Tafuta

Mama Kanisa anahimiza sera na mikakati ya uchumi na maendeleo fungamani ya binadamu inayofumbatwa katika tunu msingi za Kiinjili. Mama Kanisa anahimiza sera na mikakati ya uchumi na maendeleo fungamani ya binadamu inayofumbatwa katika tunu msingi za Kiinjili. 

Mikakati ya Maendeleo Inayojikita Katika Tunu Msingi za Kiinjili

Baba Mtakatifu Francisko anawataka Maaskofu kuwa karibu zaidi na wakleri wao; kukuza na kudumisha tunu msingi za maisha ya Kiinjili ili kupambana na saratani ya rushwa, ufisadi na kumong'onyoka kwa haki msingi, utu na heshima ya binadamu na kwamba, Maaskofu wathamini majadiliano katika ukweli na uwazi. Mikakati ya Injili inapaswa kufumbata tunu za Kiinjili.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kitume huko Amerika ya Kusini kunako mwaka 2018 alisikitika kusema kwamba, ukoloni mamboleo unaojikita katika nguvu ya kiuchumi: kwa uchimbaji wa mafuta na gesi asilia; kilimo cha mashamba makubwa ili kukidhi mahitaji ya mali ghafi ya viwanda; ni mambo yanayotishia usalama, maisha, ustawi na maendeleo ya Ukanda wa Amazonia. Baba Mtakatifu anawataka Maaskofu kuwa karibu zaidi na wakleri wao; kukuza na kudumisha tunu msingi za maisha ya Kiinjili ili kupambana na saratani ya rushwa, ufisadi na kumong'onyoka kwa haki msingi, utu na heshima ya binadamu na kwamba, Maaskofu wathamini majadiliano katika ukweli na uwazi. Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia kuanzia tarehe 6-27 Oktoba, 2019 yaliongozwa na Kauli mbiu: “Amazonia: njia mpya ya Kanisa na kwa ajili ekolojia fungamani”. Kuna umuhimu wa kuendelea kusikiliza pia kilio cha Mama Dunia na maskini kutoka Ukanda wa Amazonia, tayari kuibua mbinu mkakati utakaosaidia mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Waamini wa Ukanda wa Amazonia, wanacho kilio kingine cha ukosefu wa huduma msingi za maisha ya kiroho kutokana na uhaba wa mihimili ya uinjilishaji yaani: wakleri, watawa na makatekista.

Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake wakati wa hija yake ya kichungaji huko Puerto Maldonado, nchini Peru hapo tarehe 19 Januari 2018, aliwashukuru na kuwapongeza wananchi wa Ukanda wa Amazonia wanaoendelea kushuhudia utajiri wa kibayolojia, kitamaduni, maisha ya kiroho na hekima itakayowawezesha watu wengi zaidi kusimama kidete, kulinda, kutunza na kudumisha mazingira nyumba ya wote, kwani hapa, ni mahali patakatifu, ambapo panawawezesha watu kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani! Baba Mtakatifu alisema, yuko kati yao kuwatembelea, kuwasikiliza na kukaa pamoja nao, ili kuweza kukabiliana na changamoto mamboleo, tayari kusimama kidete kulinda na kudumisha Injili ya uhai, mazingira bora na utamaduni unaozingatia utu na heshima ya binadamu! Uwepo wa wananchi wa Ukanda wa Amazonia kuliko wakati mwingine wowote katika historia yao, sasa wanatishiwa zaidi na nguvu za kiuchumi: zinazotafuta kuchimba mafuta, gesi asilia na madini; ni sera na mikakati ya kilimo cha mashamba makubwa pamoja na sera zisizotoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu, kiasi kwamba,  watu wananyanyaswa na kudhulumiwa; rasilimali na utajiri uliopo ndani ya misitu hii hauwasaidii sana wenyeji na matokeo yake, vijana wa kizazi kipya wanakimbia ili kutafuta maisha bora zaidi ugenini.

Umefika wakati wa kuzingatia mahitaji halisi ya wananchi wa Amazonia badala ya utajiri wa eneo hili kuyanufaisha mataifa tajiri na makampuni makubwa makubwa ya kigeni! Ili kuweza kufikia sera na mikakati ya maendeleo endelevu kuna haja kwa Serikali na taasisi kuwaheshimu na kuwathamini wananchi mahalia; kwa kujenga na kudumisha majadiliano na watu mahalia sanjari na kuzingatia: tamaduni, lugha, mapokeo, haki na amana ya maisha ya kiroho. Wananchi mahalia washirikishwe kwenye majadiliano yanayogusa kwa karibu zaidi maisha yao, ili kuondokana na tabia ya ubaguzi pamoja na wananchi hao kutengwa. Baba Mtakatifu anakaza kusema, kuna “cheche za matumaini” zinazozijengea uwezo Jumuiya mahalia ili kusimama kidete: kulinda na kutunza misitu na faida ya mazao yake, inawanufaisha wananchi mahalia kwa kuboresha hali ya maisha yao, kwa kuwapatia wananchi huduma bora zaidi ya elimu na afya ili kupambana vyema na mazingira yao.

