja, hakuna sababu msingi za kujenga chuki, uhasama na hata mauaji kama yalivyotokea kwenye Agano la Kale, Kaini alipomvamia na kumuua ndugu yake Abeli kutokana na wivu usiokua na mvuto wala mashiko. Upendo wa Mungu uwabidiishe watu wote kutambuana kuwa ni ndugu wamoja licha ya tofauti zao msingi. Udugu uwe ni chachu ya upendo na mshikamano; haki, amani na maridhiano; tayari kuthaminiana, kuheshimiana na kuhudumiana kwa hali na mali. Katika muktadha huu, mchakato wa uinjilishaji mpya unachukua mkondo wake na kuwa ni ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Huu ni uinjilishaji unaowachangamotisha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusimama kidete kulinda, kutetea na kutunza mazingira nyumba ya wote. Udugu wa kibinadamu usaidie kuvunjilia mbali kuta za utengano, ubinafsi na choyo kwa kutambua kwamba, leo hii, ulimwengu una kiu ya udugu wa kweli unaopata chimbuko lake kwa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu ni Baba wa wote. Ushuhuda wa Mtakatifu Francisko wa Assisi unaotaka watu wote wajisikie kuwa ni ndugu wamoja uwahamasishe waamini na watu wote wenye mapenzi mema kutembea katika njia ya udugu!

Fratelli Tutti

 

02 October 2020, 14:58