Tafuta

Tarehe 26 Septemba, Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Siku ya Kutokomeza Silaha za Nyuklia Duniani. Tarehe 26 Septemba, Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Siku ya Kutokomeza Silaha za Nyuklia Duniani. 

Siku ya Kutokomeza Silaha Za Nyuklia Duniani 26 Sept. 2020

Tarehe 26 Septemba 2020 Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Siku ya Kutokomeza Silaha za Nyuklia Duniani, Papa Francisko anawaalika waamini kumwomba Mungu awajalie zawadi ya amani, kwa kuwa na dunia ambayo haina silaha za maangamizi. Papa anawaalika watu wote kujiondoa kabisa katika mwelekeo huu wa silaha za nyuklia kwani hili ni tishio kubwa kwa jamii ya binadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Jumuiya ya Kimataifa kila mwaka ifikapo tarehe 26 Septemba inaadhimisha Siku ya Kutokomeza Silaha za Nyuklia Duniani, changamoto iliyovaliwa njuga na Umoja wa Mataifa kunako mwaka 1946 kwa kuanzisha Tume ya Nguvu ya Atomic, iliyofutwa kunako mwaka 1952 na hatimaye kukaanzishwa Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomic, IAEA. Umoja wa Mataifa umeendelea kutoa kipaumbele cha pekee katika mchakato wa kutokomeza silaha za nyuklia duniani. Hadi leo hii, kuna silaha 13, 400 za nyuklia sehemu mbalimbali za dunia na kwamba, majadiliano kuhusu kutokomeza silaha za nyuklia bado yanaendelea. Kunako mwaka 1996 Jumuiya ya Kimataifa ilipitisha azimio la kuacha mchakato wa utengenezaji, ulimbikizaji na matumizi ya silaha za nyuklia kwani zina madhara makubwa kwa binadamu. Hii bado ni changamoto kubwa kwa Jumuiya ya Kimataifa katika ulimwengu mamboleo. Lakini, nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa wanasema, majadiliano haya yanakwenda polepole sana kwa kuhofia madhara makubwa ambayo yanaweza kusababishwa na matumizi ya silaha za nyuklia anasema Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana António Guterres katika ujumbe wake kwa maadhimisho ya Siku ya Kutokomeza Silaha za Nyuklia Duniani kwa Mwaka 2020.

Hii ni siku ambayo imeanzishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ili kuendelea kuragibisha umuhimu wa kutokomeza silaha za nyuklia kama kipaumbele cha Umoja wa Mataifa. Ni muda muafaka wa kuelimisha jamii umuhimu wa kutokomeza silaha hizi na faida zake katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ni siku muafaka kwa Jumuiya ya Kimataifa kuzungumzia changamoto hii, ili kutafuta na kudumisha misingi ya amani na usalama duniani kwa kuondokana na silaha za nyuklia. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii, tarehe 26 Septemba 2020 Siku ya Kutokomeza Silaha za Nyuklia Duniani, anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kumwomba Mwenyezi Mungu awajalie zawadi ya amani, kwa kuwa na dunia ambayo haina silaha za maangamizi. Baba Mtakatifu anawaalika watu wote kujiondoa kabisa katika mwelekeo huu wa silaha za nyuklia, kwani hili ni tishio kubwa kwa jamii ya mwanadamu!

Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu, Jumapili, tarehe 24 Novemba 2019 alizungumzia kuhusu mateso na maafa makubwa yaliyosababishwa na mashambulizi ya mabomu ya atomiki, changamoto na mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete kulinda na kudumisha misingi ya: usalama, amani na utulivu kwa kuondokana na wasi wasi pamoja na hofu inayotawala akilini na nyoyoni mwa watu kiasi cha kushindwa kuaminiana, na hivyo, kudhohofisha mafungamano ya watu wa Mataifa pamoja na mchakato wa majadiliano. Amani na utulivu wa kimataifa vinaweza kujengeka katika msingi wa mshikamano na ushirikiano wa haki kwa ajili ya huduma kwa kutambua kwamba, watu wanategemeana na kukamilisha; na wanapaswa kuwajibika kama wamoja kwa ajili ya ustawi wa familia nzima ya binadamu.

