Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika watoto kutoka sehemu mbali mbali za dunia kuungana pamoja tarehe 18 Oktoba 2020 ili kusali Rozari Takatifu, kwa kuwakumbuka na kuwaombea waathirika wa COVID-19. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika watoto kutoka sehemu mbali mbali za dunia kuungana pamoja tarehe 18 Oktoba 2020 ili kusali Rozari Takatifu, kwa kuwakumbuka na kuwaombea waathirika wa COVID-19. 

Papa: Jumapili 18 Oktoba 2020: Siku ya Watoto Kusali Rozari

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika watoto kushiriki kusali Rozari kwa ajili ya kuombea: umoja na mshikamano; amani na maridhiano kati ya watu. Lakini kwa namna ya pekee kabisa, itakuwa ni fursa kwa watoto kuwakumbuka na kuwaombea wale wote walioathirika kutokana na janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Mshikamano katika Sala!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Shirika la Kipapa kwa Ajili ya Makanisa Hitaji, ACN., katika maadhimisho ya Siku ya 94 ya Kimisionari Ulimwenguni, hapo tarehe 18 Oktoba 2020 kwa kuongozwa na kauli mbiu: “Mimi hapa, nitume mimi” Isa. 6:8., linawaalika watoto zaidi ya milioni moja kutoka sehemu mbali mbali za dunia kushiriki katika kusali Rozari Takatifu. Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 11 Oktoba 2020, ametumia fursa hii pia kuwaalika watoto kushiriki kikamilifu katika tukio hili, kwa ajili ya kuombea: umoja na mshikamano; amani na maridhiano kati ya watu. Lakini kwa namna ya pekee kabisa, itakuwa ni fursa kwa watoto kuwakumbuka na kuwaombea wale wote walioathirika kutokana na janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19.

Kardinali Mauro Piacenza, Rais wa Shirika la Kipapa kwa Ajili ya Makanisa Hitaji, ACN, anasema, janga la Virusi vya Corona, COVID-19 linaendelea kusababisha madhara makubwa kwa watu: kijamii na kiuchumi; kiroho na kiutu. Kumbe, kuna haja ya kushirikiana na kushikamana kama ndugu wamoja, kwa kutambua kwamba, msaada mkubwa zaidi ni kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Ibada kwa Rozari Takatifu iwe ni msaada mkubwa unaoendelea kupyaisha ujasiri, imani na matumaini; ulinzi na tunza kutoka kwa Bikira Maria, Afya ya Wagonjwa. Kwa mara ya kwanza kampeni na mwaliko kwa watoto kusali Rozari Takatifu kwa pamoja, ilikuwa ni mwaka 2005, huko Carcas, nchini Venezuela. Watoto wanasali Rozari Takatifu kwa ajili ya toba, wongofu wa ndani, amani na maridhiano kati ya watu! Tangu mwaka 2008, tukio hili limekuwa likiadhimishwa kimataifa na kwa mwaka 2020, zaidi ya mataifa 80 yanashiriki katika kampeni hii!

Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wa Kitume “Gaudete et exsultate” yaani “Furahini na kushangilia, wito wa utakatifu katika ulimwengu mamboleo” anamwangalia Bikira Maria aliyemwilisha Heri za Mlimani kuliko mtakatifu yoyote yule. Ni mwanamke aliyefurahia uwepo wa Mungu katika maisha yake na kuhifadhi yote katika sakafu ya moyo wake! Bikira Maria ni Mtakatifu kuliko watakatifu wote. Ni kimbilio la waamini katika ulinzi na tunza ya kimama. Anawafundisha na kuwasindikiza waamini katika utakatifu wa maisha; anawalinda bila kuwahukumu; anawafariji, kuwaombea na kuwatakatifuza kwa uwepo wake mwanana, changamoto na mwaliko kwa waamini kumkimbilia katika sala, lakini zaidi kwa njia ya tafakari ya Rozari Takatifu.

Baba Mtakatifu anasema, Rozari Takatifu ni muhtasari wa huruma ya Mungu katika maisha ya mwanadamu! Ni njia muafaka kabisa ya kutafakari maisha na utume wa Kristo Yesu, ili kumfahamu, kumpenda, kumfuasa na kumtumikia kwa njia ya upendo kwa jirani wenye shida na mahangaiko mbali mbali wanaokumbukwa katika Sala ya Rozari Takatifu. Ibada ya Rozari takatifu ni muhtasari wa Injili, unaowasaidia waamini kwa njia ya Bikira Maria Mama wa Kanisa, kumfahamu zaidi Yesu Kristo, Mkombozi wa ulimwengu.

Kampeni ya Rozari
12 October 2020, 14:45