Tafuta

Siku ya 94 ya Kimisionari Ulimwenguni kwa Mwaka 2020 inaongozwa na Kauli mbiu "Mimi hapa, nitume mimi" Is 6:8 Siku ya 94 ya Kimisionari Ulimwenguni kwa Mwaka 2020 inaongozwa na Kauli mbiu "Mimi hapa, nitume mimi" Is 6:8 

Ujumbe wa Papa Francisko Kwa Siku ya Kimisionari Ulimwenguni 2020

Nimtume nani? Ni mwaliko kutoka kwenye moyo wa huruma wa Mwenyezi Mungu unaotoa changamoto kwa Mama Kanisa na wanadamu katika ujumla wao, kusimama kidete ili kupambana na janga la Virusi, COVID-19, kwa kutambua kwamba, binadamu wote wanasafiri katika boti moja, wanahitajiana, wanakamilishana na kufarijiana. Wito wa umisionari ni kwa waamini wote!

Na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Dar Es Salaam.

Kaulimbiu “Mimi hapa, nitume mimi” (Is 6:8). Wapendwa kaka na dada zangu, Napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa Mungu kwa moyo wa kujituma kwa Kanisa lote la ulimwengu kwa kufanikisha Maadhimisho ya Mwezi maalum/pekee wa Kimisionari wa Oktoba 2019. Ninatumaini kwamba hii imehamasisha wongofu wa kimisionari katika jumuiya nyingi kwa kufuata njia iliyoongozwa na kaulimbiu: “Umebatizwa na Umetumwa kutangaza Injili: Kanisa la Kristo katika Utume ulimwenguni kote”. Katika mwaka huu uliokumbwa na mateso na changamoto zilizosababishwa na janga la “maradhi ya virusi vya Corona, COVID-19”, safari ya umisionari wa Kanisa lote inaendelea katika mwanga wa maneno yaliyomo katika wito wa Nabii Isaya: “Mimi hapa, nitume mimi” (6:8). Hili linaonekana ni jibu jipya kwenye swali la Bwana: “Nimtume nani?” (hapo juu). Mwaliko huu kutoka kwenye moyo wa huruma wa Mungu unatoa changamoto kwa Kanisa na wanadamu kwa ujumla hasa katika janga la sasa hivi linaloikabili dunia nzima. “Kama vile Mitume kwenye Injili tumeshtukizwa na dhoruba kali ambayo hatukuitarajia.

Tumegundua sasa kumbe sisi sote tuko katika boti moja, wadhaifu na tusiokuwa na mpango, lakini wakati huo huo sisi ni muhimu na bado tunahitajika, hivyo tushikamane kulisukuma boti tukiwa na nia ya kufarijiana. Katika boti hii.  sote tupo hapa. Kama ilivyokuwa kwa wale mitume, ambao kwa hofu walisema kwa sauti moja, ‘Tunaangamia’ (mstari 38), hivyo basi tumetambua kuwa tusiendelee kujifikiria wenyewe tu, bali tukishirikiana tutafanikiwa. (Tafakari katika Uwanja wa Kanisa kuu la  Mtakatifu Petro mjini Vatican, 27 Machi, 2020). Hakika tumetishika, tumekuwa tusiokuwa na mpango na tunaogopa. Maumivu na kifo mara nyingi hutufanya tujisikie binadamu wadhaifu kabisa, lakini wakati huo huo hutukumbusha dhamira yetu ya dhati ya kuwa na uhai na kuokolewa kutoka maovuni. Hivyo katika hali hii, wito wetu wa umisionari na mwito wa kujitoa kwa ajili ya mapenzi kwa Mungu na jirani, hutupa nafasi nzuri ya kushiriki katika kutoa huduma na kujumuika katika sala ya pamoja. Umisionari wetu ambao Mungu amemkabidhi kila mmoja wetu hutuondolea woga na hali ya ubinafsi hivyo kutuwezesha kujitambua kweli tunajituma kwa ajili ya wenzetu.

Katika sadaka pale Msalabani ambapo hasa utume wa Yesu ulikamilika (Rejea,Yn 19: 28-30), Mungu anatuonesha kwamba upendo wake ni kwa ajili ya kila mmoja wetu (Rejea,Yn 19: 26-27). Anatuagiza kila mmoja wetu awe tayari kutumwa, kwa sababu Yeye mwenyewe ni upendo. Upendo ambao daima uko kwenye umisionari, umeenea ilikutupa uhai. Kutokana na upendo wake kwetu, Mungu Baba alimtuma Mwanae Yesu (RejeaYn 3: 16). Yesu ndiye mmisionari wa Baba: kwani maisha na utume wake umeweka wazi hali ya utiifu wake kwa utashi wa Baba (RejeaYn 4:34; 6:38; 8:12-30; Ebr 10:5-10). Yesu aliyesulibiwa na akafufuka kwa ajili yetu anatuvute kwenye umisionari wa upendo na kwa Roho yake ambayo inatia uhai kwa Kanisa, anatufanya sisi kuwa wafuasi wake na anatutuma tukatangaze umisionari wake duniani kote na kwa watu wote.

