Tafuta

2020.09.09 Katekesi ya Papa Francisko 2020.09.09 Katekesi ya Papa Francisko 

Papa Francisko:Jibu la kijamii dhidi ya janga ni kuwa na sera za kisiasa zenye mafao ya wote!

Upendo kijamii bila ubinafsi au masilahi ya aina fulani ya mashirika ni muhimu,hasa katika suala la chanjo,ili kuweza kukabiliana na mgogoro wa virusi vya corona.Hili ndilo wazo la Papa katika tafakari ya Katekesi kwa waamini na mahujaji waliofika kwenye uwanja wa Mtakatifu Damasi mjini Vatican.Virusi ambavyo havijui tofauti za kiutamaduni na kisiasa amesema Papa ni muhimu kukabiliwa na upendo bila vizuizi.

Na Sr. Angela Rwezaula - Vatican

Katika mwanzo wa tafakari ya Papa Francisko inayohusu janga la virusi vya corona au covid -19 hasa kwa kutazama matokeo yake katika jamii nzima katika katekesi yake Jumatano tarehe 9 Septemba 2020, kwa waamini na mahujaji waliokaa katika uwanja wa Mtakatifu Damas mjini Vatican ameendeleza mada hiyo makini hasa inayoongzwa na Injili na Kanuni za Mafundisho jamii ya Kanisa. Papa Francisko amesema janga la virusi ambalo tunalipitia wote, tunaweza kuondokana nalo vema ikiwa wote tutatafuta wema wa pamoja; kinyume chake tutaondokana nalo vibaya. Kwa bahati mbaya, tunaona dharura za maslaha kwa upande. Kwa mfano kuna anayetaka kujibinafsisha uwezekano wa suluhisho, kama kesi ya chanjo na baadaye kuwauzia wengine. Baadhi wanatafuta fursa katika hali ya mizozo na migawanyiko ili kupata faida za kiuchumi au kisiasa na kuzua au kuongeza migogoro. Na wengine kwa urahisi tu hawajali lolote la mateso ya wengine, wanapitia mbali na kwenda katika njia zao (Lk 10,30-32). Hawa ni washabiki wa Ponsio Pilato, kwa maana wananawa mikono, Papa amefafanua.

Papa Francisko akiendelea amesema jibu la kikristo katika janga na madhara yake ya mgogoro wa kijamii na kiuchumi, msingi wake ni upendo, awali ya yote upendo wa Mungu ambaye daima wa kwanza kutangulia (1Yh 4,19) kwani akiwa wa  kwanza anatunguliza upendo wake na katika majibu. Yeye anatupenda upendo upeo na tunapo upokea upendo huo wa Mungu, ndipo sasi kweli tunaweza kujibu kwa namna hiyo hiyo inayofanana naye. Akitoa mfano wa wazi amesema:  “Ninapenda na siyo yule anipendaye, kama vile familia, marafiki zangu, kikundi, lakini hata wale ambao hawanipendi, hawanijuhi, au ni wageni, hata wale ambao wananifanya niteseka au ninafikiri ni maadui” (Mt 5, 44). “Mara nyingi inahitajika kubembeleza ni kuzuri zaidi kuliko hoja nyingi, kumbusu, tufikiri, ya msamaha na siyo hoja nyingi za kujitetea. Ni upendo unaojumuisha ambao huponya”, Papa ameshauri. Hii ni hekima ya kikristo. Hii ndiyo tabia ya Yesu. Ndiyo ncha ya juu kabisa ya utakatifu, na tunasema hivyo ni kupenda adui na siyo rahisi. Kwa hakika  ni kupenda wote, wakiwemo hata  maadui, ni vigumu maana hiyo ni sanaa! Amebainisha Papa. Lakini sanaa hiyo inawezekana kujifunza na kuiboresha. Upendo wa kweli unatufanya tuzae matunda na  kuwa huru daima,  ni mpana upendo wa kweli na siyo tu ule wa kupanuka lakini wa kujumuisha. Upendo huo unatunza, unaponya na kutenda mema.

