Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 3 Septemba 2020 amekutana na kuzungumza na wataalam wa mazingira wanaoshirikiana na Baraza la Maaskofu Katoliki Ufaransa katika unafsishaji wa Waraka wa "Laudato si". Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 3 Septemba 2020 amekutana na kuzungumza na wataalam wa mazingira wanaoshirikiana na Baraza la Maaskofu Katoliki Ufaransa katika unafsishaji wa Waraka wa "Laudato si".  (� Vatican Media)

Papa: Wongofu wa Kiekolojia na Utunzaji Bora wa Mazingira

Papa Francisko amekazia: Umuhimu wa kujikita katika wongofu wa kiekolojia; Unafishaji wa tunu msingi za Kiinjili za haki, amani na udugu wa kibinadamu pamoja na mwaliko kwa watu wa Mungu kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote kwa sababu madhara yake ni makubwa kwa maisha ya binadamu na ni kikwazo kikuu cha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko Alhamisi tarehe 3 Septemba 2020 amekutana na kuzungumza na wataalam wa mazingira wanaoshirikiana kwa karibu zaidi na Baraza la Maaskofu Katoliki Ufaransa kuhusu utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote “Laudato si”. Baba Mtakatifu katika hotuba yake, amedadavua mambo makuu matatu: Umuhimu wa kujikita katika wongofu wa kiekolojia; Unafishaji wa tunu msingi za Kiinjili za haki, amani na udugu wa kibinadamu pamoja na mwaliko kwa watu wa Mungu kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote kwa sababu madhara yake ni makubwa kwa maisha ya binadamu na ni kikwazo kikuu cha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko, “Laudato si” yaani “yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”, unazungumzia kwa muhtasari mambo yanayotokea katika mazingira; Injili ya Uumbaji; Vyanzo vya mgogoro wa ekolojia vinavyohusiana na watu; Ekolojia msingi; Njia za kupanga na kutenda na mwishoni ni elimu ya ekolojia na maisha ya kiroho.

Baraza la Maaskofu Katoliki Ufaransa kwa kushirikiana na wataalam waliobobea katika ekolojia na utunzaji bora wa mazingira, wameendelea kuutafakari na kuupembua Waraka wa “Laudato si”, ili kusaidi kuragibisha mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote nchini Ufaransa. Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba, binadamu wote wanaishi katika nyumba ya pamoja ambayo kwa sasa inakabiliana na uchafuzi mkubwa na madhara yake yanaonekana kwa wote. Janga la Virusi vya Corona, COVID-19 linaloendelea kumwandama mwanadamu linawakumbusha watu kwamba, wanakabiliana na udhaifu mkubwa katika masuala ya afya; watu wanategemeana na kukamilishana; wanaweza kushirikishana kwa ajili ya maboresho ya leo na kesho ya binadamu na kwamba, uchafuzi mkubwa wa mazingira ni hatari sana kwa maisha ya kijamii na kiutu. Kumbe, kuna haja ya kuanza kudadavua tema ya mazingira katika hatua na mazingira mbalimbali ya maisha ya binadamu, ili kubainisha sera na mikakati ya kisiasa na kiuchumi itakayosaidia mchakato wa maboresho ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.

