Tafuta

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Washiriki wa Mkataba wa Mfumo Mpya wa Elimu Kimataifa, tarehe 15 Oktoba 2020. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Washiriki wa Mkataba wa Mfumo Mpya wa Elimu Kimataifa, tarehe 15 Oktoba 2020. 

Papa Francisko: Mkataba Wa Mfumo Mpya Wa Elimu Kimataifa 2020

Papa Francisko kuhusu: Janga la elimu, maana, umuhimu wa kupyaisha mfumo wa elimu duniani na hatimaye, mambo msingi yanayopaswa kuzingatiwa katika maboresho ya mfumo wa elimu duniani! Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi, COVID-19 limepelekea athari kubwa katika sekta ya afya, uchumi, jamii na elimu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika kumbukumbu ya Jubilei ya Miaka 50 tangu alipopewa Daraja Takatifu ya Upadre hapo tarehe 13 Desemba 1969 alizindua Mpango mkakati wa mwaka 2020, tukio la kimataifa ambalo lilikuwa limepangwa kuzinduliwa rasmi hapo tarehe 14 Mei 2020, kwa kuongozwa na kauli mbiu “Mabadiliko ya Mfumo wa Elimu Kimataifa”. Kwa sasa tukio hili la kihistoria limeadhimishwa kuanzia tarehe 11-18 Oktoba 2020 na Mkataba wa Mfumo Mpya wa Elimu Kimataifa “Global Compact on Education” umetiwa mkwaju hapo tarehe 15 Oktoba 2020. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa njia ya video kwa washiriki wa mkutano huu kwenye Chuo Kikuu cha Kipapa cha Lateran kilichoko mjini Roma amekazia pamoja na mambo mengine kuhusu: Janga la elimu duniani, maana ya elimu, umuhimu wa kupyaisha mfumo wa elimu duniani na hatimaye, mambo msingi yanayopaswa kuzingatiwa katika maboresho ya mfumo wa elimu duniani! Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi, COVID-19 limepelekea athari kubwa katika sekta ya afya, uchumi, jamii na elimu. Kulihitajika suluhu ya haraka ili wanafunzi waweze kuendelea na masomo yao, huku wakiwa wanaishi kwenye karantini majumbani mwao.

Maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano yamewawezesha wanafunzi wengi kuendelea na masomo, lakini kuna umati mkubwa wa watoto na vijana umebaki nyuma kwa masomo na hili ni janga kubwa katika mfumo wa elimu duniani. Inakadiriwa kwamba, kuna watoto zaidi ya milioni 10 wako hatarini kutoendelea na masomo kutokana na kuyumba kwa uchumi kitaifa na kimataifa. Jambo la kusikitisha zaidi ni kuona kwamba, zaidi ya watoto milioni 250 wenye umri wa kwenda shuleni, hawataweza kupata fursa hii. Changamoto zilizoibuliwa kwenye sekta ya afya zinapaswa kushughulikiwa kikamilifu, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu pamoja na kukazia umuhimu wa kushirikiana na kushikamana katika udugu wa kibinadamu. Elimu maana yake ni mchakato unaowajengea wanafunzi matumaini ya kuondokana na ubinafsi wao; kwa kutambua, kuheshimu na kuthamini tofauti msingi zinazojitokeza, ili hatimaye kujenga na kudumisha: utamaduni wa ukarimu, mshikamano, mafungamano na hofu ya Mungu.

Upyaisho wa mfumo wa elimu katika ulimwengu mamboleo utawasaidia watu wa Mungu kupambana na changamoto zinazojitokeza kwa wakati huu, ili kujenga leo na kesho yenye matumaini. Elimu ni upendo unaowajibisha na kurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine, ili kuondokana na ubinafsi unaopelekea watu kutokuthaminiana. Kuna haja ya kujenga umoja na mshikamano unaosimikwa katika kipaji cha kusikiliza, kujadiliana na maelewano. Mabadiliko ya mfumo wa elimu duniani yanapaswa kuwahusisha wadau mbali mbali katika sekta ya elimu, ili kuondokana na ukosefu wa haki jamii; kwa kukazia utu, heshima na haki msingi za binadamu, ili hatimaye, kuweza kupambana na umaskini pamoja na tabia ya watu kutowajali wengine. Baba Mtakatifu anasema, huu ni mchakato fungamanishi unaopania kujenga madaraja yanayowakutanisha watu, ili kuondokana na upweke hasi, kwa kuwajengea vijana wa kizazi kipya matumaini. Hali hii itawasaidia vijana wengi kuondokana na ugonjwa wa sonona; utumwa mamboleo, chuki, uhasama, matusi, ukatili pamoja na uonevu mitandaoni.

Ni nafasi ya kupambana na unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya watoto wadogo; kwa kuwaokoa watoto wanaopelekwa mstari wa mbele kama askari au kuuzwa katika mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo. Vitendo vyote hivi ni udhalilishaji wa utu, heshima na haki msingi za binadamu; na ni mambo kama haya ambayo pia yamepelekea uchafuzi mkubwa mazingira nyumba ya wote pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi. Katika historia ya maisha ya mwanadamu, kuna wakati wa kufanya maamuzi magumu yatakayoacha chapa ya kudumu. Janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 ni changamoto inayohitaji mabadiliko makubwa ya mfumo wa elimu kimataifa, kwa kuwashirikisha vijana, familia, jamii, shule, taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu; dini, serikali na walimwengu katika ujumla wao, ili kuwafunda watu waliokomaa barabara. Mkazo zaidi unawekwa katika mchakato wa elimu unaopambana na ujinga ili kuboresha tamaduni za watu. Ili kuweza kufikia lengo hili anasema Baba Mtakatifu Francisko kuna haja ya kujenga utamaduni fungamanishi, shirikishi na wenye mwono mpana zaidi.