Papa Francisko katika ufafanuzi wake amesema, upendo hakomei hapo unakwenda zaidi ya  vizingiti vya uhusiano kati ya wawili, watu watatu,  marafiki au familia. Upendo unaunganisha kila kitu. Unatambua uhusiano wa kiraia na kisiasa (rej. KKK 1907.1912), unajumuisha uhusiano wa maumbile  asili (Laudato si 231). Kwa kuwa sisi ni wanajamii na wanasiasa, Papa Francisko ameongeza kusema, moja ya kielelezo cha juu cha upendo ni ile ya kijamii na kisiasa, yenye maamuzi kwa ajili ya maendeleo ya binadamu na kwa ajili ya kukabiliana na kila aina ya mgogoro (Ibid., 231). Tunatambua kuwa upendo unazaa familia na urafiki, lakini ni vema kukumbuka kuwa ni matunda hata ya uhusiano wa kijamii, kiutamaduni, kiuchumi na kisiasa kuwezesha ujenzi wa “ustaarabu wa upendo” kama alivyokuwa anapenda kusema Mtakatifu Paulo VI (rej. Ujumbe wa X wa Siku ya Amani duniania, Januari 1977). Virusi vya corona vimetuonesha kuwa wema wa kweli kwa kila mmoja ni wema wa pamoja na kinyume chake, wema wa pamoja ni wema wa kweli wa mtu (KKK 1905 -1906). Afya, licha ya kuwa ya binafsi, pia ni wema wa umma. Jamii iliyo na afya ni ile ambayo inachukuwa wajibu wa kutunza afya ya wote.

Virusi ambavyo havijuhi vizingiti, mipaka au utofauti wa utamaduni, sera za kisiasa, lazima zitambue namna ya kukabiliana na upendo usio na mipaka, vizingiti na utofauti. Upendo huo unaweza kuzaa miundo ya kijamii ambayo inatutia moyo wa kujumuisha walioathirika zaidi na siyo wa kuwabagua Na kwa maana hiyo hao wanatufanya kuelezea vema asili yetu ya kibinadamu na siyo ile mbaya zaidi.  Kwa hakika ikiwa sisi tunapenda, ni wazi kuwa  tunakuwa na msukumo wa ubunifu, imani na mshikamano na hapo ndipo zinapo patikana jitihada za dhati kwa ajili ya wema wa pamoja (Wosia wa Mt. Yohane Paulo II wa Sollicitudo rei socialis 38). Hii ni  sawa kwa ngazi iwe ndogo au kubwa ya jumuiya na hata iwe kwa ngazi ya kimataifa. Hata hivyo Papa Francisko amesisitiza kuwa bado kuna utamaduni wa kibaguzi, kwa maana ya yule nisiye mpenda, kwa wale ambao kwangu hawana faida yoyote katika jamii. Ametoa mfano mmoja kuwa amekutana na mmoja wa wanadoa ambaye ameomba sala kwa  ajili yake na kwa ajili yao, maana wanaye mtoto mlemavu. Papa ameuliza ana miaka mingapi,  wamejibu ni mingi na wanafanya nini? Wamejibu: “Sisi tunamsindikiza na kumsaidia”. Papa Francisko ameongeza kusema: “Maisha yao yote kama wazazi kwa ajili ya mtoto mlemavu. Huo ndiyo upendo! Na maadui wapinzani wa kisiasa, hata kwa mawazo yetu utafikiri ni walemavu wa kisasa, kijamii, lakini fikira tu”. Kwani ni Mungu anayejua  ni nani  kama au hapana… Sisi tunapaswa kuwasindikiza, kuwambeleza, kufanya mazungumzo; tunatakiwa kujenga nao ustaarabu wa upendo. Ndiyo ustaarabu wa kisiasa, kijamii, wa umoja wa ubinadamu wote. Kinyume na hilo vita, migawanyiko, wivu hata vita ndani ya familia, kwa sababu upendo unganishi ni wa kijamii, ni wa kifamilia, ni wa kisiasa… upendo unaenezwa kwa kila kitu”, Papa Francisko amesisitiza.

