Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema: Ijumaa tarehe 4 Septemba 2020 kufunga na kusali kwa ajili ya kuombea ustawi, maendeleo ya watu wa Mungu Lebanon. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema: Ijumaa tarehe 4 Septemba 2020 kufunga na kusali kwa ajili ya kuombea ustawi, maendeleo ya watu wa Mungu Lebanon. 

Papa: Siku ya Kufunga Na Kusali kwa Ajili ya Lebanon: 4 Sept. 2020

Baba Mtakatifu anatoa wito kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema Ijumaa tarehe 4 Septemba 2020 kufunga na kusali kwa ajili ya kuombea amani, ustawi na maendeleo ya watu wa Mungu nchini Lebanon, kama alivyofanya Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 1989. Kanisa linatambua hatari kubwa inayoinyemelea nchi ya Lebanon. Nguvu ya sala na imani ni muhimu sana!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Katekesi yake inayoongozwa na kauli mbiu “Uponyaji wa Ulimwengu”, Jumatano tarehe 2 Septemba 2020, kwenye Uwanja wa Jengo la Mtakatifu Damas lililoko mjini Vatican, amejielekeza zaidi katika mshikamano unaoratibiwa na fadhila ya imani. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu ametoa wito kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema Ijumaa tarehe 4 Septemba 2020 kufunga na kusali kwa ajili ya kuombea amani, ustawi na maendeleo ya watu wa Mungu nchini Lebanon, kama alivyofanya Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 1989, miaka thelathini iliyopita. Kutokana na matatizo na changamoto zinazofahamika na wananchi wa Lebanon, Kanisa linatambua hatari kubwa inayoinyemelea nchi ya Lebanon. Kamwe Lebanon haipaswi kuachwa peke yake iogelee katika upweke. Kwa takribani miaka 100 iliyopita, Lebanon imekuwa ni nchi ya matumaini; mahali ambapo wananchi wake wamekuwa makini kulinda na kutunza imani yao kwa Mwenyezi Mungu, kiasi cha kushuhudia Lebanon inakuwa ni mahali pa maridhiano, heshima na utulivu, ikilinganishwa na nchi nyingine jirani. Lebanon ni kielelezo cha uhuru na mfano bora wa kuigwa.

Kwa kuzingatia ustawi na maendeleo ya Lebanon na Ulimwengu katika ujumla wake, Baba Mtakatifu Francisko anasema, haiwezekani kabisa kwa Jumuiya ya Kimataifa kufumba macho kiasi kwamba, amana na utajiri wote wa Lebanon upotee na kutoweka katika uso wa dunia. Baba Mtakatifu anapenda kuchukua fursa hii, kuwahamasisha watu wa Mungu nchini Lebanon kujifunga kibwebwe ili kutafuta nguvu na ari mpya itakayowawezesha kuanza upya kuijenga nchi yao. Huu ni mwaliko kwa viongozi wa kisiasa na kidini kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Lebanon, huku wakizingatia ukweli na uwazi katika mchakato mzima wa ukarabati wa nchi yao, kwa sasa na kwa siku za usoni. Jumuiya ya Kimataifa inapaswa pia kuunga mkono juhudi za Lebanon za kutaka kujiondoa katika kipeo hiki ambacho kimeipekenya nchi hii, kiasi cha wananchi wake kukata tamaa. Kuna hatari kubwa kwa Lebanon kutumbukia katika machafuko ya kisiasa yanayoendelea kujionesha kwenye Ukanda wa Mashariki ya Kati.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, wananchi wa Lebanon wameguswa na kutikiswa sana na mlipuko wa Lebanon ambao umesababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Huu ni wakati wa kuanza upya kwa ujasiri, ari na moyo mkuu. Katika kipindi hiki kigumu, watu wa Mungu waimarishwe kwa nguvu ya imani na sala, daima wakiendelea kupyaisha ndoto ya nchi yao inayopendeza kwa kujikita katika ustawi na maendeleo fungamani ya wananchi wake. Viongozi wa Kanisa wawe mstari wa mbele kuonesha dira kwa waamini wao; kwa kuwa na ari na mwamko wa shughuli za kitume, kwa kujikita katika ufukara wa Kiinjili unaofumbatwa katika fadhila ya unyenyekevu, ili kuwashika mkono, watu wa Mungu wanaoteseka na sasa wanataka kusimama tena na kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu. Watu wa Mungu katika ujumla wao, wawe ni vyombo na mashuhuda wa haki, amani na maridhiano, tayari kusimama kidete kulinda ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; kwa kujenga utamaduni wa watu kukutana; kwa kuishi katika hali ya amani, utulivu na udugu wa kibinadamu; chachu muhimu sana katika mchakato wa upyaisho wa mafao ya wengi.

Ni katika hali na mazingira kama haya, wataweza kuwa na uhakika wa mwendelezo wa uwepo wa Ukristo pamoja na mchango wa Lebanon katika Nchi za Kiarabu na Ukanda wa Mashariki ya Kati katika ujumla wake. Udugu wa kibinadamu ni utambulisho wa waamini wa dini na madhehebu mbali mbali nchini Lebanon.Ni katika muktadha huu Baba Mtakatifu Francisko anasema, anapenda kuwaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, Ijumaa tarehe 4 Septemba 2020 kufunga na kusali kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Lebanon. Baba Mtakatifu anasema anamtuma Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwenda nchini Lebanon kama kielelezo cha mshikamano wa dhati na uwepo wake wa karibu miongoni mwa watu wa Mungu nchini Lebanon. Hii ni siku maalum ya kufunga na sala kwa ajili ya Beirut na Lebanon katika ujumla wake. Kanisa linaendelea kuonesha uwepo wake wa karibu kwa hali na mali kama sehemu ya vinasaba vyake kama kielelezo cha Injili ya upendo na mshikamano.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini wa Makanisa na Madhehebu mbalimbali ya Kikristo kujiunga pamoja naye katika siku hii maalum kwa ajili ya Lebanon, kadiri ya taratibu na watakavyoona inafaa na kupendeza. Baba Mtakatifu anahitimisha mwaliko wake kwa ajili ya siku ya kufunga na kusali ili kuiombea Lebanon kwa kuwaweka watu wote wa Mungu nchini humo chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria wa Harissa, ili aweze kupokea machungu na matumaini ya watoto wake kutoka Lebanon. Awaombee wale wote wanaolia na kuomboleza; awaombee nguvu na ujasiri wote waliopoteza ndugu, jamaa, makazi na sehemu ya mali zao. Bikira Maria wa Harissa awaombee wote hawa, ili Lebanon iweze kustawi, kuchanua na kutoa harufu nzuri tena kwa watu wa Mungu Ukanda wote wa Mashariki ya Kati.

Wakati huo huo, Padre mmoja kutoka Lebanon, amemshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa uwepo wake wa karibu pamoja na kuwatia shime kusonga mbele na kuendelea kuishi nchini Lebanon. Kwa sasa hali ni tete sana, kwani takwimu zinaonesha kwamba, kuna Wakristo zaidi ya laki tatu ambao wameonesha hati za kutaka kuhama kutoka nchini Lebanon. Kwa hakika, Lebanon kwa sasa inahitaji mshikamano wa Kanisa na kwa namna ya pekee, kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko kama kielelezo cha upendo wa udugu wa kibinadamu. Ni matumaini ya watu wa Mungu nchini Lebanon kwamba, iko “siku isiyokuwa na jina”, Baba Mtakatifu ataweza kuwatembelea na kuwaimarisha katika imani, matumaini na mapendo kwa Mungu na Kanisa lake.

Papa: Lebanon

 

 

03 September 2020, 09:11