Tafuta

Mwenyeheri Carlo Acutis alisimika maisha yake katika Ibada kwa Ekaristi Takatifu, Huduma kwa maskini, Ibada ya Rozari Takatifu pamoja na uinjilishaji kwa njia ya mitandao ya kijamii! Mwenyeheri Carlo Acutis alisimika maisha yake katika Ibada kwa Ekaristi Takatifu, Huduma kwa maskini, Ibada ya Rozari Takatifu pamoja na uinjilishaji kwa njia ya mitandao ya kijamii! 

Mwenyeheri Carlo Acutis: Ekaristi, Maskini, Uinjilishaji Na Rozari!

Mwenyeheri Carlo Acutis ni kijana aliyekuwa na upendo na ibada kwa Ekaristi Takatifu, aliyebahatika kusoma alama za nyakati, akaiona Sura ya Kristo Yesu miongoni mwa maskini. Ushuhuda wake wenye mvuto na mashiko ni dira na mwaliko kwa “Millenials”, kutambua kwamba, furaha ya kweli katika hija ya maisha inapatikana kwa kumpatia Mwenyezi Mungu kipaumbele cha kwanza

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kardinali Agostino Vallini, Jumamosi, tarehe 10 Oktoba 2020 kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Francisko wa Assisi mjini Assisi, Italia, amemtangaza Mtumishi wa Mungu Carlo Acutis, kuwa ni Mwenyeheri”. Mwenyeheri Carlo Acutis: “Teenage Computer Genius” gwiji wa intenet, aliyeanzisha wavuti kwa ajili ya katekesi, alikuwa na Ibada kwa Ekaristi Takatifu, Bikira Maria na Kanisa katika ujumla wake. Itakumbukwa kwamba, alifariki dunia tarehe 12 Oktoba 2006, akiwa na umri wa miaka 15 tu! Mama Kanisa atakuwa anaadhimisha kumbukumbu yake ya kuzaliwa mbinguni kwa njia ya kifo kila mwaka ifikapo tarehe 12 Oktoba! Baba Mtakatifu Francisko, mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili tarehe 11 Oktoba 2020 amemtaja Mwenyeheri Carlo Acutis kuwa ni kijana mwenye umri wa miaka 15 aliyekuwa na upendo na ibada kuu kwa Ekaristi Takatifu, aliyebahatika kusoma alama za nyakati, akaiona Sura ya Kristo Yesu miongoni mwa maskini na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii. Ushuhuda wake wenye mvuto na mashiko ni dira na mwaliko kwa vijana wa kizazi kipya “Millenials”, kutambua kwamba, furaha ya kweli katika hija ya maisha inapatikana kwa kumpatia Mwenyezi Mungu kipaumbele cha kwanza, kwa kumpenda na kumhudumia kwa njia ya jirani, kwa kutoa upendeleo wa pekee kwa maskini zaidi!

Kardinali Agostino Vallini katika mahubiri yake, amekazia umuhimu wa waamini kuzama zaidi katika Ibada ya Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa; mahali pa kujenga na kukuza mahusiano na mafungamano na Kristo Yesu, Mkombozi wa ulimwengu, njia kuu ya kumpeleka mwamini mbinguni. Kwa Mwenyeheri Carlo Acutis, Kristo Yesu kwake alikuwa ni: Rafiki na mwandani wa maisha; Mwalimu na Mkombozi; Nguvu na dira ya maisha. Ni katika muktadha huu, Mwenyeheri Carlo Acutis akajenga na kudumisha Ibada kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa kwa njia ya Rozari Takatifu, kiasi hata cha kujihusisha kikamilifu katika mchakato wa uinjilishaji miongoni mwa vijana wa kizazi kipya kwa njia ya internet. Ili kuwafikia vijana wengi zaidi, akaamua kuanzisha wavuti yake, kama kielelezo makini cha wema na upendo wake kwa Kristo Yesu. Mitandao ya kijamii, ikawa ni njia ya kutangaza na kushuhudia tunu msingi za maisha ya Kikristo kwa watu wa Mataifa; sanjari na kuwasaidia waamini kujenga na kudumisha urafiki na Kristo Yesu.

Ni kutokana na zawadi kubwa ya imani, matumaini na mapendo kwa Mungu, Kristo na Kanisa lake, akabahatika kukabiliana kwa ujasiri mkubwa na changamoto za ugonjwa na mahangaiko ya ndani katika maisha yake. Mambo makuu mawili, yawasaidie waamini kumkumbuka Mwenyeheri Carlo Acutis, Sala na Utume miongoni mwa vijana wa kizazi kipya! Alijipambanua kwa kusimama kidete kulinda, kutangaza na kushuhudia utakatifu wa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia; utu, heshima na haki msingi za binadamu kwa kutambua kwamba, maisha ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kumbe, yanapaswa kulindwa na kudumishwa dhidi ya utamaduni wa kifo unaokumbatia sera za utoaji mimba na kifo laini, yaani Eutanasia! Upendo kwa Mungu na jirani ni muhtasari wa Mafundisho makuu ya Kristo Yesu kwa wafuasi wake. Maisha, utume na utakatifu wake ni mfano bora wa kuigwa na vijana wa kizazi kipya!

Askofu Domenico Sorrentino wa Jimbo Katoliki la Assisi-Nocera Umbra-Gualdo Tadino katika salam zake za shukrani anasema, Mwenyeheri Carlo Acutis ni kijana aliyeng’amua siri ya uzuri na furaha ya maisha ya ujana; akawa ni chombo cha toba na wongofu wa ndani kwa kwazazi wake Andrea na Antonia, ambao kwa sasa ni mashuhuda wa utakatifu wa mtoto wao. Ni mwaliko kwa Kanisa kuendelea kuwekeza zaidi katika utume miongoni mwa vijana, ili waweze kuwa ni mashuhuda wa tunu msingi za Kiinjili na utu wema. Maisha ya Mwenyeheri Carlo Acutis yalipambwa kwa Ibada na upendo kwa Ekaristi Takatifu; Ibada kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa pamoja na huduma makini kwa maskini, kielelezo cha imani inayomwilishwa katika Injili ya upendo.

Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko: "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii”, uliotiwa saini tarehe 3 Oktoba 2020 huko mjini Assisi, Italia na kuzinduliwa rasmi tarehe 4 Oktoba 2020 sanjari na Maadhimisho ya Sikukuu ya Mtakatifu Francisko wa Assisi aliyejikita katika: huduma bora kwa maskini, amani na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, ni mwendelezo wa neema, furaha na shukrani ya watu wa Mungu. Kwa sasa Jimbo Katoliki la Assisi-Nocera Umbra-Gualdo Tadino limeanzisha Tuzo ya Kimataifa ya Mtakatifu Francisko wa Assisi na Mwenyeheri Carlo Acutis, kama njia ya kumwilisha Injili ya upendo kwa maskini sanjari na kupyaisha sera na mikakati ya uchumi kitaifa na kimataifa!

Carlo Acutis
12 October 2020, 15:41