Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko ameonesha mshikamano na wadau wote katika sekta ya utalii ambayo kwa mwaka 2020 imeathirika sana kutokana na janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na COVID-19 Baba Mtakatifu Francisko ameonesha mshikamano na wadau wote katika sekta ya utalii ambayo kwa mwaka 2020 imeathirika sana kutokana na janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na COVID-19 

Mshikamano wa Papa Francisko Na Wadau wa Sekta Ya Utalii Duniani

Siku Ya Utalii Duniani 2020: Baba Mtakatifu ametumia fursa hii, kuwatia shime wadau mbalimbali katika sekta ya utalii, lakini zaidi, makampuni machanga ambayo mengi yanaendeshwa kwa mfumo wa familia pamoja na vijana. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, wote kwa pamoja wataweza kusimama tena imara na kusonga mbele katika maboresho ya sekta ya utalii duniani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Siku ya 41 ya Utalii Duniani tarehe 27 Septemba 2020 yameongozwa na kauli mbiu “Utalii na Maendeleo Vijijini”. Maadhimisho haya yamefanyika wakati ambapo janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 linaendelea kuleta athari kubwa kwa maisha ya watu na mali zao. Utalii ni kati ya sekta ambazo zimeathirika sana kutoka na gonjwa la Virusi vya Corona, COVID-19. Usafiri wa anga ulisitishwa, mipaka ikafungwa, watu wakalazika kukaa karantini. Wadau wa sekta ya utalii, wakaathirika sana. Takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii Duniani (World Tourism Organization, UNWTO) zinaonesha kwamba, utalii kwa kipindi cha mwaka 2020 umepungua kwa kiasi cha watalii bilioni moja na hivyo kuifanya Jumuiya ya Kimataifa kupoteza kiasi cha dola za Kimarekani bilioni 1, 200, sanjari na upotevu mkubwa wa nafasi za kazi. Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 27 Septemba 2020, amesikitika kusema kwamba, gonjwa la Virusi vya Corona, COVID-19 limesababisha hasara kubwa kwa nchi nyingi duniani kwa sababu sekta ya utalii inachangia kwa kiasi kikubwa pato la mataifa mengi.

Baba Mtakatifu ametumia fursa hii, kuwatia shime wadau mbalimbali katika sekta ya utalii, lakini zaidi, makampuni machanga ambayo mengi yanaendeshwa kwa mfumo wa familia pamoja na vijana. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, wote kwa pamoja wataweza kusimama tena imara na kusonga mbele katika maboresho ya sekta ya utalii duniani.  Kwa upande wake Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana António Guterres katika ujumbe wake kwa maadhimisho ya Siku ya Utalii Duniani anasema, kuna mabadiliko na mahitaji makubwa ya watu kusafiri; umuhimu wa kulinda na kutunza amani na utulivu duniani sanjari na kutunza mazingira nyumba ya wote. Utalii ni chanzo cha ajira na mapato kitaifa na kwa watu binafsi, hali inayochangia maboresho ya maisha ya watu. Janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 limesababisha athari kubwa kiasi kwamba, ajira milioni 120 ziko hatarini kutoweka na hivyo kusababisha hasara ya asilimia 1.5% ya Pato Ghafi la Dunia, (GDP). Utalii katika nchi changa zaidi duniani umeathirika sana.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anasema,  katika mchakato wa kufufua sekta ya utalii duniani, kuna haja ya kuwekeza zaidi katika utalii salama, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na maisha ya watu vijijini. Kuna umuhimu wa kulinda na kutunza mazingira; kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi sanjari na kukuza uchumi. Utalii salama unapania kuongeza kipato cha wananchi vijijini, kwa kulinda na kutunza mazingira bora nyumba ya wote kwa ajili ya maendeleo ya wengi. Utalii unalo jukumu kubwa la kulinda tamaduni, bayoanuai na hivyo kuruhusu mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu kuchukua mkondo wake.  Katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuitia shime Jumuiya ya Kimataifa kujenga umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu, tayari kuanza upya, kwani si rahisi sana kurejesha mambo kama yalivyokuwa kabla ya ugonjwa Virusi vya Corona, COVID-19. Hii ni sehemu ya ujumbe uliotolewa na Kardinali Peter Kodwo Appiah Turkson, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu, kama sehemu ya Maadhimisho ya Siku ya Utalii Duniani.

