Tafuta

Papa Francisko akutana na kuzungumza na Wanajeshi wapya 38 wa kikosi cha Ulinzi wa Papa. Tarehe 4 Oktoba 2020 wanakula kiapo cha utii na uaminifu kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Papa Francisko akutana na kuzungumza na Wanajeshi wapya 38 wa kikosi cha Ulinzi wa Papa. Tarehe 4 Oktoba 2020 wanakula kiapo cha utii na uaminifu kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro. 

Papa Akutana na Wanajeshi Wapya 38: Kula Kiapo 4 Oktoba 2020

Papa Francisko amewashukuru wazazi kwa kuwarithisha watoto wao imani na maana ya huduma ya ukarimu kwa jirani. Papa amewakumbuka na kuwaombea wale Askari 147 waliojisadaka kwa ajili ya ulinzi wa Papa Clementi VII. Tukio kama hili linaweza kuamsha ndani mwao “uporaji wa maisha ya kiroho”, unaowafanya vijana kuhatarisha maisha yao kwa kutamani na kupenda mno vitu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kikosi cha Walinzi wa Papa kutoka Uswiss, maarufu kama “Swiss guards” kina dhamana na utume unaojikita katika wito, uaminifu, umakini na sadaka inayotekelezwa kwa moyo wa unyenyekevu bila hata ya kujibakiza. Jumapili tarehe 4 Oktoba 2020 wanajeshi wapya 38 wa Kikosi cha Ulinzi wa Papa kutoka Uswiss watakula kiapo cha utii na uaminifu kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro pamoja na waandamizi wake. Hii ni siku ambayo wanawakumbuka askari wenzao 147 kutoka Uswiss walioyamimina maisha yao mjini Roma kwa ajili ya kumtetea Papa Clemente VII kunako mwaka 1527. Maadhimisho ya Mwaka 2020 yatawahusisha wazazi, ndugu na jamaa wa karibu sana wa Askari hawa wapya.

Ijumaa tarehe 2 Oktoba 2020, Baba Mtakatifu Francisko amekutana na kuzungumza na Askari wapya wa Kikosi cha Walinzi wa Papa kutoka Uswiss, ambao wameamua kutumia muda wao wa ujana kwa ajili ya huduma kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake amewashukuru wazazi na walezi kwa kuwarithisha watoto wao imani ya Kikristo na maana ya huduma ya ukarimu kwa jirani. Baba Mtakatifu amewakumbuka na kuwaombea wale Askari 147 waliojisadaka kwa ajili ya ulinzi wa Papa Clementi VII. Tukio kama hili linaweza kuamsha ndani mwao “uporaji wa maisha ya kiroho”, unaowafanya vijana wa kizazi kipya kuhatarisha maisha yao mintarafu mwono wa kijamii, kwa kupenda na kutamani vitu.

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, uwepo wao mjini Roma utakuwa ni fursa ya kuweza kutumia vyema amana na utajiri unaopatikana mjini humu, ili kuboresha na kuimarisha utajiri wao wa kitamaduni, lugha na maisha ya kiroho. Hiki ni kipindi maalum katika maisha yao, kinachowataka waishi katika moyo wa udugu wa kibinadamu, kwa kusaidiana kwa hali na mali kama kielelezo cha ushuhuda wa furaha ya Injili. Kiapo cha utii kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro na waandamizi wake wote ni ushuhuda wa imani na wito wao unaopata chimbuko lake katika Sakramenti ya Ubatizo, yaani kutoka kwa Kristo Yesu mwenyewe.

Kumbe, Askari hawa wanaitwa kuwa watu kamili na wafuasi wa Kristo Yesu na wadau katika mapambano ya maisha yao ya kila siku. Askari hawa wawe tayari kupambana na vizingiti na changamoto mbali mbali za maisha, daima wakitegemea msaada wa Roho Mtakatifu. Daima wakumbuke kwamba, Kristo Yesu anaambatana nayo hatua kwa hatua katika maisha yao kwa uwepo wake unaowashauri na kuwafariji. Baba Mtakatifu ametumia muda huu kukishukuru na kukipongeza Kikosi cha Walinzi wa Papa kutoka Uswiss, si tu kwa kile wanachotenda, bali kwa jinsi wanavyotekeleza dhamana na wajibu wao kwa umakini mkubwa unaokita mizizi yake katika upendo. Mama Theresa wa Calcutta anasema, Siku ya mwisho, watu watahukumiwa si kwa yale yote waliotenda katika maisha, bali kwa upendo kiasi gani waliweza kuuzamisha katika shughuli zao za kila siku. Baba Mtakatifu amewahakikishia wote sala na sadaka yake na kuwaambia pia waendelee kumkumbuka kwa sala na sadaka zao katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Papa: Kiapo
02 October 2020, 15:57