Kardinali Claudio Hummes, Rais wa Mtandao wa Kanisa Amerika ya Kusini, (Pan-Amazon Ecclesial Network of the Latin American Church, REPAM) anasema, sera na mikakati ya maendeleo fungamani ya binadamu haina budi kupata chimbuko na hatimaye, kufumbatwa katika tunu msingi za Kiinjili. Kardinali Hummes katika mahojiano na Shirika la Habari za Kimissionari la Fides anakaza kusema, familia ya Mungu katika Ukanda wa Amazonia, inaendelea kujiandaa kikamilifu ili kuhakikisha kwamba, inashiriki kikamilifu katika mchakato mzima wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu wa Amazonia. Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil na Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Amerika ya Kusini na Caribbean tayari lilikwisha aanza maandalizi ya Sinodi ya Maaskofu wa Amazonia. Kanisa huko Amerika ya Kusini linakabiliwa na changamoto mbali mbali za kimissionari, kijamii na kiutu zinazopaswa kuvaliwa njuga, ili kupatiwa ufumbuzi muafaka kwa kutumia mwanga wa Injili ya huruma na matumaini!

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, hii ni njia bora zaidi ya kuishi na kutenda; ni kilio cha watu mahalia, kinachopaswa kusikilizwa; kwa kutekeleza dhamana na wito ambao Mwenyezi Mungu amemkabidhi binadamu, yaani kutunza mazingira nyumba ya wote kwani hatimaye yake ni kulinda Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Baba Mtakatifu anakiri kwamba, anafahamu mateso na mahangaiko yao yanayotokana na uchafuzi wa mazingira; uchimbaji haramu wa madini; biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo pamoja na nyanyaso za kijinsia; mateso na nyanyaso za wanawake na watoto majumbani. Hawa ni watu ambao utu na heshima yao viko mashakani kama alivyokuwa anasema Mtakatifu Turibius wa Magrovejo wakati wa maadhimisho ya Mtaguso III wa Lima, miaka mia tano iliyopita, lakini hata leo hii, kilio chao bado kinasikika. Kanisa litaendelea kutekeleza dhamana yake ya kinabii kwa kuwa ni sauti ya wanyonge na wale wanaoteseka.

Baba Mtakatifu anasikitishwa sana na hali ya “wananchi mahalia ambao wametengwa kwa hiyari yao wenyewe” ( PIAV). Hawa ni watu ambao hawana tena uhuru, mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa kushikamana ili kuwatetea ili kuondokana na uwezekano wa kutokea kwa maafa makubwa kwa watu sanjari na uharibifu wa mazingira! Mwanadamu akumbuke kwamba, amepewa dhamana ya kulinda na kutunza mazingira na  Mwenyezi Mungu na wala si mmiliki wa kazi ya uumbaji. Kumbe, mtindo wa maisha na hekima ya watu mahalia iwasaidie watu wa Mataifa kujizatiti katika kuboresha hali ya maisha ya wananchi wa Amazonia. Ukanda wa Amazonia ni alama ya maisha, hifadhi ya tamaduni na tofauti za kibayolojia; mambo ambayo yanapaswa kulindwa dhidi ya ukoloni mamboleo. Familia za watu mahalia daima zimekuwa mstari wa mbele kulinda Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo, lakini kutokana na mwingiliano wa watu tamaduni hizi zinaanza kufifia, changamoto ni kusimama kidete kutunza tamaduni, mapokeo na lugha ili kuenzi hekima ya wahenga. Elimu inawasaidia watu kujenga daraja na utamaduni wa watu kukutana, kumbe, hii ni dhamana nyeti ya Serikali inayopaswa kutamadunishwa na kushirikishwa kama ustawi na mafao ya wananchi wengi.

