Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko anasema, waamini walei wanapaswa kupewa nafasi kubwa zaidi katika maisha na utume wa Kanisa kwa kushiriki kikamilifu katika maamuzi mbali mbali. Baba Mtakatifu Francisko anasema, waamini walei wanapaswa kupewa nafasi kubwa zaidi katika maisha na utume wa Kanisa kwa kushiriki kikamilifu katika maamuzi mbali mbali.  

Nia za Baba Mtakatifu Mwezi Oktoba 2020: Wanawake Katika Maisha Na Utume Wa Kanisa

Baba Mtakatifu Francisko katika nia zake za kimisionari kwa Mwezi Oktoba 2020 anaendelea kukazia umuhimu wa wanawake kushiriki katika maisha na utume wa Kanisa bila kutumbukia katika mwono tenge wa karama za waamini walei, tayari kupyaisha Uso wa Mama Kanisa! Wanawake wanapaswa kushirikishwa katika vikao kwa ajili ya maamuzi ya maisha na utume wa Kanisa! Walei!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanakazia umuhimu wa wito na utume wa waamini walei unaopata chimbuko lake kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Waamini walei wanashirikishwa huduma za Kristo za kikuhani, kinabii na kifalme katika utume wa watu wa Mungu kwa ujumla. Waamini walei wanatimiza wajibu huu kadiri ya hali zao katika Kanisa na katika ulimwengu. Wanashiriki azma ya kutangaza na kushuhudia Injili sanjari na kuyatakatifuza malimwengu, kwa njia ya chachu ya tunu msingi za Kiinjili. Utume huu unatekelezwa katika imani, matumaini na mapendo, ambayo Roho Mtakatifu hueneza mioyoni mwa wanakanisa wote. Waamini walei waendeleze mchakato wa kuinjilisha na wa kutakatifuza malimwengu, huku wakionesha bidii ya kupenyeza roho na mwamko wa kikristo katika mpango wa malimwengu. Baba Mtakatifu Francisko katika nia zake za kimisionari kwa Mwezi Oktoba 2020, anasali ili kwa neema ya Ubatizo, waamini walei na hasa zaidi wanawake, waweze kushiriki zaidi katika dhamana na utume wa uongozi ndani ya Kanisa.

Baba Mtakatifu katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro anaendelea kujitahidi kuhakikisha kwamba, wanawake wanapata nafasi za uongozi katika maisha na utume wa Kanisa na kamwe wasiachwe nyuma. Huu ni mwaliko wa kuhakikisha kwamba, haki za wanawake zinaheshimiwa na kuthaminiwa katika maisha na utume wa Kanisa. Wanawake washirikishwe katika nafasi za kiutendaji pamoja na maamuzi. Rej. EG. 104. Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili tarehe 11 Oktoba 2020 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican amesema, hakuna mtu awaye yote ambaye amebatizwa kama Padre au Askofu, bali wote wamebatizwa kama waamini walei. Waamini walei ni mihimili ya maisha na utume wa Kanisa. Leo hii kuna haja ya kuwashirikisha zaidi waamini walei na hasa wanawake katika maisha na utume wa Kanisa. Hii inatokana na ukweli kwamba, wanawake wengi wamekuwa wakibakizwa nyuma katika maisha na utume wa Kanisa hasa wakati wa kufanya maamuzi mazito kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa.

Baba Mtakatifu katika nia zake za kimisionari kwa Mwezi Oktoba 2020 anaendelea kukazia umuhimu wa wanawake kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa bila kutumbukia katika mwono tenge wa karama za waamini walei, tayari kupyaisha Uso wa Mama Kanisa! Baba Mtakatifu wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, amependa kuonesha uwepo wake wa karibu kwa watu wanaoteseka kutoka na janga la moto unaoendelea kuteketeza misitu sehemu mbali mbali za dunia, kiasi hata cha kuhatarisha maisha ya watu na mali zao. Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu amewakumbuka wananchi wa California, nchini Marekani, Amerika ya Kati na hasa katika eneo la Pantana, Uruguay pamoja na Argentina. Majanga haya ya moto ni matokeo ya ukame wa muda mrefu lakini pia kuna baadhi ya watu wameshiriki katika kuchoma misitu kwa makusudi, jambo ambalo ni hatari sana katika mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote!

Baba Mtakatifu ameonesha furaha yake kwa Serikali za Armenia na Azerbaijan ambazo zimetiliana saini mkataba wa kusitisha mashambulizi ya silaha, ili kuruhusu huduma kuweza kutolewa na hatimaye, amani ya kudumu kuweza kupatikana. Mchakato wa usitishwaji wa mapambano ya silaha ni dhaifu sana, lakini Baba Mtakatifu anapenda kuwatia moyo wadau wote kujielekeza zaidi katika amani. Anapenda pia kuwahakikishia watu wote wa Mungu walioathirika kutokana na machafuko ya kisiasa kati ya nchi hizi mbili, kwamba, yuko pamoja nao kwa njia ya sala. Anaendelea kuwaombea wale wote ambao maisha yao yako hatarini kutokana na vita kati ya Armenia na Azerbaijan.

Papa: Waamini Walei
12 October 2020, 14:24