Tafuta

Papa Francisko Waraka wa Kitume "Scripturae Sacrae Affectus": Waraka Wa Kitume Juu ya Maandiko Matakatifu, Miaka 1600 Tangu Alipofariki Dunia Mtakatifu Jerome, Padre na Mwalimu wa Kanisa. Papa Francisko Waraka wa Kitume "Scripturae Sacrae Affectus": Waraka Wa Kitume Juu ya Maandiko Matakatifu, Miaka 1600 Tangu Alipofariki Dunia Mtakatifu Jerome, Padre na Mwalimu wa Kanisa. 

Waraka Wa Kitume "Scripturae Sacrae affectus" Mt. Jerome!

Papa Francisko: "Scripturae Sacrae Affectus" Yaani “Waraka wa Kitume Juu ya Upendo Kwa Maandiko Matakatifu, Miaka 1600 Tangu Alipofariki Dunia Mtakatifu Jerome”, Padre na Mwalimu wa Kanisa aliyeweka Maandiko Matakatifu kuwa kiini cha maisha yake, awasaidie waamini kupyaisha ndani mwao upendo wa kusoma, kutafakari na kumwilisha Maandiko Matakatifu katika maisha.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mtakatifu Jerome (Jina kamili ni Eusebius Sophronius Hieronymus) kwa agizo la Papa Damasi wa kwanza, kwa muda wa miaka 23 alifanya kazi ya kutafsiri na kupanga vitabu vya Biblia kwa lugha ya Kilatini, maarufu kama “Vulgata” iliyopitishwa na Mababa wa Mtaguso wa Trento (1545-1563) kwamba inafaa kufundishia imani. Alifariki dunia tarehe 30 Septemba 420 akiwa ameliachia Kanisa utajiri mkubwa wa Maandiko Matakatifu. Mama Kanisa tarehe 30 Septemba 2020 anaadhimisha kumbukumbu ya miaka 1600 tangu Mtakatifu Jerome alipofariki dunia. Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Katekesi yake, Jumatano tarehe 30 Septemba 2020, Sikukuu ya Mtakatifu Jerome, Padre na Mwalimu wa Kanisa amesema kwamba, “ametia mkwaju” kwenye Waraka wa Kitume Unaojulikana kama: "Scripturae Sacrae Affectus" Yaani “Waraka wa Kitume Juu ya Upendo Kwa Maandiko Matakatifu, Miaka 1600 Tangu Alipofariki Dunia Mtakatifu Jerome”. Mtakatifu Jerome Padre na Mwalimu wa Kanisa aliyeweka Maandiko Matakatifu kuwa kiini cha maisha yake, awasaidie waamini kupyaisha ndani mwao ari, moyo na upendo wa kusoma, kutafakari na kumwilisha Maandiko Matakatifu katika uhalisia wa maisha yao. Waamini wajenge utamaduni wa kujadiliana na Mwenyezi Mungu kwa njia ya Maandiko Matakatifu.

Katika Waraka huu, Baba Mtakatifu Francisko anachambua: Historia na mchango wa Mtakatifu Jerome katika Maandiko Matakatifu, Hekima ya Mtakatifu Jerome inayofumbatwa katika ushuhuda wake kwa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu; Upendo kwa Maandiko Matakatifu, Masomo ya Maandiko Matakatifu yanayohitaji mwongozo makini ili kuweza kuyatafakari na hatimaye, kuyatafsiri na kuyamwilisha katika uhalisia wa maisha ya mtu. Mchango wa Mtakatifu Jerome katika kutafsiri na kupanga Biblia ya Kilatini, Vulgata; Tafsiri yake kama sehemu ya utamadunisho. Mtakatifu Jerome na Kiti Kitakatifu cha Mtakatifu Petro. Mwaliko wa kupenda kile alichopenda Mtakatifu Jerome, yaani Maktaba ya Maandiko Matakatifu.

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko kwa njia ya barua binafsi “Motu Proprio” “Aperuit Illis” ameanzisha “Domenika ya Neno la Mungu” itakayokuwa inaadhimishwa kuanzia sasa kila mwaka, Jumapili ya III ya Kipindi cha Mwaka wa Kanisa. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, Jumapili hiyo itakuwa ni fursa kwa watu wa Mungu kujenga utamaduni wa kusoma, kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha yao. Utambulisho wa Wakristo unafumbatwa kwa namna ya pekee, katika mahusiano ya dhati kati ya: Kristo Mfufuka, Maandiko Matakatifu na Jumuiya ya waamini. Ndiyo maana Mtakatifu Jerome anasema “Kutojua Maandiko Matakatifu ni kutomfahamu Kristo”. Baba Mtakatifu anasema, wazo la kuanzisha “Domenika ya Neno la Mungu” lilimwijia mara baada ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya Huruma ya Mungu, ili kuendeleza majadiliano kati ya Mwenyezi Mungu na waja wake; mwaliko wa kuendelea kulipyaisha Kanisa kwa amana na utajiri unaobubujika kutoka katika Maandiko Matakatifu.

Maandiko Matakatifu
30 September 2020, 16:02