Baba Mtakatifu anasema, Nagasaki ni mji ambao umeshuhudia maafa makubwa kwa binadamu sanjari na uharibifu wa mazingira nyumba ya wote; kielelezo cha mashindano ya utengenezaji wa silaha za maangamizi; upotevu mkubwa wa rasilimali fedha ambayo ingeweza kutumika kuchochea maendeleo fungamani ya binadamu pamoja na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Rasilimali fedha inayotumika kwa ajili ya kutengeneza, kuboresha na kuhifadhi na hatimaye, kuuza silaha za maangamizi, nyuma yake kuna kilio cha watoto na familia nyingi duniani. Watu wanatamani amani ya kudumu ili kuondokana na vitisho vya silaha za maangamizi na kwamba, hii ni changamoto inayowahusisha watu wote; kwa kujenga na kudumisha utamaduni wa kuaminiana na wala si katika tabia ya kupimana nguvu.

Kuna haja ya kudhibiti biashara ya silaha kimataifa na maendeleo makubwa ya teknolojia kuhusu masuala ya kijeshi. Hii ni dharura inayohitaji kushughulikiwa na viongozi wote wa Jumuiya ya Kimataifa. Baba Mtakatifu anakaza kusema, Kanisa Katoliki kwa upande wake, litaendelea kuhimiza umuhimu wa watu wa Mataifa kudumisha amani. Kanisa linaunga mkono Kanuni ya Sheria ya Kimataifa kuhusu Silaha za Nyuklia, ikiwa ni pamoja na Mkataba wa Kimataifa wa kupiga rufuku utengenezaji, ulimbikizaji na matumizi ya silaha za kinyuklia duniani. Amani ni kazi ya haki na matunda ya upendo! Amani inatishiwa sana na mashindano ya silaha; utengenezaji na biashara ya silaha pamoja na mchakato wa ulimbikizaji wa silaha duniani! Ni wajibu wa Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha amani ambalo ni jina jipya la maendeleo fungamani ya binadamu! Baba Mtakatifu anasema, dunia bila kuwa na silaha za kinyuklia inawezekana kabisa na ni muhimu sana na kwamba, silaha hizi za maangamizi kamwe haziwezi kuwasaidia viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kuwa na uhakika wa usalama wa raia na mali zao kitaifa na kimataifa.

Kuna haja ya kufanya upembuzi yakinifu kuhusu madhara yake katika maisha ya watu sanjari na mazingira; kwa kuondoa hofu, mazingira ya kutoaminiana, chuki na uhasama vinavyozungumza “dhana ya silaha za nyuklia”. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kujielekeza zaidi katika kubuni sera na mikakati itakayosaidia utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ifikapo mwaka 2030. Kunako mwaka 1964, Mtakatifu Paulo VI alishauri kuanzishwa kwa Mfuko wa Maendeleo kwa Nchi Maskini, ambao ungechangiwa kwa kuchukua sehemu ya bajeti ya serikali mbali mbali kwa ajili ya matumizi ya kijeshi. Kumbe, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kutengeneza mazingira ya kuaminiana, kwa sababu hii ni changamoto pevu kwa Jumuiya ya Kimataifa. Umefika wakati wa kusikiliza na kujibu kilio cha maskini kutoka sehemu mbali mbali za dunia, kwa kujenga na kuimarisha utamaduni wa majadiliano; toba na wongofu wa ndani, ili utamaduni wa uhai, upatanisho na udugu viweze kutawala katika akili na nyoyo za watu.

Baba Mtakatifu Francisko baada ya hotuba yake, aliwaomba waamini wa dini mbali mbali kuungana pamoja naye kwa ajili ya kusali ile sala ya Mtakatifu Francisko wa Assisi kwa ajili ya kuombea amani duniani: Ee Bwana unifanye kuwa chombo cha amani. Palipo chuki nieneze upendo. Palipo na mashaka pawe na imani. Palipo na tumaini pawe na matumaini. Palipo na giza pawe na mwanga. Palipo na huzuni pawe na furaha. Ee Bwana Mungu,unijalie; Nisitafute kufarijiwa bali kufariji Nisitafute kupendwa bali kupenda. Kwani ni katika kutoa ndipo tunapopokea Ni kwa kusamehe ndipo tunaposamehewa. Na ni kwa kufa ndipo tunazaliwa katika uzima wa milele, AMINA.  Huu ni mwaliko kwa watu wa Mungu kuongoka na kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu, ili aweze kuwageuza kuwa ni vyombo vya amani na hivyo kutorudia tena kwenye makosa ya zamani.

Silaha Duniani 2020
26 September 2020, 14:52