Tafuta

Mfuko wa Benki ya Dawa Kimataifa kwa Mwaka 2020 unaadhimisha kumbukumbu ya miaka 2020 tangu kuanzishwa kwake kwa kukutana na Baba Mtakatifu Francisko. Mshikamano wa huduma ya dawa! Mfuko wa Benki ya Dawa Kimataifa kwa Mwaka 2020 unaadhimisha kumbukumbu ya miaka 2020 tangu kuanzishwa kwake kwa kukutana na Baba Mtakatifu Francisko. Mshikamano wa huduma ya dawa! 

Papa Francisko: Miaka 20: Mfuko wa Benki Ya Dawa Kimataifa

Papa Francisko amegusia: Umaskini unaopelekea hata watu kukosa uwezo wa kiuchumi wa kununua dawa; umuhimu wa tafiti za kisayansi ili kutoa suluhu ya changamoto mpya na zile za zamani. Madhara ya Virusi vya corona- COVID-19 na kwamba, maadhimisho ya Siku ya Kuchangia Dawa ni kielelezo cha ukarimu na ujirani mwema unaoweza kusaidia mchakato wa maboresho ya jamii.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mfuko wa Benki ya Dawa Kimataifa, “Fondazione Banco Farmaceutico"  mwaka 2020 unaadhimisha kumbukumbu ya Miaka 20 tangu kuanzishwa kwake. Hiki ni kipindi cha kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa wema na ukarimu wake wote aliowatendea. Tangu kuanzishwa kwake, takwimu zinaonesha kwamba, Mfuko wa Benki ya Dawa Kimataifa umekusanya dawa kiasi cha paketi 14, 417, zenye thamani ya Euro milioni 127, 202. Dawa hizi zimechangwa na makampuni pamoja na wadau mbalimbali wapatao 1, 859 na hivyo kuweza kuwahudumia wagonjwa, maskini na wasiojiweza milioni 473, 000. Siku ya kukusanya dawa nchini Italia ilikuwa ni kuanzia tarehe 4 hadi 10 Februari 2020 na kilele chake kilikuwa ni Jumamosi tarehe 8 Februari 2020. Mfuko wa Benki ya Dawa Kimataifa, “Fondazione Banco Farmaceutico"  katika kilele cha maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 20 tangu kuanzishwa kwake, wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 19 Septemba 2020 hapa mjini Vatican.

Baba Mtakatifu katika hotuba yake amezungumzia umaskini unaopelekea hata watu kukosa uwezo wa kiuchumi wa kununua dawa; umuhimu wa tafiti makini za kisayansi ili kutoa suluhu ya changamoto mpya na zile za zamani. Baba Mtakatifu amegusia pia madhara ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya corona- COVID-19 na kwamba, maadhimisho ya Siku ya Kuchangia Dawa ni kielelezo cha ukarimu na ujirani mwema unaoweza kusaidia mchakato wa maboresho ya jamii. Baba Mtakatifu anasema, kumbukumbu ya miaka ishirini tangu kuanzishwa kwa Mfuko wa Benki ya Dawa Kimataifa, “Fondazione Banco Farmaceutico" ni muda wa kuwapongeza wadau wote pamoja na kumshukuru Mwenyezi Mungu, kwa sababu leo hii Mfuko huu umevuka mipaka ya Italia na sasa ni Mfuko wa Benki ya Dawa Kimataifa. Maskini wasiokuwa na uwezo hata wa kujinunulia dawa, wanajikuta katika hali ngumu zaidi, inayoweza kuhatarisha hata maisha yao. Kuna watu wanashindwa kupata dawa kwa kukosa fedha na wakati mwingine, dawa nyingine hazipatikani katika maeneo mengine ya dunia.

