Tafuta

Papa Francisko Papa Francisko 

Papa Francisko:mamlaka ya kweli ni kuhudumia si kunyonya wengine!

Wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana,Dominika tarehe 4 Oktoba 2020 katika siku kuu ya Mtakatifu Francis wa Assisi,umetangazwa Waraka Mpya wa “Fratelli tutti”,Papa Francisko ameshauri kufanya kazi kwa ajili ya kutangaza Injili.Ni mbaya sana kuona ndani ya Kanisa wapo wenye mamlaka wanaotafuta mafao yao binafsi.

Na Sr. Angela Rwezaula-Vatican.

Katika Injili ya siku ya leo (Mt 21,33-43) Yesu akiwa tayari anaona mateso na kifo chake anasimulia kisa cha wakulima wauaji ili kuwaonya wakuu wa makuhani na wazee wa watu ambao wanataka kuchukua njia mbaya. Hawa kiukweli wanazidi kukuza nia za ukatili dhidi yake na watafuta namna ya kumwondoa kabisa. Ndiyo Mwanzo wa tafakari ya Papa Francisko kabla ya sala ya Malaika wa Bwana kwa waamini na mahujaji waliokusanyika katika uwanja wa Mtakatifu Petro Vatican tarehe 4 Oktoba 2020 kusali sala ya Malaika wa Bwana.  Papa Francisko akiendelea amesema simulizi hiyo inaonesha mwenye shamba ambaye baada ya kulitunza vema shamba lake la mizabibu alikuwa asafiri na akawakabidhi wakulima. Baadaye wakati wa matunda ulipokaribia aliwatuma watumwa wake ili apokee matunda; lakini wale wakulima wakawakamata na kuwapiga viboko na baadhi hata kuwaua. Mwishowe akatuma idadi kubwa ya watumwa kuliko ya kwanza, lakini wale wakatendea yale yale. (Mt 21, 34-36). Cha kushangaza Papa Francisko ameongeza ni pale ambapo mwenye shamba anaamua kumtuma mwanaye. Wakulima lakini hakuwaheshimu na zaidi walifikiria wakimwondoa basi wataweze kurithi shamba hilo na hivyo wakaamua kumuua hata yeye (Mt 21, 37-39).

Picha ya shamba hili iko wazi, kwani inawakilisha watu ambao Bwana aliwachagua na kuwaumba kwa uangalifu mkubwa. Watumwa waliotumwa na Bwana wa shamba ni manabii waliotumwa na Mungu, wakati mwana, ni sura ya Yesu mwenyewe. Kama walivyokataliwa manabi ndivyo hivyo hata Kristo alivyokataliwa na kuuwawa, Papa amesisitza. Mwisho wa simulizi, Yesu anauliza swali wakuu wa watu "Atakapokuja yule bwana wa shamba la mizabibu atawatendea nini wale wakulima? (Mt 21,40). Hata bila kufikiia kwa kufuata mantiki ya simuliza wakataja hukumu yao wenyewe kwamba “Bwana atawaangamiza vibaya sana wale wakulima na shamba la mizabibu atawakabidhi wakulima wengine watakaomlipa matunda kwa wakati wake” (Mt 21,41).

Katika msemo huu mgumu sana, Papa amesisitiza, Yesu anaweka mbele ya watesi wake uwajibikaji na anafanya hivyo kwa uwazi kabisa. Lakini tusifikiri kuwa ushauri huo ni kwa ajili ya wale waliokuwa wanamkataa Yesu kwa wakati ule. Hii ni sawa na kila wakati hata kwa kwa enzi zetu. Hata leo hii Mungu anasubiri matunda ya shamba lake la mizabibu kutoka kwa  wale ambao aliwakabidhi kufanya kazi ndani mwake. Sisi sote”. “Katika kila enzi, wale ambao wana mamlaka, yaani mamlaka yoyote, hata katika Kanisa, kwa watu wa Mungu, wanaweza kujaribiwa kufanya masilahi yao wenyewe, badala ya yale ya Mungu mwenyewe. Na Yesu anasema kuwa, mamlaka ya kweli ni wakati mtu anapotoa huduma, ni katika kutumikia, na sio kunyonya wengine. Shamba la mizabibu ni la Bwana, sio letu. Mamlaka ni huduma na kwa njia hiyo  inapaswa kutekelezwa kwa faida ya wote na kwa kueneza Injili. Ni mbaya kuona wakati watu wenye mamlaka katika Kanisa wanatafuta masilahi yao”, Papa Francisko amefafanua.

Papa Francisko akiendelea amesema katika somo la Pili la liturujia ya siku Mtakatifu Paulo anatulezea namna ya kuwa mfanyakazi bora katika shamba la Bwana. Mambo yote yoyote ya kweli, yoyote yaliyo ya staha ,yaliyo ya haki yaliyo safi na yenye kupendeza, yenye sifa nzuri yatafakarini. Hizo ndizo  jitihada zetu ya kila siku (Fil 4,8). Papa amerudia kukazia hayo na kwamba ndiyo tabia ya kuwa na mamlaka  hata ya kila mmoja wetu kwa sababu kila mmoja wetu katika udogo wake anayo mamlaka kwa kiasi fulani. Tutakuwa namna hii Kanisa moja ambalo daima ni tajiri la matunda ya utakatifu. Tutatoa sifa ya utukufu kwa Baba anayetupenda kwa upendo upeo wa mwanaye ambaye anaendelea kutupatia wokovu, kwa Roho Mtakatifu anayetufungulia moyo na kutusukuma kuelekea ukamilifu wa wema. Kwa kuhitimisha Papa Francisko ameomba kuelekeza kwa Mama Maria Mtakatifu kiroho, kwa kuungana na waamini waliounganisha Katika madhabahu ya Mama Maria wa Pompei kwa ajili ya sala na katika mwezi wa Oktoba kupyaisha jitihada za kusali Rosari Takatifu.

04 October 2020, 15:28