Ujumbe wa mwaka huu uliokuwa umechaguliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii Duniani (World Tourism Organization, UNWTO), ulionesha mchango mkubwa ambao ungeweza kutolewa na sekta ya utalii katika mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu kwa kujielekeza zaidi vijijini. Lengo ni kukuza na kudumisha utalii fungamani na unaowajibisha kwa kuzingatia kanuni ya haki jamii, uchumi sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Hapa mkazo unawekwa katika kutunza tamaduni za watu mahalia, kutambua na kuthamani Jumuiya mahalia na haki yake ya kuwa mdau katika mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu na uwajibikaji wa kijamii katika eneo husika. Kumbe, huu ni utalii unaochangia mwingiliano na mafungamano kati ya sekta ya utalii, Jumuiya mahalia pamoja na watalii wenyewe. Mfumo huu ni muhimu sana katika kukuza pia sekta ya kilimo, kwa kuwawezesha hata wakulima wadogo wadogo kuchangia katika uzalishaji wa chakula. Kilimo na utalii vijijini vinaweza kuchangia ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, kwa kuheshimu na kuzingatia ekolojia kwa kuendelea kujikita katika mshikamano na udugu wa kibinadamu, sanjari na kuibua mitindo mipya ya maisha.

Sekta ya utalii na kilimo vinaweza kusaidia kuibua utamaduni mpya; kwa kulinda na kudumisha tunu msingi za maisha ya binadamu; kwa kuendeleza mazingira bora nyumba ya wote. Hili ni hitaji msingi la kimaadili na dharura inayohitaji utekelezaji wa pamoja. Utalii Vijijini ni fursa ya kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano na jirani pamoja na kudumisha mazingira bora nyumba ya wote kwa kuondokana na kishawishi cha mabadiliko makubwa yanayoweza kuwa ni sababu ya hofu na wasi wasi. Utalii ukuze na kujenga ujirani mwema, usaidie watu kutembeleana ili kukuza na kudumisha umoja na udugu wa kibinadamu kati ya watu wa Mataifa. Katika kipindi hiki cha janga la Virusi vya Corona, COVID-19 utalii unaowajibisha na fungamani ni muhimu sana katika mapambano dhidi ya umaskini ambao umeongezeka maradufu kutokana na janga la Virusi vya Corona, COVID-19. Mama Kanisa anapenda kuonesha uwepo wake wa karibu na mshikamano kwa wadau wa sekta ya utalii duniani. Kardinali Peter Kodwo Appiah Turkson Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu anawahimiza wadau mbalimbali katika sekta ya utalii, kuhamasisha utalii unaowajibisha, kwa kuzingatia kanuni ya hakijamii na uchumi fungamani; kwa kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote pamoja na kuheshimu tamaduni za watu mahalia.

Utalii vijijini upewe msukumo wa pekee, kwa kuwahusisha wanavijiji katika mchakato wa maamuzi mbalimbali bila kusahau maboresho ya ujira kwa wafanyakazi mahalia. Mwaliko unatolewa kwa wanaharakati wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, kusaidia kuragibisha wongofu wa kiekolojia; kwa kuthamini utu, heshima na haki msingi za binadamu. Huu ni mwaliko wa kuendeleza uchumi fungamani unaotoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini, pamoja na kuwajengea uweazo wa kiuchumi wakulima wadogo wadogo. Makanisa mahalia yasaidie kukuza utalii vijijini; wananchi wasaidie wafanyakazi katika sekta ya utalii ambao kwa wakati huu wanakabiliana na hali ngumu ya maisha, sanjari na mchakato wa utunzaji bora wa mazingira.

Utalii 2020
28 September 2020, 14:58