Mwelekeo huu unaweka mgawanyo mkubwa kati ya mataifa na watu katika ujumla wao. Kimaadili, ikiwa kama dawa inaweza kuponya ugonjwa fulani, basi, dawa hii inapaswa kutumiwa na wagonjwa wote, vinginevyo, huo unakuwa ni mwanzo wa ukosefu wa haki ya kupata dawa muafaka. Kuna maelfu ya watu wanaoendelea kupoteza maisha yao kwa kukosa dawa, ambayo inapatikana sehemu nyingine za dunia. Hizi ndizo athari za ulimwengu wa utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine. Baba Mtakatifu anasema, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuanzisha mchakato wa utandawazi wa tiba kwa wagonjwa wote, yaani kwa kuwapatia nafasi wagonjwa wote kupata dawa muafaka, ili kuokoa maisha ya watu wengi duniani ambao wanapoteza maisha kwa kukosa dawa katika maeneo yao, hata kama dawa hii inapatikana sehemu nyingine za dunia. Ili kuweza kufikia hatua hii, kuna haja ya kujizatiti kikamilifu kwa kuwa na sera zinazowashirikisha wadau wote.

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, maendeleo ya sayansi yatasaidia mchakato wa kupata suluhu ya matatizo na changamoto za zamani na zile zinazoibuka kwa wakati huu. Tafiti makini za kisayansi ni tunu adhimu na mfano bora zaidi unaoonesha jinsi ambavyo ujuzi na akili ya mwanadamu vinavyofanya kazi katika mchakato wa kuganga na kutibu magonjwa yanayomwandama mwanadamu. Makampuni yanayosaidia tafiti makini za kisayansi, utengenezaji pamoja na ugavi wa dawa hayana budi kujielekeza pia katika ugawaji sawa wa dawa miongoni mwa Jumuiya ya Kimataifa. Kwa upande wao, wafamasia wanaitwa kutekeleza dhamana na huduma ya tiba kwa wagonjwa kwa kuonesha ujirani mwema kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Watambue kwamba, kwa njia ya sayansi na kwa kusukumwa na dhamiri nyofu watatekeleza dhamana kwa ajili ya mafao ya mtu mzima. Serikali na taasisi zake zitambue kwamba, kwa njia ya sera na huduma ya kifedha, wanapaswa kujenga na kudumisha ulimwengu unaosimikwa katika msingi wa haki, kiasi kwamba, hata maskini wanaweza kupata huduma msingi katika maisha yao.

Uzoefu na mang’amuzi ya janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, umethibitisha kwamba, kwa hakika, hii imekuwa ni dharura ya kiafya. Takwimu zinaonesha kwamba, zaidi ya watu milioni moja wamekwisha kupoteza maisha kutokana na Virusi vya Corona, COVID-19. Madhara yake yanaendelea kujionesha kutokana na kuyumba kwa uchumi kitaifa na kimataifa, hali ambayo inaendelea kuzalisha maskini wengi duniani pamoja na familia nyingi kujikuta kwamba, zinaingia katika hali ngumu na tete katika maisha. Pamoja na huduma ya huruma na upendo inayotolewa kwa maskini, kuna haja pia kujielekeza zaidi katika mapambano dhidi ya umaskini wa dawa, kwa kuhakikisha kwamba, chanjo mpya zinawafikia watu wengi zaidi. Baba Mtakatifu Francisko anasema kwa uchungu mkubwa kwamba, litakuwa ni jambo la kusikitisha sana, ikiwa kama chanjo ya Corona, COVID-19 itatoa kipaumbele cha kwanza kwa matajiri zaidi duniani au chanjo hii ikabinafsishwa na kumilikiwa na taifa fulani, badala ya kuwa ni kwa ajili ya mafao ya wengi.

Mwishoni, Baba Mtakatifu amewapongeza wanachama na wadau wote wa Mfuko wa Benki ya Dawa Kimataifa, “Fondazione Banco Farmaceutico"   kwa ajili ya huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Siku ya Kukusanya Dawa ni kielelezo cha ukarimu pamoja na matumizi sahihi ya mali za dunia kwa ajili ya maboresho ya jamii na ushuhuda wa upendo kwa jirani, kama mwaliko kutoka katika Injili ya Kristo Yesu. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko amewapatia wote baraka zake za kitume! Amewapongeza wanachama wa Mfuko huu ambao wanatoka katika dini na imani mbalimbali, lakini wote watambue kwamba ni ndugu na watoto wa Mwenyezi Mungu. Anawashukuru kwa kazi na ukarimu wao na anawaomba waendelee kumkumbuka na kumsindikiza kwa njia ya sala na sadaka zao katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Papa: Benki ya Dawa
19 September 2020, 16:21