Kardinali Claudio Hummes, Rais wa Mtandao wa Kanisa Amerika ya Kusini ulioanzishwa kunako mwaka 2014 huko Brasilia, nchini Brazil anasema, Sinodi hii ilikuwa ni kwa ajili ya Watu wa familia ya Mungu katika ujumla wake kwani watashiriki wakleri, watawa na waamini walei. Maandalizi ya nyaraka mbali mbali yatapata chimbuko lake katika uhalisia wa maisha ya wananchi wa Amazonia na kwamba, waamini walei ndio wanaoguswa na kuathirika zaidi kutokana na changamoto za kimisionari, kijamii na kiutu huko Amazonia, kumbe, wanategemewa sana na Mama Kanisa kwamba, watashirikisha uzoefu na mang’amuzi yao kutoka katika medani mbali mbali za maisha, ili kuweza kufanikisha maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu wa Ukanda wa Amazonia na utekelezaji wake. Baba Mtakatifu Francisko analitaka Kanisa pia kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kuanzisha shule, taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu pamoja na kuwaendeleza watu mahalia. Vijana wafundwe vyema uelewa mpya wa binadamu, kusoma tena historia ya watu na maendeleo yao. Baba Mtakatifu anawashukuru wasanii wote kwa juhudi zao za kuonesha mwono wa ulimwemgu, utajiri wa tamaduni. Umefika wakati kwa wananchi mahalia kuandika historia ya nchi yao; kujitambulisha, kwani watu hawa wanahitaji kusikilizwa pengine kuliko wakati mwingine wowote wa historia yao.

Kardinali Claudio Hummes katika mahojiano maalum na Fides anasema, tangu Mwaka 2013, Baba Mtakatifu Francisko aliwataka viongozi wa Ukanda wa Amazonia unaojikita hasa katika masuala ya haki na mshikamano; utume na huduma ya upendo,  kuhakikisha kwamba, Injili inatamadunishwa katika uhalisia wa maisha ya wananchi wa Amazonia, ili Kanisa liweze kupata sura mpya ya watu wa Amazonia kwa kuwa na: wakleri pamoja na watawa wake! Hii ni changamoto inayohitaji ari, ujasiri na moyo wa kuthubutu, kwani kila jambo linawezekana mbele ya Mwenyezi Mungu. Kuna changamoto kubwa ya uharibifu mkubwa wa mazingira nyumba ya wote na ukoloni mamboleo unaofumbatwa katika nguvu ya kiuchumi inayotishia ustawi, maendeleo na mafao ya wananchi wa Amazonia. Sinodi ya Maaskofu wa Amazonia ilipania pamoja na mambo mengine, kuibua mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji na kitume kwenye Ukanda wa Amazonia. Kuna uhaba mkubwa wa mihimili ya uinjilishaji, hali inayowafanya waamini wa Amazonia kukosa huduma makini na endelevu za kichungaji, kiasi hata cha kujisikia kwamba, wametelekezwa na Mama Kanisa.

Baba Mtakatifu Francisko kwa upande wake, amewapongeza wamisionari wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya kuwatetea wananchi wa Amazonia, dhamana ambayo wanaitekeleza kama ushuhuda kwa Injili ya furaha na matumaini. Kristo Yesu alijimwilisha katika tamaduni za Kiyahudi, chachu mpya ya utambulisho wa mtu. Utamadunisho ni mchakato unaolitajirisha Kanisa na kwamba, Kanisa linataka kuwajengea uwezo wa kupambana na changamoto za maisha, ili siku moja Kanisa liweze kuwa na sura ya Amazonia inayofumbatwa na uwepo wa watu mahalia. Hiki ndicho kiini cha Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Ukanda wa Amazonia iliyoadhimishwa mjini Vatican kunako mwaka 2019. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, wataendelea kuimarisha mafungamano ya kijamii, kimaumbile na mang’amuzi ya imani yao kwa Kristo na Kanisa lake.

Kardinali Claudio Hummes anasema, Kanisa halina budi kushiriki katika mchakato wa sera na mbinu mkakati wa shughuli za maendeleo endelevu ya binadamu huko Amazonia kwa kujikita katika Injili inayotoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima, haki na mahitaji msingi ya binadamu. Kanisa linapenda kukazia Injili ya upendo na mshikamano unaowashirikisha wananchi mahalia katika maamuzi na utekelezaji wa sera na mikakati yake. Kanisa linataka kutoa kipaumbele cha pekee katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote ili kulinda Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo, sera na mikakati isiyozingatia haki msingi za binadamu. Kanisa linataka kutangaza na kushuhudia Injili ya furaha na matumaini; kwa kujikita katika mchakato mzima wa utamadunisho, ili kweli Injili iweze kugusa, kuganga na kutakasa maisha ya watu mahalia, ili kweli waweze kuwa ni mashuhuda na vyombo vya Injili ya matumaini na huruma ya Mungu kwa waja wake!

Ukanda wa Amazonia

 

 

20 October 2020, 08:04