Watu wawe na ujasiri wa kushinda kinzani binafsi ili kuimarisha mafungamano ya kijamii, ili watu wote waweze kuzungumza lugha moja ya udugu wa kibinadamu. Ubora wa elimu unapimwa kwa kuangalia thamani yake katika maisha na uwezo wa kuanzisha utamaduni mpya unaowashirikisha watu wengi zaidi. Baba Mtakatifu anapenda kutoa wito kwa watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia, kutoka katika sekta ya utamaduni, sayansi, sanaa na michezo na wafanyakazi katika sekta ya mawasiliano ya jamii kushiriki katika Mkataba wa Mfumo Mpya wa Elimu Kimataifa “Global Compact on Education” kwa njia ya ushuhuda na kazi zao. Wasaidie kuhamasisha tunu msingi za utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, haki na amani; uzuri, wema, ukarimu na udugu wa kibinadamu. Kila mtu ajitahidi kuwajibika, ili kuendeleza mchakato wa mageuzi; ili kuganga na kuponya ulimwengu huu ambao umejeruhiwa vibaya; kila mmoja, akijitahidi kuwa ni Msamaria mwema, anayeguswa na mahangaiko ya wengine, badala ya kuchochea chuki na uhasama kati ya jamii. Huu ni mfumo wa elimu wenye mwono mpana na wenye uwezo wa kuwashirikisha wote ili kutoa majibu yatakayosaidia kujenga mafungamano ya kijamii kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ulimwengu mamboleo unawahitaji watu watakaojenga na kudumisha amani na utulivu.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, ni katika muktadha huu, kila mtu binafsi, anawajibika kutoa kipaumbele cha kwanza katika mchakato wa mfumo mpya wa elimu: utu na heshima ya binadamu, ili hatimaye, kila mtu aweze kuonesha: uzuri na upekee wake; uwezo wa kuhusiana na kufungamana na wengine katika hali na mazingira yanayowazunguka, ili kuondokana na utamaduni wa chuki na uhasama ambao kimsingi umepitwa na wakati. Huu ni muda wa kusikiliza na kujibu kilio cha watoto na vijana wanaorithishwa tunu msingi, uelewa na ufahamu, ili kwa pamoja waweze kujenga leo na kesho inayosimikwa katika haki, amani na maisha bora zaidi. Huu ni mwaliko wa kuhakikisha kwamba, watoto na vijana wengi zaidi wanashiriki katika mchakato wa elimu bora. Katika hali na mazingira kama haya, familia zinapaswa kuwa ni sehemu ya wadau wakuu katika sekta ya elimu. Watu wajifunze na kuwafunza wengine ukarimu, kwa kutoa msaada zaidi kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Jamii inapaswa kuendelea kujifunza ili kupata mifumo mipya ya kiuchumi na kisiasa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na huduma bora kwa familia nzima ya binadamu pamoja na kudumisha ekolojia fungamani. Jamii ijitahidi kutumia na kulinda vyema zaidi mazingira nyumba ya wote, bila kukwapua rasilimali ya dunia; kwa kubadili mtindo wa maisha, ili kutunza mazingira kwa kuzingatia kanuni ya auni na mshikamano unaowazunguka na kuwaambata wote. Baba Mtakatifu anawaambia washiriki wa mkutano huu kwamba, lengo kuu ni kuanzisha Mkataba wa Mfumo Mpya wa Elimu Kimataifa “Global Compact on Education” utakaotekelezwa kwenye nchi mbali mbali, kwa kuwekeza nguvu zaidi na vipaji ili kuanzisha mchakato wa ushirikiano na vyama vya kiraia ili kuleta mageuzi. Mafundisho Jamii ya Kanisa kadiri ya Ufunuo wa utu mpya ndani ya Kristo Yesu unaiwezesha jamii kujenga msingi thabiti pamoja na kuwa na rejea makini zinazonesha dira na mwongozo wa kufuata wakati wa dharura. Uwekezaji huu unafumbatwa kwa namna ya pekee kabisa katika mafungamano ya udugu wa kibinadamu, ambayo ni wazi, ili kuhakikisha kwamba watoto na vijana wanapata elimu bora kadiri ya utu na heshima ya binadamu, ili kutekeleza wito wake wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu.

Ni wakati wa kuangalia ya mbeleni kwa ujasiri na matumaini, haki na amani. Haya anasema Baba Mtakatifu Francisko ni matumaini ya uzuri, wema, amani na utulivu ndani ya jamii. Hii ni changamoto ya kuhakikisha kwamba, mjenzi mkuu wa amani anahusishwa kikamilifu, kila mtu kadiri ya nafasi na uwezo wake, bila kumtenga mtu awaye yote. Wote kwa pamoja washikamane na kusonga mbele, ili kujenga utamaduni unaosimikwa katika amani na utulivu; umoja na udugu ili hatimaye, kuondokana na utamaduni usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine!

Mkataba wa Elimu
15 October 2020, 15:37