Kile kifanyikacho katika familia, kifanyikacho katika mitaa, kifanyikacho katika kijiji , na kile kifanyikacho katika mji mkubwa, na katika kimataifa ni sawa sawa! Ndiyo mbegu sawa ambayo inatoa matunda. Ikiwa wewe katika familia na katika mtaa mnaanza na wivu, na mapambano, mwishowe kutakuwa na vita. Badala yake ikiwa unaanza na upendo na kushirikishana upendo na  msamaha, hapo kutakuwa na upendo na msamaha kwa wote. Kinyume chake, ikiwa suluhisho la janga hili lina alama ya ubinafsi, iwe ni ya watu, kampuni au mataifa, labda tutaweza kutoka kwenye virusi vya corona, lakini kiukweli siyo katika shida ya kibinadamu na ya kijamii ambayo virusi vimeangazia na kuonesha. Kwa njia hiyo kuwa makini  Papa anaonya ya kutojenga juu ya mchanga ( Mt 7,21-27)! Ili kujenga jamii iliyo salama, jumuishi, yenye haki na amani, lazima kuitengeneza juu ya mwamba wa wema wa pamoja. Wema wa pamoja ni mwamba. Hiyo ndiyo kazi ya wote, si kwa ajili ya mtaalam mmoja tu. Kila mzalendo ni mhusika wa wema wa pamoja,  amesisitiza Papa.

Mtakatifu Thomas wa Acquinas alikuwa anasema kwamba uhamasishaji wa wema wa pamoja pia ni uwajibu wa haki ambayo inaangukia kwa kila mzalendo. Na kwa upande wa wakristo pia ni utume. Kama alivyokuwa akifundisha Mtakatifu Iginatius wa Loyola, kuwa “kuelekeza jitihada zetu katika wema wa pamoja ni namna ya kupokea na kueneza utukufu wa Mungu”. Kwa bahati mbaya, siasa mara nyingi hazina sifa njema na tunajua kwanini. Papa Francisko amesema:  “Hiyo haina maana kuwa wanasiasa wote ni wakatili, hapana sina maana ya kusema hivyo,  ila ninasema, kwa bahati mbaya siasa mara nyingi hazina sifa nzuri. Lakini hatutakiwi kukata tamaa katika maono haya, badala yake ni kujibu kwa kuonyesha ukweli kwamba sera nzuri zinawezekana kwa kiwango ambacho kila raia  hasa, wale ambao huchukua jukumu la ahadi na nyadhifa za kijamii na kisiasa, kujikita katika msingi wa matendo yao kwa kanuni za maadili na kuongozwa na upendo wa kijamii na kisiasa.  Wakristo kwa namna ya pekee, waamini walei, wanaalikwa kutoa ushuhuda mzuri katika hilo na wanaweza kufanya hivyo, shukrani kwa fadhila ya upendo ili kukuza mwelekeo wake wa kijamii.

Papa Francisko anasema hiki ni kipindi cha kukuza upendo wetu kijamii na ndillo alitaka  kusisitizia kuwa “upendo wetu kijamii ni katika kuchangia wote kuanzia na udogo wetu. Wema wa pamoja unahitaji ushiriki wa wote. Ikiwa mmoja anaweka lake na hakuna hata mmoja anayeachwa nje, basi tutaweza kuanzisha tena uhusiano mzuri katika jamuiya, kitaifa, kimataifa na pia katika maelewano sawa na mazingira” (rej. LS, 236). Na kwa namna ya ishara zetu hata zile za kinyenyekevu zitaweza kuonesha chochote yaani sura ya Mungu tuliyo nayo kwa sababu Mungu ni Utakatifu, Mungu ni upendo. Hii ndiyo tafsiri nzuri zaidi ya Biblia. Anatueleza Mtume Yohane aliyekuwa anapendwa na Yesu: ‘Mungu ni Upendo’. Kwa msaada wake, tutaweza kuponyesha dunia kwa kufanya kazi wote pamoja kwa ajili ya wema wa pamoja na siyo kwa ajili ya faida binafsi, bali kwa ajili ya wema wa pamoja wa wote. Amehitimisha Papa Francisko.

09 September 2020, 14:25