Tafuta

Papa Francisko: Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 15 Oktoba linaadhimisha Kumbukumbu ya Mtakatifu Theresa wa Yesu, Bikira na Mwalimu wa Kanisa. Papa Francisko: Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 15 Oktoba linaadhimisha Kumbukumbu ya Mtakatifu Theresa wa Yesu, Bikira na Mwalimu wa Kanisa. 

Papa Francisko: Mtakatifu Theresa wa Yesu Mwalimu wa Kanisa: Sala!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Mtakatifu Theresa wa Yesu ni mwalimu wa maisha ya kiroho, aliyebahatika kuwafundisha watu namna nzuri zaidi ya kusali, kwa kujenga mahusiano na mafungamano ya ndani na Mwenyezi Mungu. Mara nyingi alijitenga na kujipatia muda binafsi wa kukaa mbele ya Mwenyezi Mungu, wakazungumzana kama watu wapendanao katika maisha.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko baada ya Katekesi yake kuhusu Fumbo la Sala: Sala ya Zaburi, Jumatano tarehe 14 Oktoba 2020 ametumia fursa hii kutoa salam na matashi mema kwa wamonaki wa Shirika la Watrappisti “Order of Cistercians of the Strict Observance; Kwa Kilatin: Ordo Cisterciensis Strictioris Observantiae, OCSO) lililoanzishwa na Abate Armand Jean Le Bouthillier de Rancé kutoka nchini Ufaransa kunako mwaka 1664 ili kuleta mageuzi makubwa katika maisha na utume wa Kanisa. Wamonaki hawa kutoka Vitorchiano, Italia kwa sasa wanajiandaa kwenda nchini Ureno ili kufungua monasteri mpya. Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuombea miito mitakatifu, ili Bwana wa mavuno aweze kutuma watenda kazi wema, watakatifu na wachapakazi. Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza Wamonaki hawa ambao kwa sasa wanaonekana kuwa na idadi kubwa ya miito ya kitawa!

Baba Mtakatifu Kwa wanajeshi wa NATO kutoka katika kambi ya Cecchignola, mjini Roma, amewataka waendelee kujiaminisha chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Malkia wa amani. Waendelee kusimamia ustawi, mafao na maendeleo ya wengi na kwamba, Roho Mtakatifu atende kazi ndani mwao, ili hatimaye, waweze kuwa kweli ni vyombo, wajenzi na mashuhuda wa Injili ya amani duniani! Baba Mtakatifu amewataka wazee, vijana, wagonjwa na wanandoa wapya kukuza na kudumisha ndani mwao hekima na tunu msingi za Kiinjili, kwa kusikiliza, kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha yao. Walishwe na kurutubishwa na Neno la Mungu pamoja na Ekaristi Takatifu, chakula cha kiroho, tayari kutangaza na kushuhudia Ukweli. Ili waamini waweze kutambua mapenzi ya Mungu katika maisha yao, hawana budi kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano ya dhati kabisa na Mwenyezi Mungu katika sala.

Kwa njia hii, wataweza kugundua ndani mwao kwamba, kwa hakika Mwenyezi Mungu ni mwingi wa huruma, mapendo na msamaha, anayewalinda na kuwatunza daima. Mwenyezi Mungu mwenyewe awajaze neema na baraka zake za daima! Amewashukuru na kuwapongeza waamini kutoka Poland walioadhimisha Jumapili tarehe 11 Oktoba 2020 Siku ya Papa Kitaifa, kama mwendelezo wa kumbukumbu hai ya Mtakatifu Yohane Paulo II. Hii ni siku ambayo Kanisa nchini Poland limeitenga maalum kwa ajili ya kumkumbuka na kumwombea Khalifa wa Mtakatifu Petro. Baba Mtakatifu Francisko anawashukuru kwa mchango wao wa hali na mali katika maisha na utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Wote hawa amewaweka chini ya ulinzi na maombezi ya Mtakatifu Yohane Paulo II.

Tarehe 15 Oktoba 2020 Mama Kanisa anaadhimisha Kumbukumbu ya Mtakatifu Theresa wa Yesu, au maarufu kama Mtakatifu Theresa wa Avila, Bikira na Mwalimu wa Kanisa. Mwanzoni kabisa alijulikana kama “Teresa de Cepeda y Ahumada” aliyezaliwa tarehe 28 Machi 1515 mjini Avila, nchini Hispania. Muasisi wa Shirika la Wakarmeli. Alifariki dunia tarehe 4 Oktoba 1582. Akatangazwa kuwa ni Mwalimu wa Kanisa na Mtakatifu Paulo VI kunako mwaka 1970. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Mtakatifu Theresa wa Yesu ni mwalimu wa maisha ya kiroho, aliyebahatika kuwafundisha watu namna nzuri zaidi ya kusali, kwa kujenga mahusiano na mafungamano ya ndani na Mwenyezi Mungu. Mara nyingi alijitenga na kujipatia muda binafsi wa kukaa mbele ya Mwenyezi Mungu, wakazungumzana kama watu wapendanao katika maisha. Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kujifunza namna bora zaidi ya kusali, kwa kujenga na kudumisha urafiki na mafungamano mema na Mwenyezi Mungu na kwamba, maneno ya kuzungumza na Mungu yanapatikana katika Kitabu cha Sala ya Zaburi.

Miito Mitakatifu
14 October 2020, 14:33