“Umisionari, ‘Kanisa katika kwenda mbele” huo si mpango wa ujasiriamali ambao unafanywa kwa nguvu za utashi tu. Ni Kristo mwenyewe anayeliwezesha Kanisa kwenda nje kwa utume. Katika utume wa Uinjilishaji, unasonga mbele kwa sababu Roho Mtakatifu anakusukuma na kukubeba”. (Pasipo yeye hatuwezi kufanya lolote: Kuwa mmisionari katika ulimwengu wa sasa (Rejea katika kitabu cha Una conversazione   con Gianni Valente, Libreria Editrice Vaticana: San Paolo, 2019, 16-17). Mungu siku zote, hutupenda akiwa wa kwanza na kwa upendo wake huu, anakuja kwetu na kutuita. Wito wetu binafsi unatokana na ukweli kwamba ni wana wa Mungu katika Kanisa, familia yake, ndugu zake wa kiume na Mtakatifu katika ujenzi wa Kanisa? Je tuko tayari, kama Bikira Maria Mama wa Yesu, kutoa huduma kikamilifu kadiri ya mapenzi ya Mungu (Rejea   Lk 1:38)? Uwazi huu wa kutoka moyoni ni muhimu kama kweli tunataka kumwambia Mungu: “Nipo hapa, Bwana nitume mimi” (Rejea; Is 6:8). Na hii sio kinadharia, bali katika sura halisia ya maisha ya Kanisa na ya historia.

Tukitambua Mungu anatuambia nini wakati huu wa janga la maradhi yatokanayo na virusi vya Corona, COVID-19 tunapata pia changamoto katika kutekeleza majukumu ya umisionari wetu kwa ajili ya Kanisa. Maradhi, mateso, hofu na kutengwa na jamii pia ni changamoto kwetu. Umaskini wa wale wanaoachwa kufa bila msaada wowote, wanaokimbiwa na ndugu zao, wale waliopoteza kazi pamoja na mapato, wasiokuwa na makazi na wale ambao hawana njia ya kupata chakula, yote ni changamoto kwetu.   Pia kulazimika kukwepa msongamano wa watu na kutii amri ya kujifungia ndani, hutupa nafasi ya kutambua  umuhimu  wa  kuendeleza  uhusiano  wa kijamii na uhusiano wa kuwa karibu na Mungu. Mbali na kuzidi kwa imani ya kutojiamini na utepetevu katika Maisha, hali hii ndiyo itufanye sisi tuzidi kuwa waangalifu katika kujenga mahusiano na watu wengine.

Na sala, ambayo kwayo Mungu anagusa na kusisimua mioyo yetu, itufanye tuwe wawazi zaidi na kutambua mahitaji ya ndugu zetu kwa ajili ya heshima na uhuru, pamoja na uwajibikaji wetu katika kuwahudumia viumbe wa Mungu. Kukosa uwezekano wa kujumuika kama Kanisa na kuadhimisha Ekaristi Takatifu, imetulazimu “kuonja joto” ambalo limesababisha jumuiya nyingi za Kikristu zishindwe kuadhimisha Misa kila Dominika. Katika yote, swali la Mungu: “Nimtume nani” limeelekezwa mara nyingine kwetu, tena linasubiri jibu la ukarimu na uhakika: “Mimi hapa, unitume mimi” (Is 6:8). Mungu anaendelea kuwatafuta wale atakaoweza kuwatuma duniani na kwa mataifa yote kuwa mashahidi wa upendo wake, nguvu zake za kuwaokoa kutoka kwenye dimbwi la dhambi na mauti na kuwaondoa katika maovu yote (Rejea, Mt 9:35-38; Lk 10:1-12). Maadhimisho Siku ya Kimisionari Ulimwenguni, pia ni muda muafaka wa kuimarisha jinsi ya kusali, tafakari na matoleo ya sadaka kwa wahitaji, hizi ni njia nyingi za kushiriki kikamilifu katika Utume wa Yesu katika Kanisa lake.

Matoleo yanayokusanywa wakati wamaadhimisho ya Kiliturujia ya Dominika  ya tatu ya mwezi Oktoba yanalenga katika kutegemeza utume wa Uinjilishaji unaoendeshwa kwa jina langu kupitia Mashirika ya Kipapa kwa lengo la kufanikisha mahitaji ya kiroho na kimwili ya watu na Makanisa ulimwenguni kote na wokovu wa watu wote. Tunaomba, Bikira Maria Mbarikiwa sana, Nyota ya Uinjilishaji na Mtuliza wa Wenye Uchungu, mfuasi wa umisionari wa Mwanae Yesu, azidi kutuombea na kutuimarisha.

Imetolewa na Baba Mtakatifu Francisko,

Roma, Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Lateran.

Tarehe 31 Mei 2020. Sherehe ya Pentekoste!

Siku ya Kimisionari 2020
16 October 2020, 15:16