Tafuta

Maadhimisho ya Siku ya 106 ya Wakimbizi na Wahamiajki Duniani Kwa mwaka 2020: Walengwa zaidi: watu wasiokuwa na makazi maalum kutokana na vita na majanga asilia. Maadhimisho ya Siku ya 106 ya Wakimbizi na Wahamiajki Duniani Kwa mwaka 2020: Walengwa zaidi: watu wasiokuwa na makazi maalum kutokana na vita na majanga asilia. 

Siku ya 106 ya Wakimbizi 2020: Watu Wasiokuwa na Makazi Maalum!

Baba Mtakatifu Francisko anasema kauli mbiu ya Mwaka 2020: “Kama Kristo Yesu, wanalazimishwa kukimbia”. Hivi ndivyo hali ilivyo kwa wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum. Baba Mtakatifu amewasalimia wote na kuwahakikishia sala na sadaka yake kwa wakimbizi, wanahamiaji pamoja na wale wote wanaowahudumia kwa moyo wa huruma na mapendo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Siku ya 106 ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani tarehe 27 Septemba 2020 yameongozwa na kauli mbiu “Kama Kristo Yesu, wanalazimishwa kukimbia”. Kuwakaribisha, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwashirikisha watu wasiokuwa na makazi maalum. Baba Mtakatifu Francisko anasema wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji kwa wakati huu linagumishwa zaidi kutokana na changamoto mamboleo yaani: vita na dharura mbali mbali ambazo zimesababishwa na mabadiliko ya tabianchi, kiasi cha kuzalisha wimbi kubwa la wakimbizi na watu wasiokuwa na makazi maalum hata katika nchi zao wenyewe. Ni watu wanaoteseka kutokana na umaskini na kwamba, nchi nyingi duniani hazina miundombinu kwa ajili ya kutoa huduma kwa wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi ya kudumu.

Takwimu za mwaka 2020 zinaonesha kwamba, kuna zaidi ya watu milioni 45.7 ambao hawana makazi ya kudumu kutokana na vita na machafuko mbalimbali sanjari na athari za mabadiliko ya tabianchi kutoka katika nchini 61 duniani. Baba Mtakatifu anasema, hivi karibuni Idara ya Wahamiaji na Wakimbizi, Baraza ya Kipapa la Huduma ya Maendeleo Fungamani ya Binadamu limechapisha Mwongozo Wa Shughuli za Kichungaji kwa Watu Wasiokuwa na Makazi Maalum(IDPs). Baba Mtakatifu katika ujumbe wake kwa Mwaka 2020 anapenda kujikita zaidi na changamoto ya watu wasiokuwa na makazi maalum; watu ambao wamesahaulika katika agenda za kitaifa na kimataifa. Baba Mtakatifu mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, tarehe 27 Septemba 2020 ametambua uwepo wa wakimbizi na wahamiaji waliofika kuadhimisha Siku ya 106 ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani.

Wakimbizi na wahamiaji hawa wakiwa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro wamekusanyika na kuzunguka Mnara “Angeli senza saperlo” yaani “Mnara wa Malaika Pasipo kujua”. Mkazo ni kudumisha upendo na udugu wa kibinadamu kwa kuendelea kuwafadhili wageni, maana kwa njia hii wengine wamewakaribisha malaika pasipo kujua: Rej. Ebr. 13: 2. Baba Mtakatifu anakaza kusema, “Kama Kristo Yesu, wanalazimishwa kukimbia”. Hivi ndivyo hali ilivyo kwa wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum. Baba Mtakatifu amewasalimia wote na kuwahakikishia sala na sadaka yake kwa wakimbizi, wanahamiaji pamoja na wale wote wanaowahudumia kwa moyo wa huruma na mapendo. Janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 lisiifanye Jumuiya ya Kimataifa kusahau mahangaiko ya watu sehemu mbali mbali za dunia.

