Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko anawataka watu wote wa Mungu kuzingatia itifaki ya mapambano dhidi ya Virusi vya Corona - COVID-19. Baba Mtakatifu Francisko anawataka watu wote wa Mungu kuzingatia itifaki ya mapambano dhidi ya Virusi vya Corona - COVID-19. 

Papa Francisko: Zingatieni Itifaki ya Mapambano Dhidi Ya COVID-19

Dr. Matteo Bruni, Msemaji mkuu wa Vatican amesema, hivi karibuni, Wanajeshi 4 wa Kikosi cha Ulinzi wa Papa kutoka Uswiss wameambukizwa Virusi vya Corona, COVID-19 na kwa sasa wanaishi katika karantini. Upembuzi umefanywa ili kutambua ni watu wangapi ambao wameambukizwa na Virusi vya Corona, COVID-19 kutoka kwa maaskari hao. Papa: Zingatieni itifaki dhidi ya COVID-19.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko kwa kuzingatia itifaki ya mapambano dhidi ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, mara baada ya katekesi yake, Jumatano tarehe 14 Oktoba 2020 hakuzunguka kusalimiana na kuzungumza na mahujaji pamoja na wageni waliokuwa wamehudhuria kwenye Katekesi hii kuhusu Fumbo la Sala: Sala ya Zaburi. Kutokana na kuongezeka kwa maambukizi ya Virusi vya Corona, COVID-19, wananchi wote wa Italia kwa sasa wanalazimika kuvaa barakoa muda wote wanapokuwa nje ya makazi yao na mikusanyiko ya watu imezuiliwa. Baba Mtakatifu kwa kuzingatia busara ya kichungaji, amewaomba mahujaji na wageni waliokuwa wamehudhuria kupokea salam na matashi yake mema, huku wakiendelea kuzingatia umbali wa kijamii unaotakiwa kama sehemu ya utekelezaji wa itifaki dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19.

Hii inatokana na ukweli kwamba, anatembea na kusalimiana na watu, wengi wao wanashindwa kujizuia na hatimaye, kujikuta kwamba, wakiwa wamesongamana ili kusalimiana naye! Hali na mazingira kama haya yanaweza kusababisha maambuzi makubwa ya Virusi vya Corona, COVID-19. Kwa kuzingatia sheria, taratibu na kanuni za afya bora dhidi ya Virusi vya Corona zinazotolewa na Serikali pamoja na wataalam wa afya, kuna uwezekano mkubwa wa kuzuia maambukizi mapya ya Virusi vya Corona, COVID-19.

Wakati huo huo, Dr. Matteo Bruni, Msemaji mkuu wa Vatican amesema, hivi karibuni, Wanajeshi 4 wa Kikosi cha Ulinzi wa Papa kutoka Uswiss wameambukizwa Virusi vya Corona, COVID-19 na kwa sasa wanaishi katika karantini. Upembuzi yakinifu umefanywa ili kutambua ni watu wangapi ambao wameambukizwa na Virusi vya Corona, COVID-19 kutoka kwa maaskari hao. Tangu sasa wanajeshi wote wa Kikosi cha Ulinzi wa Papa watatakiwa kuvaa barakoa wakati wote pamoja na kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa. Kwa sasa kuna jumla ya wagonjwa 7 wa Virusi vya Corona, COVID-19 mjini Vatican na wanaendelea kupatiwa tiba muafaka katika maeneo ya makazi yao!

Papa: Covid-19

 

 

 

 

14 October 2020, 15:12