Tafuta

Papa Francisko tarehe 20 Oktoba 2020 atashiriki Sala ya Kiekumene na Majadiliano ya Kidini kwa ajili ya Kuombea Amani Duniani katika moyo wa Assisi wa mwaka 1986. Papa Francisko tarehe 20 Oktoba 2020 atashiriki Sala ya Kiekumene na Majadiliano ya Kidini kwa ajili ya Kuombea Amani Duniani katika moyo wa Assisi wa mwaka 1986. 

Papa Francisko: Sala Ya Kuombea Amani Kadiri ya Moyo wa Assisi

Baada ya Sala ya Kiekumene, Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 20 Oktoba 2020 ataungana na viongozi wa dini mbali mbali duniani kwenye Uwanja wa Campidoglio kusali kwa ajili ya kuombea amani duniani. Amani inasimikwa katika misingi ya ukweli, haki, upendo na uhuru kamili mambo msingi yanayofafanuliwa katika Waraka wa Kitume wa “Pacem in terris” yaani “Amani Duniani”.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko Jumanne tarehe 20 Oktoba 2020 majira ya Alasiri, anatarajia kushiriki katika Sala ya Kuombea Amani Kadiri ya Moyo wa Assisi. Kwa mwaka huu Sala hii inaongozwa na kauli mbiu “Hakuna anayejiokoa mwenyewe: Amani na Udugu”. Hii ni sala ambayo imeandaliwa na Jumuiya ya Mtakatifu Egidio, itakayowashirikisha waamini wa Madhehebu mbali mbali ya Kikristo na hivyo kuadhimishwa kwenye Kanisa kuu la “Santa Maria in Aracoeli” lililoko karibu sana na Makao makuu ya Jiji la Roma. Baada ya Sala ya Kiekumene, Baba Mtakatifu ataungana na viongozi wakuu wa dini mbali mbali duniani kwenye Uwanja wa Campidoglio kusali kwa ajili ya kuombea amani duniani. Amani inasimikwa katika misingi ya ukweli, haki, upendo na uhuru kamili mambo msingi yanayofafanuliwa katika Waraka wa Kitume wa “Pacem in terris” yaani “Amani Duniani”. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanawahimiza Wakristo kwa busara na mapendo, kwa njia ya majadiliano ya kidini, umoja na ushirikiano na waamini wa dini nyingine, kutoa ushuhuda wa imani na wa maisha yao.

Waamini watambue, wahifadhi na kukuza mema ya kiroho, kimaadili, pamoja na tunu msingi za kijamii na za kitamaduni ambazo zinapatikana kutoka kwa waamini wa dini nyingine. Majadiliano ya kidini kati ya waamini wa dini mbali mbali ni nyenzo msingi ya kupambana na tabia ya ubinafsi, misimamo mikali ya kidini na kiimani, ili kujenga na kudumisha umoja, upendo na mshikamano na maridhiano kati ya watu, kila mtu akipewa nafasi ya kushuhudia imani yake! Kumbe, katika mchakato wa majadiliano ya kidini, Wakristo wanapaswa kumuungama Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, chanzo cha imani, furaha na matumaini kwa waja wake. Mwenyezi Mungu ni kiini cha majadiliano na watu wake na kamwe hajaacha kuzungumza na wanadamu katika safari ya maisha yao hapa duniani, kama ilivyokuwa kwenye Agano la Kale hata leo hii, Mwenyezi Mungu anazungumza na binadamu kwa njia ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Kristo ni ufunuo wa huruma na upendo wa Baba wa milele, aliyetumwa kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti.

Mtakatifu Yohane Paulo II tarehe 26 Oktoba 1986, kwa mara ya kwanza katika historia, aliwakutanisha viongozi wa kidini huko mjini Assisi, nchini Italia, kwa ajili ya kusali na kuombea amani duniani! Mkutano huu, ukawa ni chachu ya kuendelea kujikita katika majadiliano ya kidini na kiekumene, ili kudumisha amani duniani. Sala na ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya kila siku ni nyenzo msingi ya ujenzi wa amani duniani. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI, Miaka 25 baadaye, aliwataka waamini wa dini mbali mbali kuendeleza roho na moyo wa sala kutoka Assisi kwa kudumisha majadiliano na upatanisho. Alikazia umuhimu wa vijana kufundwa utamaduni wa haki na amani na kwamba, majadiliano ya kidugu ni muhimu sana katika kukuza haki, amani na mshikamano wa udugu wa kibinadamu.

Kwa upande wake, Baba Mtakatifu Francisko anasema majadiliano ni sehemu ya vinasaba vya maisha ya waamini wa dini mbali mbali duniani. Haya ni majadiliano ambayo yanafumbatwa katika utu na tunu msingi za maisha ya binadamu, ili kujenga na kudumisha leo na kesho iliyo bora zaidi inayosimikwa katika amani ya kweli. Jambo la msingi ni waamini kushiriki katika mchakato wa ujenzi wa utamaduni wa amani kwa njia ya majadiliano katika ukweli, uwazi, haki na usawa! Umoja, udugu wa kibinadamu na usawa ni nyenzo madhubuti dhidi ya vitendo vya kigaidi na misimamo mikali ya kiimani. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, leo hii waamini wa dini mbali mbali wanakabiliwa na changamoto kuu tatu: Mosi, Utambulisho wa dini yao; nani ni Mungu wao na ushuhuda wa maisha mintarafu kile wanachokiamini katika maisha. Pili ni changamoto pia ya kuheshimu watu wenye imani tofauti kwa kutambua kwamba, hawa si adui bali ni wanandani wa hija ya maisha kuelekea katika ukweli. Tatu ni changamoto ya ukweli katika imani wanayoungama na kuishuhudia.

Yote haya yakizingatiwa kama sehemu ya mchakato wa majadiliano ya kidini, hakuna sababu ya vita vya kidini, nyanyaso na dhuluma kwa misingi ya kiimani kama inavyoshuhudiwa kwa sasa sehemu mbali mbali za dunia. Majadiliano ya kidini ni sehemu muhimu sana inayoweza kuwasaidia waamini kufahamu imani yao kwa dhati, ili kuweza kuitangaza na kuishuhudia, vinginevyo hapa ni shughuli pevu kabisa, kwani badala ya amani na utulivu, watu watakuwa na woga, mashaka na wasi wasi usiokuwa na mvuto wala mashiko kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Waamini wasiwe na woga wa kutangaza na kushuhudia imani kwa watu wa Mataifa, huu ni utajiri mkubwa wa maisha ya kiroho.

Papa: Amani
17 October 2020, 15:26