Kanisa Katoliki kwa upande wake, linataka kujifunga kibwebwe ili kuhakikisha kwamba, linashiriki kikamilifu katika mchakato wa kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote. Kanisa linatambua matatizo, changamoto na fursa zilizopo na kwamba, Kanisa lenyewe halina majibu yaliyokwisha kutayarishwa mapema. Mama Kanisa anatambua na kukiri matatizo na changamoto za kiteknolojia, kiuchumi na kisiasa pamoja na nguvu kubwa inayohitajika katika utekelezaji wake. Kanisa linataka kujikita zaidi katika majiundo ya dhamiri nyofu, ili hatimaye, kuwaelekeza watu wa Mungu katika wongofu wa kiekolojia unaoweza kusimama imara na kupambana na changamoto mamboleo. Wongofu wa kiekolojia ni sehemu ya Injili ya Uumbaji inayobainisha mchango mkubwa unaotolewa na dini mintarafu ekolojia kama msingi wa maendeleo kamili ya mwanadamu. Sayansi na dini, kwa njia zao tofauti za kuufahamu ukweli, zinaweza kuingia kwenye majadiliano ya kina na yenye manufaa kwa pande zote mbili. Rejea. LS, 62.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, kazi ya uumbaji ni kielelezo cha huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu; ni alama ya uzuri na wema wa Muumbaji wake. Kila kiumbe ni kielelezo cha wema wa Mungu na kina nafasi ya pekee kama zawadi ulimwenguni. Kwa Mkristo anapaswa kuheshimu na kutunza kazi ya uumbaji ambayo amekabidhiwa na Mwenyezi Mungu, ili aweze kuilima, kuitunza na kuiendeleza kadiri ya uwezo wake. Mwanadamu amepewa dhamana ya kusimamia kazi ya uumbaji na wala si mtawala anayeweza kuitumia kama chanzo tu cha faida na masilahi binafsi. Kazi ya uumbaji haina budi kutumiwa kwa kufuata kanuni za maelewano, haki, udugu wa kibinadamu na amani kama ambavyo Kristo Yesu amewaagiza wafuasi wake. Rej. LS, 82. Kinyume chake, ikiwa kama kazi ya uumbaji itatumiwa vibaya, matokeo yake ni kuibuka kwa matabaka makubwa, dhuluma na vurugu dhidi ya watu walio wengi.

Mtakatifu Yohane Paulo II anasema, mwanadamu amepewa ardhi na Mwenyezi Mungu ili aweze kuilima, kumbe, kuna haja ya kuheshimu nia thabiti ya Mungu Muumbaji mintarafu kanuni maadili na utu wema, kwa sababu mambo yote yanaingiliana. Tabia ya kutojali, ubinafsi, tamaa mbaya, kiburi na jeuri ya kudhani kwamba, binadamu ni mtawala wa kazi ya uumbaji imepelekea uharibifu mkubwa wa mazingira pamoja na matumizi mabaya ya rasilimali na utajiri wa dunia. Matokeo yake ni ongezeko la balaa la umaskini, kazi za suluba wanazofanyishwa wanawake na watoto dhidi ya utu, heshima na haki zao msingi; sanjari na kubomolewa kwa kanuni bora za maisha ya ndoa na familia. Ni katika mantiki hii, utamaduni wa kifo umejipenyeza dhidi ya Injili ya uhai, ambamo maisha yanapaswa kulindwa tangu mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake, hadi mauti ya kawaida inapomfika kadiri ya mpango wa Mungu.

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kudadavua kwa kusema kwamba, iwapo migogoro iliyopo ya kiekolojia ni ishara ndogo ya usasa wa kitamaduni, kimaadili na kiroho, hakutakuwepo na muafaka wa uhusiano wa mwanadamu na mazingira bila kuwa na mwafaka msingi wa mahusiano ya kibinadamu. Rej. LS, 119. Ili kuweza kupata mahusiano mapya kati ya binadamu na mazingira, kuna haja ya kuwa na toba na wongofu wa kiekolojia, kama tiba ya moyo wa mwanadamu anayetamani kuganga na kuuponya ulimwengu kutokana na kinzani za kijamii na kimazingira. Baba Mtakatifu anapenda kuwatia shime wataalamu wa mazingira kujifunga kibwebwe kulinda na kutunza mazingira. Hata kama hali ya mazingira inaonekana kuwa ni tete sana, lakini kama Wakristo bado wana matumaini, kwa kumwangalia Kristo Yesu, Neno wa Mungu aliyefanyika mwili na kuja kuwatembelea na kukaa kati ya waja wake, ili kuwaganga na kuwaponya, kwa kuwakirimia amani na ulinganifu ambao walikuwa wameupoteza kati yao wenyewe na kati ya binadamu na mazingira. Mwishoni mwa hotuba yake, Baba Mtakatifu Francisko anasema, Mwenyezi Mungu hawezi kuwatelekeza, hawezi kuwaacha wakiwa pweke, kwani Yeye ameungana kabisa na dunia na upendo wake unawahimiza kutafuta njia mpya za kusonga mbele.

Papa: Ufaransa

 

 

03 September 2020, 15:00