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu, anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuwaangalia kwa jicho la huruma wale wote walioathirika kutokana na ukosefu wa fursa za ajira, waliotelekezwa na kusukumizwa pembezoni mwa jamii na hata wakati mwingine kukataliwa kutokana na janga la Virusi vya Corona, COVID-19. Kristo Yesu alilazimika kukimbilia Misri pamoja na wazazi wake na hivyo kuonja hofu na mashaka kuhusu hatima ya maisha yao. Leo hii, kuna mamilioni ya watu wanaohisi na kuonja hali kama hiyo. Kuna watu wanaokimbia nchi na makazi yao kwa sababu ya baa la njaa, vita, hatari mbali mbali za maisha na hivyo wanatafuta hifadhi, usalama na maisha bora zaidi. Kristo Yesu yuko kati pamoja na watu wote hawa kama hata ilivyo kwa wale wote wanaoteseka kwa baa la njaa, kiu, uchi, wagonjwa, wafungwa na wageni. Waamini wanahamasishwa kuhakikisha kwamba, wanauona Uso wa Kristo Yesu anateseka kati pamoja na watu wote hawa.

Waoneshe ujasiri wa kuwaendea ili kukutana nao, kuwapenda na kuwahudumia kwa niaba ya Kristo Yesu. Watu wasiokuwa na makazi maalum ni fursa nyingine tena ya kukutana na Kristo Yesu, tayari kuwakaribisha, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwashirikisha katika maisha ya jumuiya inayowapatia ukarimu. Kama ilivyokuwa kwa wafuasi wa Emau waliweza kumtambua Kristo Yesu kwa kumega mkate, janga la Virusi vya Corona, COVID-19 liwasaidie waamini kufahamu changamoto wanazokabiliana nazo watu wasiokuwa na makazi maalum. Jambo la msingi ni kuwa karibu nao, ili kuwahudumia kwa huruma na mapendo kama ilivyokuwa kwa yule Msamaria mwema. Na kwa njia hii, wataweza kujenga ujirani mwema. Waamini wajenge utamaduni wa huduma ya upendo kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu, siku ile iliyotangulia kuteswa kwake, wakati wa Karamu ya mwisho, Kristo Yesu alipowaosha Mitume wake miguu.

Ili kupatana kuna haja ya kuwasikiliza kwa makini wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Sanaa ya kusikiliza kilikuwa ni kigezo muhimu sana kwa Jumuiya ya kwanza ya Wakristo na hatimaye, wakaweza kushirikishana amana na utajiri wao, kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu, kuweza kuwalisha watu elfu tano kwa mikate mitano na samaki wawili. Watu wajihusishe kikamilifu ili kuwaendeleza jirani zao kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu na yule mwanamke Msamaria. Janga la Virusi vya Corona, COVID-19, limeonesha umuhimu wa kushirikiana na kushikamana, ili watu waweze kutambua kwamba, wanapendwa na kuthaminiwa na huo ni mwanzo wa ujenzi wa utamaduni wa ukarimu, udugu wa kibinadamu na mshikamano wa kweli. Kuna haja ya kushirikiana ili kujenga Ufalme wa Mungu hapa duniani. Hakuna sababu ya kuwa na: kinzani, mipasuko na wivu usiokuwa na mvuto wala mashiko. Hakuna tena muda wa ubinafsi wala ubaguzi. Ili kuweza kulinda na kudumisha mazingira bora nyumba ya wote anasema Baba Mtakatifu Francisko kuna haja ya kuhakikisha kwamba, kuna kuwepo na ushirikiano na mshikamano wa kimataifa na hata kwa watu mahalia bila kumtenga awaye yote.

Baba Mtakatifu Francisko, mwishoni mwa ujumbe wake kwa Maadhimisho ya Siku ya 106 ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani kwa Mwaka 2020 yanayoongozwa na kauli mbiu “Kama Kristo Yesu, wanalazimishwa kukimbia”. Kuwakaribisha, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwashirikisha watu wasiokuwa na makazi maalum, anapenda kuwakabidhi watu wote wasio kuwa na makazi maalum, chini ya ulinzi na tunza ya Mtakatifu Yosefu, Mlinzi mwaminifu wa Familia Takatifu ya Nazareti. Mtakatifu Yosefu awafariji na kuwalinda wale wote wanaotumbukizwa katika vita, umaskini pamoja na kuyakimbia makazi na nchi zao. Mtakatifu Yosefu awaombee nguvu ya kuweza kudumu, awafariji katika mateso na mahangaiko yao, awape ujasiri katika majaribu wanayokumbana nayo. Mtakatifu Yosefu, awaombee wale wasiokuwa na ajira, ili waweze kupata ajira na makazi salama.

Wakimbizi

 

 

 

 

28 September 2020, 15:48